Mgogoro wa ufadhili Gaza: Shughuli za misaada ziko hatarini
Mgogoro wa ufadhili Gaza: Shughuli za misaada ziko hatarini
"Ni vigumu kufikiria kwamba watu wa Gaza watanusurika katika mgogoro huu bila UNRWA... tumepokea ripoti kwamba watu katika eneo hilo wanasaga chakula cha ndege ili kutengeneza unga," amesema Thomas White, Mkurugenzi wa Masuala ya UNRWA huko Gaza na Naibu Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.
Bwana White akitaja mahitaji "makubwa" ambayo sasa yanawakabili zaidi ya watu milioni mbili katika eneo hilo ambao wanategemea UNRWA kama mfadhili wao kamili wa maisha yao, alionya kwamba hali mbaya ya kibinadamu ambayp ipo tayari inaweza kuwa mbaya zaidi kufuatia uamuzi wa nchi wafadhili 16 kusitisha ufadhili wao kwa shirika hilo.
Shutuma
Kuna shutuma kuwa baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walishirikiana na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas wakati wa mashambulizi yake ya kigaidi kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, 2023 ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.
Chombo cha juu zaidi cha uchunguzi cha Umoja wa Mataifa tayari kinafanya uchunguzi juu ya madai hayo kwa ombi la UNRWA, ambayo ina jukumu muhimu huko Gaza kama shirika kubwa zaidi la kibinadamu likiwa na wafanyakazi 13,000, na zaidi ya 3,000 wanaendelea kufanya kazi mpaka sasa.
Muda mfupi baada ya Kamishna Jenerali wa UNRWA Philippe Lazzarini kutangaza kuwafuta kazi mara moja wafanyakazi wanaokabiliwa na tuhuma hizo na uamuzi wake wa kuhusisha Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Uangalizi wa Ndani mjini New York, nchi kadhaa wafadhili zimesitisha ufadhili wa dola milioni 440.
Wito wa Katibu Mkuu Guterres
"UNRWA ndio uti wa mgongo wa kujibu changamoto zote za kibinadamu huko Gaza. Ninatoa wito kwa Nchi Wanachama wote kuhakikisha kwamba UNRWA inaendelea na kazi ya kuokoa maisha,” alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, wakati akihutubia Kamati ya Haki za Palestina siku ya Jumatano.
Wahudumu wa kibinadamu wameonya kwamba watu wengi wameendelea kuhama kutafuta hifadhi huko kusini wakati mashambulizi ya Israel hasa katika mji wa kusini Khan Younis yakiendelea.
“Rafah imekuwa bahari ya watu wanaokimbia mashambulizi ya mabomu,” alisema Bw. White, wakati UNRWA ikiripoti kwamba makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makombora na mapigano huko Khan Younis wiki hii tu, zaidi ya watu milioni 1.4 tayari wamejazana katika mkoa wa kusini wa Rafah.
“Wengi wanaishi katika majengo ya kubahatisha, mahema au nje na sasa wanahofia kwamba hawatapokea tena chakula au usaidizi mwingine wa kibinadamu kutoka kwa UNRWA," ilisema taarifa ya UNRWA
Ikiashiria vikwazo vya muda mrefu vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza tangu vita vilipozuka tarehe 7 Oktoba, UNWRA ilitoa onyo jipya kwamba njaa “inakuja’.
“Tunaendelea kuratibu na Jeshi la Israel ili kuweza kwenda kaskazini, lakini hili kwa kiasi kikubwa limekataliwa,” alisema Bw. White. “Misafara yetu inaporuhusiwa kwenda eneo hilo, watu hukimbilia kwenye lori ili kupata chakula na mara nyingi hula papo hapo.”