Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel inasema inataka kusambaratisha Hamas, lakini mwelekeo wa sasa utasambaratisha Gaza:Hastings

Jengo la makazi ya watu lilivyosambaratsihwa na mashambulizi Gaza
© UNRWA/Mohammed Hinnawi
Jengo la makazi ya watu lilivyosambaratsihwa na mashambulizi Gaza

Israel inasema inataka kusambaratisha Hamas, lakini mwelekeo wa sasa utasambaratisha Gaza:Hastings

Msaada wa Kibinadamu

Ili kukabiliana na janga la kibinadamu linaoongezeka kwa kasi huko Gaza, mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa yanaweka tayari misaada ya kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na chakula na vifaa vya matibabu katika mpaka wa Misri. Kufungua kivuko kutoka upande wa Israeli ni muhimu sana yamesema mashirika hayo leo.

Hata hivyo, mamlaka ya Israel imehusisha msaada wa kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas tangu kundi hilo la wanamgambo lilipoanzisha shambulio baya la Oktoba 7, amesema Lynn Hastings, mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa misaada ya kibinadamu katika eneo linalokaliwa la Palestina.

Katika mahojiano maalum na UN News leo Jumapili Bi. Hastings amesema 

"Wamesema wanataka kuangamiza Hamas, lakini mwelekeo wao wa sasa unaenda kuangamiza Gaza," 

Akitoa wito wa kuachiliwa huru bila masharti na mara moja kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas, pia Bi. Hastings amehimiza "kuingia mara moja bila masharti Gaza kwa ajili ya utoaji wa misaada ya kuokoa maisha.” 

Ameonya "Tunatarajia kwamba hivi punde hakutakuwa na maji zaidi yatakayosalia, ikiwa sio kesho, basi kufikia Jumanne."

Lynn Hastings Mratibu mkazi na mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo linalokaliwa la Palestina
UN OCHA OPT
Lynn Hastings Mratibu mkazi na mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo linalokaliwa la Palestina

Ni kuhusu kupoteza ubinadamu wetu

Akizungumza na Reem Abaza wa Idhaa ya Kiarabu ya UN News amesema, " Kwa hakika ni kuhusu kupoteza ubinadamu wetu ikiwa jumuiya ya kimataifa itaruhusu hili kuendelea. Tunachokiona sasa ni vitendo vya kinyama, ulimwengu unahitaji kudai kwamba tuweze kutoa msaada ambao uko mlangoni mwa Gaza."

Ombi hilo la Mratibu Mkazi linakuja wakati mzozo huu wa hivi punde kati ya Israel na Hamas ukiingia siku yake ya 10 na muda uliowekwa na Israel kwa raia wapatao milioni 1.1 kuondoka eneo la kaskazini mwa Gaza, kabla ya kile kinachotarajiwa kuwa hatua kubwa ya vikosi vya ardhini vya Israel kuingia Gaza, umekwisha jana.