Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yatoa dola milioni 10 kusaidia waliokimbia Sudan na kuingia Sudan Kusini

Raia wa Sudan Kusini waliorejea nchini kutoka Sudan wakiwasili katika mpaka wa Joda katika Jimbo la Upper Nile.
© WFP/Eulalia Berlanga
Raia wa Sudan Kusini waliorejea nchini kutoka Sudan wakiwasili katika mpaka wa Joda katika Jimbo la Upper Nile.

CERF yatoa dola milioni 10 kusaidia waliokimbia Sudan na kuingia Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF bwana Martin Griffiths, leo ametangaza kutenga dola milioni 10 kutoka kwenye mfuko huo kwa ajili ya kuwasaidia wanaume, wanawake na watoto wanaokimbia Sudan na kuingia katika nchi jirani ya Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa Griffiths pesa hizo zitatumika kujenga makazi, kutoa usaidizi wa pesa taslimu, kujenga mitambo ya maji, vyoo na vifaa vya usafi, na kusaidia usafiri wa watu wapya ambao kwa sasa wanakaa kwenye vituo vya mpito viliyofurika watu kupindukia.
 

Ameongeza kuwa “Tunatazamia kwamba maelfu ya watu wa ziada wanaweza kuvuka mipaka na kuingia Sudan Kusini kutoka Sudan katika kipindi cha miezi sita ijayo, tna hivyo kuongeza shinikizo katika mfumo ambao tayari una changamoto kubwa.”
 

Watu 60,000 wameingia Sudan Kusini katika mwezi mmoja

Mratibu huyo amesema katika mwezi mmoja tu uliopita, zaidi ya watu 60,000 wamewasili Sudan Kusini, kufuatia kuzuka kwa mapigano ndani na karibu na Wad Medani, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan.
Na hadi kufikia leo, takriban watu nusu milioni wamevuka mpaka kutoka Sudan hadi Sudan Kusini tangu katikati ya mwezi Aprili.