Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanazaliwa jehanamu Gaza huku kukiwa na uhaba mkubwa wa huduma na misaada: UNICEF

Watoto karika hospitali ya Al-Shifa Kaskazini mwa Gaza (kutoka Maktaba)
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto karika hospitali ya Al-Shifa Kaskazini mwa Gaza (kutoka Maktaba)

Watoto wanazaliwa jehanamu Gaza huku kukiwa na uhaba mkubwa wa huduma na misaada: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limeonya kwamba watoto wanazaliwa katika hali ya jehanamu Gaza huku wengi huenda wakafariki dunia kutokana na vita na hali mbayá ya maisha na huduma Gaza.

Shirika hilo likirejelea wito wa dharura wa kimataifa wa kusitishwa kwa mapigano, limeripoti kuwa karibu watoto 20,000 wamezaliwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel ya kulipiza kisasi mashambulizi ya Hamas yaliyosababisha vifo vya watu 1,200 Israel na takriban 250 kuchukuliwa mateka Oktoba 7 mwaka jana .

Shirika hilo limesema wakati vita hii ikiendelea, ikiwa ni sikua ya 105 leo watoto hao 20,000 wamezaliwa katika hali ya jehanamu na hii ikimaanisha kwamba mtoto 1 amezaliwa kila baada ya dakika 10.

Wito wa kusitisha mapigano mara moja

Shirika la UNICEF likirejelea wito wa dharura wa kimataifa wa kusitishwa kwa mapigano,  limesema matatizo ya muda mrefu ya upatikanaji wa misaada yamemaanisha kuwa upasuaji kwa wagonjwa umefanywa bila ganzi wakati wanawake wengine wameshindwa kujifungua na watoto wao wamekufa kwa sababu wahudumu wa afya wamezidiwa uwezo.

"Akina mama wanakabiliwa na changamoto zisizoelezeka katika kupata huduma ya matibabu ya kutosha, lishe na ulinzi kabla, wakati na baada ya kujifungua," amesema mtaalamu wa mawasiliano wa UNICEF Tess Ingram.

Ameongeza "Kuwa mama kunapaswa kuwa ni wakati wa kusherehekeae lakini huko Gaza, ni ishara ya mtoto mwingine anayezaliwa katika hali ya kuzimu."

Amesisitiza kuwa ni lazima jumuiya ya kimataifa kushinikiza kuendelea kufikishwa kwa misaada muhimu ya kibinadamu Gaza ili kunusuru maisha ya maelfu ya watoto na raia wa eneo hilo linalokaliwa.