Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN tuko tayari kuisaidia athari za mafuriko Tanzania: Zlatan Milisic

Zlatan_Milišić, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania wakati wa mahojiano na Stella Vuzo wa UNIC Dar es salaam. (Maktaba)
UN Tanzania/Ahimidiwe Olotu
Zlatan_Milišić, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania wakati wa mahojiano na Stella Vuzo wa UNIC Dar es salaam. (Maktaba)

UN tuko tayari kuisaidia athari za mafuriko Tanzania: Zlatan Milisic

Msaada wa Kibinadamu

Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ikiongozwa na mratibu mkazi Zlatan Milisic leo imesema iko tayari kwa ombi la serikali kuisaidia Tanzania kupitia kundi la uratibu wa dharura kutoa msaada zaidi kukabiliana na athari za mafuriko makubwa ya hivi karibuni nchini humo.

Timu hiyo inayojumuisha mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na washirika wake  kwa mwezi mzima uliopita imekuwa ikitoa msaada kwa maeneo yaliyoathirika vibaya na mafuriko hayo ya Hanang jimboni Manyara Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

Takriban watu 140 wamejeruhiwa , zaidi ya 9000 wameathirika na 760 kutawanywa na mafuriko hayo.

Msaada kwa waathirika wa mafuriko

Kwa mujibu wa timu hiyo ya Umoja wa Mataifa “Msaada muhimu unawafikia takriban watu 9,000, na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetoa mgawo wa chakula wa miezi mitatu. Pia, Shirika la Afya Duniani WHO linaangazia kuzuia magonjwa, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF likitoa huduma za maji na usafi wa mazingira, kusambaza vifaa vya usafi, matangi ya maji na mengine mengi.”

Kwa upande wake, Shirika la Umoja la Idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA limesambaza vifaa 1,200 vya hedhi kwa wanawake na wasichana, wakati Shirika la Umoja wa Mataifa Mataifa la Uhamiaji IOM, lilijiunga na tathmini ya timu ya Umoja wa Mataifa kusaidia zaidi mahitaji ya wakimbizi wa ndani.