Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa wanawake katika ushirikiano wa kimataifa watambuliwa

Wanawake viongozi wa nchi na serikali wakiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya kushirilki mkutano wa viongozi wanawake chini ya UNGA77
Steven Viju Philip
Wanawake viongozi wa nchi na serikali wakiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya kushirilki mkutano wa viongozi wanawake chini ya UNGA77

Mchango wa wanawake katika ushirikiano wa kimataifa watambuliwa

Wanawake

Ikiwa leo ni ni siku ya kimataifa ya wanawake katika ushirikiano wa kimataifa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la  Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi ya Utamaduni, UNESCO Audrey  Azoulay amesema kujenga usawa kupitia ushirikiano wa kimataifa kunamaanisha, kutambua nafasi ya wanawake wanaojihusisha na ushirikiano wa kimataifa,na kuwafanya wao chanzo cha hamasa kwa wale wote wanaotaka kushiriki katika mabadiliko hayo.

Bi. Azoulay amesema hayo kupitia wavuti wa UNESCO ambayo ndiyo inasimamia siku hii iliyoanzishwa na Mkutano wake Mkuu tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2021 kupitia azimio namba 41 C/57.

Nafasi ya wanawake katika kuchagiza amani na maendeleo endelevu

Azimio hilo lilitangaza tarehe 25 mwezi Januari kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya wanawake katika ushirikiano wa kimataifa ikiwa na lengo la kutambua mchango muhimu wa wanawake katika kusongesha haki za binadamu, amani na maendeleo endelevu ndani ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNESCO anasema tayari wanawake walio katika nafasi zinazowawezesha kushiriki katika ushirikiano wa kimataifa wamekuwa chanzo cha hamasa kwa wengine wanaotaka mabadiliko.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Usawa wa kijinsia katika kutatua dharura ya mabadiliko ya tabianchi.” 

Lengo la UNESCO ni kutambua wanawake viongozi katika mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ili kuchagiza mazungumzo kuhusu majawabu ya kimataifa dhidi ya ubaguzi wa kijinsia ambao unakwamisha hatua dhidi ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi.

Halikadhalika kuchagiza ongezeko la uwakilishi wa wanawake kwenye nafasi za msingi za kupitisha maamuzi ambayo yanaumba na kutekeleza ajenda za ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha ushirikiano huo unafanya kazi kwa ajili ya wanawake na wasichana kupitia hatua za kuleta mabadilko chanya ya kijinsia na mikataba.

Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa OCHA akiwa kwenye moja ya vikao kuhusu mabadiliko ya tabianchi wakati wa mkutano wa COP28 huko Dubai, Falme za kiarabu
COP28/Mahmoud Khaled
Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa OCHA akiwa kwenye moja ya vikao kuhusu mabadiliko ya tabianchi wakati wa mkutano wa COP28 huko Dubai, Falme za kiarabu

Bi. Msuya wa OCHA ajivunia kuwa mwanasayansi na sehemu ya ushirikiano wa kimataifa

Miongoni mwa wanawake viongozi katika nyanja ya ushirikiano wa kimataifa ni Joyce Msuya ambaye kwa sasa ni Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya uratibu wa misaada ya dharura.

Kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, Bi. Msuya amesema “kama mwanasayansi ninayejivunia, mwanamke na mwana ushirikiano wa kimataifa nataka kusaidia wanawake wengi zaidi waingie katika tasnia hii.”

Bi. Msuya ambaye ni Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA ameongeza kuwa “kunahitajika wanawake wengi zaidi katika meza ya kupitisha maamuzi, hasa pindi linapokuja suala la mabadiliko ya tabianchi. Heko siku ya wanawake katika ushrikiano wa kimatafai.”

Siku ya leo imeadhimishwa kwa kufanyika mkutaon wa viongozi wanawake kwenye mfumo wa ushirikiano wa kimataifa ukimulika majawabu ya kimataifa katika ubaguzi wa kijinsia unaokwamisha hatua dhidi ya dharura za tabianchi.

Mapendekezo ya mkutano huu yatawasilishwa kwenye mikutano ikiwemo ule wa Umoja wa Mataifa kuhusu Muongo wa Bahari utakaofanyika Barcelona, Hispania mwezi Aprili mwaka huu, siku ya uhuru wa vyombo vya habari Mei 2024, Jukwaa la Sayansi duniani, Novemba 2024 na Mkutano wa dunia kuhusu bahari mwezi Juni mwaka 2025.