Ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani unaenda mrama:Guterres 

24 Aprili 2022

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba lengo la siku hii limeanza kwenda mrama. 

Katika ujumbe wake maalum kwa ajili ya siku hii inayoadhimishwa kila mwaka Aprili 24 Antonio Guterres amesema  nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kwa kuridhia au kukubali mkataba wa Umoja wa Mataifa, zimejitolea wenyewe kwa maadili ya kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani. 

“Lakini tunapoadhimisha siku ya kimataifa ya mwaka huu ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani, ahadi hii inavunjwa. Kanuni za msingi za ushirikiano wa kimataifa ziko katika shinikizo kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.” 

Ameongeza kuwa kuanzia mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi hadi kuongezeka kwa vita ikiwa ni pamoja na vita vinavyoendelea nchini Ukraine utawala wa silaha za maangamizi makubwa, dharura za kiafya na mfumo wa kimataifa wa ulinzi wa wakimbizi na thamani ya diplomasia viko katika tishio kubwa kutoka kila pembe. 

Kwa mantiki hiyo amesema “Tunahitaji kubadilisha wakati huu wa shida kuwa wakati wa mshikamano wa kimataifa. Mapendekezo katika ripoti yangu kuhusu ajenda yetu ya pamoja yanalenga kulinda na kuimarisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa na kuunda mtandao, na mshikamano wa kimataifa ambao unafaa kwa siku zijazo.” 

Hivyo amesisitiza kwamba “Katika Siku ya Kimataifa ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani, natoa wito kwa serikali na viongozi wote kurejesha dhamira yao ya mazungumzo na suluhu za kimataifa ambazo ndiyo njia pekee endelevu ya amani.” 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter