Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha muafaka wa usitishaji mapigano na kuachilia mateka Gaza

Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.
WHO
Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.

UN yakaribisha muafaka wa usitishaji mapigano na kuachilia mateka Gaza

Amani na Usalama

Muafaka uliofikiwa jana jioni wa kuwaachilia mateka waliochukuliwa wakati wa shambulizi la Hamas huko Israel Kusini Oktoba 7 umekaribishwa na  Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye amesema Umoja huo uko tayari kutumia hatua hiyo njema kwa ajili ya masuala ya kibinadamu.

Kwa hakika muafaka huo ni habari njema ambayo imepokelewa kwa mikoni miwili na mashirika karibu yote ya Umoja wa Mataifa na wahudumu wa kibinadamu huku Katibu Mkuu Guterres kupitia taarifa yake iliyotolewa leo akisema “Ni hatua muhimu kuelekea kunakostahili na Umoja wa Mataifa utasaidia kwa kila hali kufanikisha hilo lakini mengi zaidi yanahitajika kufanywa.”

Tor Wennesland ambaye ni mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati ameunga mkono kauli hiyo ya Guterres akikaribisha usitishaji huo wa mapigano Gaza wa saa 96 au siku nne.

Amesisitiza kwamba “Usitishaji maiugano huo lazima utumiwe kikamilifu kuwezesha kuachiliwa kwa mateka na kushughulikia mahitaji makubwa ya Wapalestina Gaza”

Watu wanatafuta hifadhi katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)
WHO
Watu wanatafuta hifadhi katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)

Bahari ya mahitaji

Kufuatia tangazo la siku nne la kusitisha mapigano Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limetoa wito mpya wa upatikanaji salama na usiozuiliwa wa fursa za kibinadamu katika Ukanda huo. 

"Mapigano yanahitaji kukomeshwa ili tuweze kuongeza hatua zetu za misaada haraka," amesema Dkt. Ahmed Al-Mandhari, Mkurugenzi wa WHO wa Kanda ya Mediterania ya Mashariki. 

Ameongeza kuwa "Hatuwezi kuendelea kutoa matone ya misaada huko Gaza katika bahari yamahitaji."

Wakati huo huo, WHO imesema uhamishaji mpya wa wagonjwa unaendelea katika hospitali ya Al-Shifa ya Gaza City, na zaidi kufuata kaskazini mwa Gaza.

Mgogoro usio na maana

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas unapaswa kuanza ndani ya saa 24 baada ya kutangazwa kwake. 

Katika taarifa yake, Bwana Wennesland alikaribisha juhudi za Serikali za Misri, Qatar na Marekani katika "kuwezesha makubaliano hayo”.

Mwakilishi wa WHO katika eneo linalokaliwa la Palestina, Dkt. Richard Peeperkorn, amesema kuwa habari zozote za kusitishwa uhasama kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka zinakaribishwa, lakini mwisho wa kweli wa mapigano unahitajika.

Katika mkutano wa WHO huo na waandishi wa habari mjini Cairo, Dkt. Al-Mandhari ametoa wito wa "kusitishwa wa usitishaji wa kudumu wa mapigano na kusema kwamba pande zinazohusika katika mzozo huo zinapaswa kuweka ustawi na afya ya watu wao kama kipaumbele chao cha kwanza".

Afisa huyo pia ameongoza dakika moja ya kimya kumuenzi mfanyakazi wa WHO Dima Alhaj, aliyeuawa huko Gaza jana Jumanne, pamoja na jamaa wengine wengi. "Tunapohuzunika, tunakumbushwa juu ya hali ya isio na maana ya mzozo huu na ukweli kwamba huko Gaza leo hakuna mahali palipo salama kwa raia, ikiwa ni pamoja na wenzetu wa Umoja wa Mataifa," alisema.

Tangu kuanza kwa Israel kulipiza kisasi mauaji ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 kusini mwa Israel na mateka 240 kutekwa nyara, wafanyakazi 108 wa Umoja wa Mataifa wameuawa katika Ukanda huo.

 Dima Alhaj mfanyakazi wa WHO aliyeuawa Gaza pamoja na mwanaye wa miezi 6, mumewe na kaka zake wawili
WHO
Dima Alhaj mfanyakazi wa WHO aliyeuawa Gaza pamoja na mwanaye wa miezi 6, mumewe na kaka zake wawili

Uhamisho mpya wa hospitali unaendelea

Dkt. Peeperkorn leo amesema kwamba ujumbe huo ulikuwa unaendelea kwa uratibu wa karibu na washirika wa kibinadamu wa Hilali Nyekundu ya Palestina na madaktari wasio na mipaka MSF, kuwahamisha wagonjwa na wahudumu wa afya waliosalia Al-Shifa.

Operesheni  hiyo inafuatia uhamishaji wa awali baina ya mashirika wa watoto 31 wanaozaliwa kabla ya wakati uliofanywa siku ya Jumapili. 

Kati ya wagonjwa 220 na wahudumu wa afya 200 ambao bado wako hospitalini, wanaopewa kipaumbele watakuwa wagonjwa 21 wa dialysis, wagonjwa 29 walio na majeraha ya uti wa mgongo na wale walio katika uangalizi maalum, amesema Dkt. Peeperkorn.

Pia amefahamisha kwamba wakati huo huo, shirika la afya la Umoja wa Mataifa limepokea maombi ya kuhama kutoka hospitali nyingine tatu kaskazini mwa Gaza ambazo ni hospitali ya Al-Ahli Arab, hospitali ya Al-Awda na hospitali ya Indonesia, na mipango yalikuwa yanaendelea, na WHO na washirika wake bila kuacha juhudi zozote za "kuhakikisha kuwa hii inafanyika katika siku zijazo".

