Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa dola milioni 13 kwa waathirika wa Kenneth Msumbiji, watu 38 wapoteza maisha

28 Aprili 2019. katika eneo la Mahate Pemba -maporomoko ya udongo ymeathiri eneo hilo baada ya kimbunga Kenneth kuikumba Msumbiji. Watu wengi bado wako katika eneo hilo na baadhi ya nyumba zinaonekana ziko karibu sana na bonde lililosababishwa na maporomo
OCHA/Saviano Abreu
28 Aprili 2019. katika eneo la Mahate Pemba -maporomoko ya udongo ymeathiri eneo hilo baada ya kimbunga Kenneth kuikumba Msumbiji. Watu wengi bado wako katika eneo hilo na baadhi ya nyumba zinaonekana ziko karibu sana na bonde lililosababishwa na maporomo

UN yatoa dola milioni 13 kwa waathirika wa Kenneth Msumbiji, watu 38 wapoteza maisha

Msaada wa Kibinadamu

Fedha za msaada zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zitasaidia kuhakikisha chakula , malazi, huduma za afya na maji safi vinapatikana kwa waathirika wa kimbunga Kenneth nchini Msumbiji. Nchi hiyo ina watu 18,000 waliotawanywa na kimbunga Kenneth ambao hivi sasa wanapata hifadhi kwenye makazi ya muda. Watu38 wamefariki dunia kufuatia kimbunga hicho kufikia sasa.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, dola milioni 13 zimetolewa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kuwasaidia waathirika wa kimbunga Kenneth nchini Comoro na Msumbiji.

Msaada huo umetangazwa na mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcok na ni sehemu ya msaada wa mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF. Lowcok  amesema kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha huduma za msingi kama chakula, malazi, afya na maji vinatolewa kwa waathirika.

Athari za kimbunga

Eneo lililoathirika sana na kimbunga Kenneth ni jimbo la Kaskazini la Cabo delgado nchini Msumbiji ambako hadi sasa watu 38 wamepoteza maisha katika kimbunga hicho kinachoelezwa kuwa moja ya vimbunga vikali kuwahi kuikumba nchi hiyo.

Akizungumza na UN news kutoka Pemba Cabo Delgado gavana wa jimbo hilo Julio Parrugue amesema eneo hilo lililoko pwani linahitaji mikakati madhubuti ya kuhimili majanga ya asili.

Katika picha hii  Antonio Manuel anayeishi katika eneo la Pemba nchini Msumbiji akiwa amesimama nje ya mabaki ya nyumba yake iliyosambaratishwa kabisa na kimbunga Kenneth tarehe 25 Aprili 2019
WFP/Deborah Nguyen
Katika picha hii Antonio Manuel anayeishi katika eneo la Pemba nchini Msumbiji akiwa amesimama nje ya mabaki ya nyumba yake iliyosambaratishwa kabisa na kimbunga Kenneth tarehe 25 Aprili 2019

Mnepo

Ameongeza kuwa “Tunakabiliwa na janga kubwa la asili. Tulitangaziwa na taasisi ya kitaifa ya utabiri wa hali ya hewa na tukafikisha tarifa hizo kwa watu wetu, tulichukua hatua madhubuti za tahadhari. Hata hivyo kutokana na athari kubwa za kimbunga hiki tunahitaji kuwa makini zaidi na kuchukua tahadhari zaidi kwa sababu tutahitaji kujipanga vizuri ili kuwa tayari kukabiliana na athari kama hizo. Na kisha tunahitaji kujiandaa hata zaidi ili tuweze kuwa na mnepo.”

Mvua kubwa inaendelea kunyesha hata baada ya kusambaratisha nyumba 4,000, pia kuharibu shule na vituo vya afya.

Kimbunga Kenneth kimekumba eneo hilo la Kusini mwa Afrika mwisho wa msimu wa mvua wakati ambapo vina vya mito tayari vilikuwa vimejaa maji. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mvua kubwa inatarajiwa katika siku chache zijazo na hivyo kufanya hali kuwa mbaya zaidi. Shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO limeonya kwamba kuna hatari ya mafuriko na maporomoko ya udongo  na kwamba athari za kimbunga Kenneth zinaweza kuwa mara mbili ya zile zilizosababishwa na Idai katika maeneo yaliyoathirika.

Hali halisi ya kimbunga 

Kimbunga Kenneth kinachukuliwa kuwa si chakawaida kwa sababu hakujawahi kutokea kimbunga kama hicho Kaskazini mwa Msumbiji. Suala lingine linalotia hofu ni kwamba kimbunga hicho kimepiga hata katika wilaya ambazo zimeathirika na uasi katika miaka miwili iliyopita. Katika maeneo hayo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limetangaza kwamba linashirikiana kwa karibu na serikali kuwasaidia wakimbizi wa ndani. Kwa pande wa Comoro OCHA inasema kumekuwa na uharibifu wa nyumba 3,500, umeme umekatika baada ya nguzo kuangushwa, barabara hazipitiki n adaraja moja limebomoka. Baadhi ya shule na vituo vya afya pia vimeathirika.

Hatari

Kimbunga Kenneth hadi sasa kimetawanya watu takribani 1,000 kisiwani Comoro na serikali ya nchi hiyo inakadiria kwamba watu 680,000 huenda wakawa hatarini.

Kwa upande wa Tanzania hakukuwa na taarifa zozote za uharibifu wa kimbunga hicho , lakini mvua, mafuriko na maporomoko ya udongo katika mikoa ya Mtwara na Lindi yameiweka nchi hiyo katika tahadhari.