Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji ushirikiano wa kimataifa sasa kuliko wakati mwingine wowote:Guterres

Jengo la sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York, Marekani ambako masuala ya ushirikiano wa kimataifa hupatiwa kipaumbele
UN /Rick Bajornas
Jengo la sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York, Marekani ambako masuala ya ushirikiano wa kimataifa hupatiwa kipaumbele

Tunahitaji ushirikiano wa kimataifa sasa kuliko wakati mwingine wowote:Guterres

Masuala ya UM

Ushirikiano wa kimataifa unahitajika duniani kuliko wakati mwingine wowote ili kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikibali dunia hivi sasa kwa pamoja.

 

Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipozungumza kwenye mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuhusu “kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na jukumu la Umoja wa Mataifa “.

Guterres amekumbusha kwamba mjadala huu unafanyika siku chache kabla ya kuadhimisha miaka 100 ya kumalizika kwa vita vikuu vya kwanza ya dunia vilivyokuwa vibaya na vyenye athari kubwa lakini zaidi ya yote vikikumbusha kwamba kutokuwepo kwa  mkakati wa ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kutatua matatizo ya kimataifa , ndio ilikuwa chachu ya kuzuka kwa vita hivyo na athari zake kudumu kwa miongo.

Zahma ya vita vikuu vya pili vya dunia ndio ikawa kengele ya kuiamsha jumuiya ya kimataifa kuwa na ushirika uliopo sasa ambao umethibitisha kuokoa maisha, kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuepuka kutumbukia katika vita ya tatu ya dunia na mafanikio mengine. Na kuongeza

"Miaka ya karibuni imeshuhudia mafanikio katika diplomasia ya kimataifa, zaidi ya yote ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi. Pia operesheni za amani zilizoidhinishwa na Baraza hili ni kielelezo muhimu cha hatua za ushirikiano wa kimataifa, ulinzi wa amani umesaidia nchi nyingi kujikwamua baada ya vita.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuhusu “kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na jukumu la Umoja wa Mataifa". “.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuhusu “kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na jukumu la Umoja wa Mataifa". “.

 

Lakini kwa upande mwingine amesema juhudi hizo za ushirikiano wa kimataifa zipo katika shinikizo kubwa “Huu ni wakati ulioghubikwa na migogoro mingi, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la mivutano ya kibiashara. Ni wakati ambao watu wanakimbia kuvuka mipaka kusaka usalama na fursa, bado tunakabiliwa na hatari ya uzalishaji wa silaha za maangamizi na ndio tunaanza kutambua uwezekano wa hatari ya teknolojia mpya, imani za watu zinazidi kupotea, matumaini kukandamizwa na inaonekana kila tishio la kimataifa linapoongezeka basi ushirikiano ndio unavyozidi kuwa mdogo, na kuongeza kuwa,

“Hii ni hatari sana katika changamoto zilizopo sasa ambazo kuzikabili mitazamo ya kimataifa ni muhimu. Katika mtazamo huu mgumu tunahitaji kuhamasisha kurejea katika ushirikiano wa kimataifa . Tunahitaji mfumo wenye mabadiliko, ulioboreshwa na wnye ushirikiano imara wa kimataifa.”

Ameongeza kuwa tunahitaji ahadi za sheria ambazo zinafuata misingi ya Umoja wa Mataifa na kuwa na taasisi mbalimbali na miakata ambayo itaifanya katiba ya Umoja wa Mataifa kuwa hai.

Katika mukhtadha huo amezichagiza nchi wanachama zote kuwekeza kujenga mfumo sawia wa utandawazi na unaofanya kazi kwa ajili ya wote ukienda sanjari na ajenda ya 2030.

Kama sehemu ya ulinzi wa raia walinda amani kutoka Ethiopia walioko UNMISS wanao utaratibu wa kuwasindikiza  wanawake wapokwenda kutafuta kuni porini ili kuhakikisha wapo salama wakati wanafanya shughuli za kuhudumia familia zao.
picha ya UNMISS
Kama sehemu ya ulinzi wa raia walinda amani kutoka Ethiopia walioko UNMISS wanao utaratibu wa kuwasindikiza wanawake wapokwenda kutafuta kuni porini ili kuhakikisha wapo salama wakati wanafanya shughuli za kuhudumia familia zao.

 

Kuhusu mabadiliko kwenye Umoja wa Mataifa amesema yana mchango muhimu na ataendelea kushinikiza mabadiliko hayo katika mihimili mikuu ya Umoja wa Mataifa na zaidi ya yote kukumbusha kwamba dira ya yote hayo ni katiba ya Umoja wa Mataifa ambayo inasisitiza maadili ya kimataifa, Amani, maendeleo, haki za binadamu na utawala wa sheria mambo yanayochagiza dunia kuishi kama kitu kimoja kwa Amani. Na amesisitiza kuwa ahadi hizo ndizo zinazohitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote duniani.