Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasaidizi wa kibinadamu wa UN Gaza wanahaha, jamii ikikaribia kusambaratika kabisa

Familia zinaendelea kupata hifadhi katika makazi ya UNRWA Khan Younis Kusini mwa Gaza
© UNICEF/Abed Zaqout
Familia zinaendelea kupata hifadhi katika makazi ya UNRWA Khan Younis Kusini mwa Gaza

Wasaidizi wa kibinadamu wa UN Gaza wanahaha, jamii ikikaribia kusambaratika kabisa

Amani na Usalama

Wanawake na watoto wanabeba mzigo mkubwa wa vifo na majeruhi wakati wanajeshi wa Israeli wakipambana na wanamgambo wa Kipalestina katika eneo lote linalokaliwa la Gaza, bila mahali pa usalama pa kwenda, na usambazaji wa misaada ukitatizwa na vita, ukosefu wa kuwafikia wenye uhitaji na uhaba wa vifaa vinavyovuka kuingia katika Ukanda huo yameonya leo mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Adele Khodr, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, leo amesema katika taarifa yake kwamba Gaza ni "mahali hatari zaidi duniani kuwa mtoto . Umegeuka kuwa rundo la vifusi, bila uhai ndani yake.”

Wafanyikazi huyo wa UNICEF amesema kuwa karibu watoto milioni moja sasa wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mzunguko wa ghasia uanze tarehe 7 Oktoba.

Makambi yamejaa pomoni

Bi. Bi Khodr ameonya kwamba "Sasa wanasukumwa zaidi na zaidi kwenda kusini katika maeneo madogo, yaliyojaa watu pomoni bila maji, chakula, au ulinzi, na kuwaweka katika hatari kubwa ya magonjwa ya kuambukiza ya kupumua na magonjwa yatokanayo na maji".

Ameongeza kuwa "Vizuizi na changamoto zinazowekwa kwenye utoaji wa misaada ya kuokoa maisha kwenda na kuvuka Ukanda wa Gaza ni hukumu nyingine ya kifo kwa watoto".

Amesisitiza kwamba mfumo mzima wa kibinadamu unasuasua, haswa chini ya dhiki kubwa inayosababishwa na hatua zilizowekwa na Israeli wakati mashambulizi yanaendelea.

"Usitishaji mapigano mara moja na wa muda mrefu wa kibinadamu ndio njia pekee ya kukomesha mauaji na kujeruhi watoto", amesema.

Jana Ijumaa, Marekani ilipinga azimio la Baraza la Usalama la kutaka kusitishwa kwa mapigano, ikisema kwamba kukomesha mapigano sasa kutawaacha Hamas kuendelea Gaza ambao ni kichocheo cha maafa, kulingana na Balozi wa Marekani Robert Wood.