Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya nusu ya watu Gaza kukosa chakula ifikapo Juni:UNRWA

Zaidi ya watu milioni moja sawa nusu ya watu wote Gaza wanategemea msaada wa chakula kutoka kwa jamii ya kimataifa (maktaba 2010)
ECHO/Fadwa Baroud
Zaidi ya watu milioni moja sawa nusu ya watu wote Gaza wanategemea msaada wa chakula kutoka kwa jamii ya kimataifa (maktaba 2010)

Zaidi ya nusu ya watu Gaza kukosa chakula ifikapo Juni:UNRWA

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya watu milioni moja sawa na nusu ya watu wote Gaza huenda wasiwe na mlo kabisa ifikapo mwezi Juni mwaka huu limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNRWA iliyotolewa leo wakati huu ambao Waislamu wote kote duniani wako katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao mara nyingi huambatana na shamra za futari, Ukanda wa gaza zaidi ya watu wake wanategemea msaada wa chakula kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, na endapo UNRWA haitopata fedha za ziada takriban dola milioni 60 ifikapo Juni, basi uwezo wa shirika hilo kuendelea kutoa misaada kwa wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Kipelestina Gaza , wakiwemo 620,000 wanaohesabiska kuwa ni hohehahe wasiojiweza hata kumudu mahitaji ya msingi ya chakula na kulazimika kuishi kwa chini ya dola 1.6 kwa siku na pia watu wengine 390,000 masikini, watakabiliwa na athari kubwa. Akisisitiza kuhusu hali hiyo mbele ya waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis hii leo  Maththias Schmale , mkurugenzi wa operesheni wa UNRWA amesema “Watu hawana mwelekeo, asilimia 53 ya watu wanaopaswa kuwajiriwa hawana ajira na matumaini ni kidogo sana ya kupata ajira, na Gaza ni Zaidi ya asilimia 50. Asilimia 80 ya wakimbizi ambao wameorodheshwa kwetu wanaishi chini ya kiwango cha umasikini na wanategemea kwetu msaada wa chakula.”

Ufadhili wa UNRWA

Ripoti imeongeza kuwa UNRWA inafadhiliwa kwa asilimia kubwa na michango ya kujitolea na hivi sasa fedha zinazotolewa ni ndogo kuliko mahitaji . Ikilinganishwa na mwaka 2000 ambapo kulikuwa na wakimbizi laki 8 tu wanaotegemea msaada wa UNRWA hivi sasa ni watu Zaidi ya milioni moja ambao wanahitaji msaada wa dharura wa chakula ambapo bila msaada huo hawawezi kuishi.” Hii ni ongezeko la zaidi ya 1/10 na zaidi limetokana na vikwazo vilivyopelekea Gaza kufungwa na athari za kiuchumi, vita vivyosambaratisha maisha ya watu na miundombinu na mvutano wa ndani unaoendelea katika siasa za Wapalestina tangu mwaka 2007 baada ya Hamas kuingia madarakani “ Amesema Schmale.

Zaidi ya hapo vifo vya wapalestina 195 wakiwemo wanafunzi 14 wa shule za UNRWA ,maandamano yaliyodumu kwa mwaka mzima , pamoja na athari za kiuchumi, kiwmili na kiakili kutokana na majeraha, vimekuja baada ya migogoro mikubwa mitatu Gaza tangu 2009, ambayo ilikatili Maisha ya watu 3790 na kujeruhi wengine Zaidi ya 17,000 kwa pamoja.

Hali halisi

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa mwaka 2017ilitabiri kwamba Gaza kutakuwa hakuishiki ifikapo mwaka 2020. Leo hii kukiwa na asilimia 53 ya wasio na ajira na zaidi ya milioni moja wanaotegemea msaada wa chakula kutoka UNRWA, ni bahati tu ya hatua za UNRWA na mashirika mengine ya misaada ya Umoja wa Mataifa ndio vilivyosaidia kusitoisha zahma kubwa Zaidi ya kibinadamu hadi sasa na kusambaratisha kabisa kwa eneo hilo la Gaza.

Kukiwa na hali iliyotawala ya sintofahamu kuhusu hatma ya mchakato wa amani baina ya Israel na Palestina , UNRWA ndio kiungo pekee kinacholeta ladha ya maisha katika eneo hilo, na likiweza kuendelea kutimiza wajibu na majukumu yake basi inakuwa ndio msaada pekee wa kuwahakikishia uhai mamiliobni ya watu wa Gaza. Na kitu cha haraka Zaidi kwa sasa ni msaada wa chakula ambao unatolewa na shirika hilo ambao sasa uko njiapanmda kutokana na ukata.