Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yatia saini makubaliano ya kutoa chanjo mpya ya malaria kwa ajili ya ya kunusuru watoto

Mhudumu wa afya akiwa ameshika sindano ya chanjo ya malaria nchini Ghana wakati wa kampeni ya chanjo kwa wingi. (Maktaba)
WHO
Mhudumu wa afya akiwa ameshika sindano ya chanjo ya malaria nchini Ghana wakati wa kampeni ya chanjo kwa wingi. (Maktaba)

UNICEF yatia saini makubaliano ya kutoa chanjo mpya ya malaria kwa ajili ya ya kunusuru watoto

Afya

Shirika la Umoja wa Mqataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limetangaza makubaliano ya kupata chanjo ya pili ya malaria duniani, R21/Matrix-M. 

Mpango huo ni hatua kubwa kuelekea kukidhi mahitaji makubwa ya dozi mpya ya chanjo dhidi ya malaria ugonjwa ambao bado unaua mtoto mmoja wa chini ya umri wa miaka 5 kila dakika.

Kwa mujibu wa UNICEF mkataba huo wa muda mrefu uliotiwa saini na Serum Life Sciences kwa ajili ya kuanzia mwaka 2024 - 2028 ni masharti ya kabla ya kufuzu ya chanjo kutoka kwa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO

"Inasikitisha na haikubaliki kwamba karibu watoto nusu milioni wanakufa kwa malaria kila mwaka. Makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuwalinda watoto zaidi kutokana na ugonjwa huu hatari,” amesema mkurugenzi wa kitengo cha ugavi cha UNICEF Leila Pakkala.

Chini ya makubaliano haya ya miaka minne, UNICEF inatarajia kuanza kutoa chanjo ya R21/Matrix-M katikati ya mwaka 2024, na chanjo zikianza katika kipindi hicho. 

Hii ni nyongeza ya kazi ya UNICEF ya kupanua wigo wa ufikiaji wa chanjo ya malaria, na inakamilisha chanjo ya kwanza ya kihistoria ya RTS,S. 

Uwasilishaji wa RTS,S unatarajiwa kuanza mwishoni mwa 2023.

Matunda ya miaka 35 ya utafiti

Chanjo za malaria za R21/Matrix-M na RTS,S ni matokeo ya miaka 35 ya utafiti na maendeleo limesema shirika la UNICEF.

Ni chanjo za kwanza zinazotengenezwa dhidi ya ugonjwa wa vimelea. Zote mbili zinachukua hatua dhidi ya Plasmodium falciparum, vimelea hatari zaidi vya malaria duniani na vilivyoenea zaidi barani Afrika. 

Chanjo hizo ni nyongeza muhimu kwa kisanduku cha zana za hatua katika mapambano dhidi ya malaria.

UNICEF ndiyo mnunuzi mkubwa zaidi wa chanjo duniani, ikinunua zaidi ya dozi bilioni 2 za chanjo kila mwaka kwa ajili ya chanjo za kawaida za watoto na kukabiliana na milipuko kwa niaba ya karibu nchi 100. 

Ununuzi huu wa chanjo ya malaria ya R21/Matrix-M utasaidia kuongeza usambazaji wa kimataifa na kuharakisha upatikanaji sawa wa chanjo ya malaria kwa watoto na familia.