Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Hakuna mbadala' wa kazi ya UNRWA kuokoa maisha huko Gaza - Sigrid Kaag

 Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza akitoa maelezo kwa wanahabari kufuatia mashauriano na Baraza la Usalama.
UN Photo/Manuel Elías
Sigrid Kaag, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza akitoa maelezo kwa wanahabari kufuatia mashauriano na Baraza la Usalama.

'Hakuna mbadala' wa kazi ya UNRWA kuokoa maisha huko Gaza - Sigrid Kaag

Masuala ya UM

Hakuna shirika linaloweza kuchukua nafasi ya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita, Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza Sigrid Kaag amewaeleza waandishi wa habari leo Januari 30 nje ya Baraza la Usalama katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.  

Mbali na uamuzi wa kisiasa, ambao ungepaswa kufanywa na Baraza Kuu, "hakuna jinsi shirika lolote linaweza kuchukua nafasi ya uwezo mkubwa na muundo wa UNRWA na uwezo wake na ujuzi." Bi.Kaag amesema.

Pia amebainisha jukumu muhimu ambalo shirika hilo limefanya kwa miongo kadhaa, kabla ya mzozo wa sasa, katika elimu, huduma za afya na huduma zingine. UNRWA ilianzishwa na Baraza Kuu mnamo Desemba 1949.

Operesheni za UNRWA ziko hatarini baada ya nchi kadhaa wafadhili, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ujerumani na Japan, kusimamisha ufadhili kutokana na madai makubwa kwamba wafanyakazi wake kadhaa walihusika katika mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 nchini Israel.

Shirika limeanzisha uchunguzi, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika atawajibishwa, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa mashitaka ya jinai.

Amezungumza kwa mara ya kwanza

Mazungumzo ya Bi. Kaag kwa waandishi wa habari yamekuja baada ya mkutano wake wa kwanza wa faragha kwa Baraza la Usalama tangu kuchukua jukumu lake kuu la uratibu kwa mujibu wa azimio la Baraza 2720 (2023).

Jukumu lake ni kuwezesha, kuratibu, kufuatilia na kuthibitisha shehena za misaada ya kibinadamu kwa Gaza na pia kuanzisha utaratibu wa Umoja wa Mataifa wa kuharakisha usafirishaji wa misaada ya kibinadamu hadi kwenye eneo hilo kupitia Mataifa ambayo sio sehemu ya mzozo.

Bi. Kaag amesisitiza kwamba mafanikio ya mamlaka yake "ni kuhusu uwezo wa kufikia na kukidhi mahitaji" ya raia huko Gaza.

Sifa za Sigrid Kaag

Bi Kaag, raia wa Uholanzi ameshikilia nyadhifa mbalimbali za juu katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. Aliteuliwa na Katibu Mkuu tarehe 26 Desemba 2023 na kuanza kazi yake tarehe 8 Januari.

Alikuwa Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon kutoka 2015 hadi 2017 na kutoka 2013 hadi 2015 alikuwa mkuu wa Shirika la Pamoja la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Misheni ya Silaha za Kemikali nchini Syria.

Pia aliwahi kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP (2010-13) na alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini (2007-10).

Pia kabla ya hapo, Bi Kaag alishikilia nyadhifa kadhaa za juu katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) na UNRWA.

Anazungumza Kiarabu fasaha na lugha nyingine tano.

Pia alishikilia majukumu mengi ya juu katika Serikali ya Uholanzi, ikiwa ni pamoja na kama Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje.