Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICJ: Mahakama kuu ya UN ya haki, chanzo cha ushauri wa mamlaka

Bendera ya Umoja wa Mataifa ikipepea mbele ya kasri la amani , maskani ya mahakama ya kimataifa yaHaki The Hague Uholanzi
UN Photo
Bendera ya Umoja wa Mataifa ikipepea mbele ya kasri la amani , maskani ya mahakama ya kimataifa yaHaki The Hague Uholanzi

ICJ: Mahakama kuu ya UN ya haki, chanzo cha ushauri wa mamlaka

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya kimataifa ya haki ICJ ni moja ya vyombo vikuu sita vya Umoja wa Mataifa na hapa tunakutanabaisha inafanyaje kazi, nani anawasilisha kesi ICJ na je maamuzi yake yana mashiko gani?.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ni nini na kwa nini ni muhimu?

Wasifu wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ulipata hadhi ya juu mwezi Januari, kufuatia uamuzi wa Afrika Kusini wa kupeleka kesi dhidi ya Israel katika mahakama hiyo kwa kukiuka majukumu yake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari. Huu ni ufafanuzi utangulizi kuhusu ICJ, na inafanya nini.

ICJ ni ya nini, na inafanya kazi vipi?

Tweet URL

ICJ, ambayo iko katika kasri la amani huko The Hague, jiji la Uholanzi, ilianzishwa mwaka 1945 kama njia ya kusuluhisha mizozo kati ya nchi. 

Mahakama hiyo pia hutoa maoni ya ushauri kuhusu masuala ya kisheria ambayo yamewasilishwa kwake na vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa vilivyoidhinishwa.

Ikijulikana sana kama 'Mahakama ya Dunia', ICJ ni mojawapo ya vyombo vikuu sita vya Umoja wa Mataifa, kwa msingi sawa na Baraza Kuu, Baraza la Usalama, Baraza la Kiuchumi na Kijamii ECOSOC, Baraza la Udhamini na Sekretarieti, na ICJ ni moja vyombo hivyo pekee ambayo haipo New York.

Tofauti na Mahakama ya Haki ya Muungano wa Ulaya, ICJ si mahakama kuu ambayo mahakama za kitaifa zinaweza kugeukia, inaweza tu kusikiliza mzozo inapoombwa kufanya hivyo na nchi moja au zaidi.

Mahakama hiyo inaundwa na majaji 15, ambao wote wamechaguliwa kuhudumu kwa miaka tisa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama. Uchaguzi hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa theluthi moja ya viti, na majaji wanaostaafu wanaweza kuchaguliwa tena. 

Wanachama wa Mahakama hawawakilishi serikali zao bali ni mahakimu huru, na kunakuwa na hakimu mmoja tu wa taifa lolote kwenye Mahakama.

Kesi zinafunguliwa kwa wahusika kuwasilisha na kubadilishana mashauri yenye maelezo ya kina ya mambo ya hakika na ya sheria ambayo kila upande unategemea, na awamu ya maelezo ya mdomo inayojumuisha vikao vya hadhara ambapo mawakala na mawakili huhutubia Mahakama. 

Nchi zinazohusika huteua wakala wa kutetea kesi yao, mtu ambaye ana haki na wajibu sawa na wakili katika mahakama ya kitaifa. 

Wakati mwingine, mwanasiasa mkuu anaweza kutetea nchi yake, kama ilivyokuwa katika kesi ya mwaka 2020 ya Gambia dhidi ya Myanmar.

Baada ya hatua hii, majaji wanajadiliana kwa kutumia kamera kwa faragha, nyuma ya milango iliyofungwa, na kisha Mahakama kutoa uamuzi wake.

Urefu wa muda huu unaweza kuwa kuanzia wiki chache hadi miaka kadhaa.

Kwa nini ICJ ni muhimu?

ICJ ndiyo mahakama pekee ya kimataifa inayosuluhisha mizozo kati ya nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. 

Hii ina maana kwamba inatoa mchango muhimu kwa amani na usalama duniani, na kutoa njia kwa nchi kutatua masuala bila kutumia migogoro.

Mahakama ya kimataifa ya Haki ICJ ikitoa maamuzi dhidi ya pingamizi lililowasilishwa na Marekani dhidi ya thamani za Iran kwenye kasri la amani (Kutoka Maktaba)
UN Photo/ICJ-CIJ/Frank van Beek
Mahakama ya kimataifa ya Haki ICJ ikitoa maamuzi dhidi ya pingamizi lililowasilishwa na Marekani dhidi ya thamani za Iran kwenye kasri la amani (Kutoka Maktaba)

Ni kesi za aina gani zinazopelekwa ICJ?

Mahakama inaweza kutoa uamuzi juu ya aina mbili za kesi: "kesi zenye utata" ambazo ni mabishano ya kisheria kati ya nchi na “Ushauri wa mashauri” ambao ni maombi ya maoni ya ushauri kuhusu masuala ya kisheria yanayowasilishwa  kwake na vyombo vya Umoja wa Mataifa na mashirika fulani maalumu.