Ameeleza kuwa uhamishaji huo unafanywa tu kwa ombi na kama suluhu ya mwisho.

Mashambulizi dhidi ya huduma ya afya

Dkt. Al-Mandhari amesema amesikitishwa na ukweli kwamba hata hospitali hazijalindwa kutokana na majanga ya mzozo wa Gaza. 

WHO imeandika mashambulizi 178 dhidi ya huduma za afya katika Ukanda huo yamefanyika tangu Oktoba 7 na kati ya hospitali 36 zilizopo hospitali 28 hazifanyi kazi tena.

Hospitali nane zilizosalia, zote za kusini, "zimezidiwa uwezo", amesema, na juhudi zote lazima zifanywe ili zifanye kazi na kupanua wigo wa uwezo wao wa vitanda.

Eneo la Gaza lilikuwa na vitanda 3,500 vya hospitali kabla ya kuongezeka kwa machafuko ya sasa na idadi hiyo sasa iko chini ya 1,400.

Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini misaada ya kibinadamu, ikiongozwa na WHO ilifika katika Hospitali ya Al-Shifa kaskazini mwa Gaza ili kutathmini hali ilivyo.
WHO
Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini misaada ya kibinadamu, ikiongozwa na WHO ilifika katika Hospitali ya Al-Shifa kaskazini mwa Gaza ili kutathmini hali ilivyo.

Msaada zaidi unahitajika

Mtazamo wa kusitishwa kwa mapigano umeibua matumaini ya kuboreshwa kwa upatikanaji msaada kwa raia wa Gaza waliokata tamaa na ongezeko la kiasi cha misaada inayokuja.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA, malori ya misaada ambayo yamekuwa yakiingia Gaza tangu tarehe 21 Oktoba yanawakilisha takriban asilimia 14 tu ya kiasi cha kila mwezi cha usafiri wa kibinadamu na wa kibiashara uliokuwa unafika katika eneo hilo kabla ya kuanza kwa uhasama uliopo, hii haijumuishi mafuta, ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku kabisa na mamlaka ya Israel hadi siku chache zilizopita.

OCHA imesema siku ya Jumanne, lita 63,800 za mafuta ziliingia Gaza kutoka Misri, kufuatia uamuzi wa Israel kuanzia tarehe 18 Novemba "kuruhusu kuingia kila siku kwa kiasi kidogo cha mafuta kwa ajili ya shughuli muhimu za kibinadamu". 

Mafuta yanayoingia yanasambazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la masaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, kusaidia usambazaji wa chakula na uendeshaji wa jenereta katika hospitali, vifaa vya maji na vyoo, makazi na huduma nyingine muhimu.

Hakuna chakula kaskazini

Habari za makubaliano ya kusitisha mapigano zilikuja huku kukiwa na hofu ya njaa kuenea kaskazini, eneo ambalo limezuiwa kutoka kusini na operesheni za kijeshi za Israeli. 

Mashirika ya kibinadamu hayajaweza kutoa msaada huko tangu tarehe 7 Novemba. Kutokana na ukosefu wa vifaa vya kupikia na mafuta, "watu wanaamua kutumia mboga mbichi chache au matunda ambayo hayajaiva ambayo yamesalia kwao", OCHA imesema, huku kukiwa hakuna maduka ya kuoka mikate yaliyofunguliwa.

OCHA pia imeonya kwamba mifugo kaskazini "inakabiliwa na njaa na hatari ya kifo kutokana na uhaba wa malisho na maji na mazao yanazidi kutelekezwa".

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limesema siku 10 zilizopita kwamba linawachukulia raia wote wa Gaza kuwa na uhaba wa chakula.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema tangu kuanza kwa machafuko ya sasa watu 191 wanaopata hifadhi katika vituo vyake wameuawa na wengine 798 kujeruhiwa huku shule mbili za UNRWA zikisambaratishwa kabisa na milipuko. Na jana tu limesema shambulio kwenye hospitali ya Al-Awda Kaskazini mwa Gaza limekatili maisha ya watu 4 wakiwemo madaktari 3 na kumjeruhi muuguzi.

Familia zinapata makazi katika hospitali ya Al shifa ( Maktaba)
© Bisan Ouda for UNFPA
Familia zinapata makazi katika hospitali ya Al shifa ( Maktaba)

Mahitaji ya afya ya akili yanaongezeka kwa kasi

Dhiki inayosababishwa na mabomu ya mara kwa mara, kuhama na msongamano mkubwa wa watu katika makazi ya UNRWA, ambapo baadhi jumla ya watu 400 wanapaswa kutumia choo kimoja, vimekuwa vikiathiri sana kisaikolojia wakazi wa Gaza. 

OCHA imesema kuwa mahitaji ya huduma ya afya ya akili yanaongezeka, hasa kwa walio hatarini zaidi ambao ni watoto, watu wenye ulemavu na wale walio na hali ngumu.

"Huduma chache tu za msaada wa kisaikolojia na msaada wa kwanza wa kisaikolojia zinatolewa katika baadhi ya makazi kote Gaza ambapo wahusika wa ulinzi wanapata hifadhi na wana uwezo wa kutoa huduma, limesema shirika la OCHA. 

Huduma nyingi zimeripotiwa kuharibiwa na wafanyikazi wengi hawawezi kufanya kazi.

OCHA pia imeangazia ongezeko la harakati za watoto wasio na wazazi au walezi na familia zilizotengwa lilisema kuwa mpango wa mashirika ya kimataifa unaandaliwa ili kukabiliana na hali hii, ikiwa ni pamoja na usajili wa kesi.