Kesi iliyoletwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel tarehe 29 Desemba 2023 ni mara ya kwanza kwa kesi yenye utata kuwasilishwa dhidi ya Israel katika mahakama ya ICJ. Maoni ya ushauri ya mwaka 2004 yaligundua kuwa ujenzi wa ukuta uliojengwa na Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na kuzunguka Jerusalem Mashariki, na utawala unaohusishwa nayo, ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Afrika Kusini inadai kwamba “matendo na kutotenda kwa Israeli kuna tabia ya mauaji ya kimbari, kwani wamejitolea kwa lengo mahususi . . kuwaangamiza Wapalestina huko Gaza kama sehemu ya kundi kubwa la taifa, rangi na kabila la Palestina”.

Afrika Kusini inataka kufahamu mamlaka ya Mahakama hiyo kuhusu Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa Umoja wa Mataifa wa 1948, ambapo nchi zote mbili zimetia saini , lakini Israel inakana madai hayo.

Kesi nyingine ya hivi majuzi ambayo ilipata umakini wa kimataifa ilihusu uamuzi dhidi ya Myanmar mwezi Januari 2020, kuamuru nchi hiyo kuwalinda watu wake walio wachache wa kabila la Rohingya na uharibifu wa ushahidi unaohusiana na tuhuma za mauaji yakimbari. 

Kesi hiyo, iliyowasilishwa na Gambia, ilipata umaarufu sana kwa kuonekana kwa Aung San Suu Kyi, kiongozi wa wakati huo wa Myanmar, akiwa The Hague kutetea nchi yake.

Aung San Suu Kyi mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ
ICJ/Frank van Beek
Aung San Suu Kyi mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ

Kuhusu "mashauri ya ushauri", tarehe 20 Januari 2023, Baraza Kuu liliomba maoni ya ushauri kutoka kwa Mahakama hiyo juu ya "matendo ya Israeli yanayoathiri haki za binadamu za watu wa Palestina katika eneo linalokaliwa la Palestina, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki" na, Machi 2023, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha, azimio la kuitaka mahakama kutoa maoni ya ushauri kuhusu wajibu wa mataifa kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, huku wazungumzaji wengi katika mjadala huo wakipongeza hatua hiyo kama hatua muhimu katika miongo mingi ya mapambano ya haki ya mabadiliko ya tabianchi. Taratibu zote mbili za ushauri zinaendelea.

Nani anaweza kuleta kesi Mahakamani ICJ?

Nchi yoyote mwanachama inaweza kuleta kesi dhidi ya nchi nyingine yoyote mwanachama, iwe iko kwenye mzozo au la, wakati maslahi ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa yamo hatarini. 

Katika kesi ya Gambia dhidi ya Myanmar kwa mfano, Gambia haikuhusika moja kwa moja na tuhuma za mauaji ya kimbari dhidi ya Myanmar, lakini hilo halikuizuia nchi hiyo kuchukua hatua hiyo, kwa niaba ya Jumuiya ya Ushirikiano wa nchi za Kiislamu OIC.

Raia walipoteza maisha katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine kufuatia shambulio
© UNOCHA/Saviano Abreu
Raia walipoteza maisha katika kijiji kidogo cha Hroza Mashariki mwa Ukraine kufuatia shambulio

Ni nini athari za uamuzi wa Mahakama ya ICJ?

Maamuzi ya ICJ ni ya mwisho na hakuna uwezekano wa kukata rufaa.

Ni juu ya mataifa yanayohusika kutumia maamuzi ya Mahakama katika mamlaka yao ya kitaifa na mara nyingi wanaheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kuzingatia.

Iwapo nchi itashindwa kutekeleza majukumu iliyo nayo chini ya hukumu, njia pekee iliyobaki ni kugeukia Baraza la Usalama ambalo linaweza kupigia kura azimio, kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa. 

Hii ilitokea katika kesi iliyowasilishwa na Nicaragua dhidi ya Marekani mwaka 1984, ikitaka kulipwa fidia kwa msaada wa Marekani kwa waasi wa Contra. 

ICJ iliamua kuunga mkono Nicaragua, lakini Marekani ilikataa kukubali matokeo hayo. Kisha Nicaragua ilipeleka suala hilo kwa Baraza la Usalama, ambapo azimio husika lilipigiwa kura ya turufu na Marekani.

Je, ICJ ina tofauti gani na ICC?

Kuna mkanganyiko wa mara kwa mara kati ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Njia rahisi zaidi ya kuelezea tofauti ni kwamba kesi za ICJ zinahusisha nchi, na ICC ni mahakama ya jinai, ambayo huleta kesi dhidi ya watu binafsi kwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Pia, wakati ICJ ni chombo cha Umoja wa Mataifa, ICC iko huru kisheria na Umoja wa Mataifa ingawa imeidhinishwa na Baraza Kuu. 

Ingawa si nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo ni washirika wa ICC, inaweza kuanzisha uchunguzi na kufungua kesi zinazohusiana na madai ya uhalifu uliofanywa katika eneo hilo au na raia wa nchi mwanachama wa ICC au wa nchi ambayo imekubali mamlaka yake. 

ICC kesi mbalimbali zimesikilizwa na maamuzi yametolewa kuhusu ukiukaji mbalimbali, kuanzia kwa kutumia ubakaji kama silaha ya vita hadi kuwaandikisha watoto kuwa wapiganaji.