Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICJ yaitaka Myanmar iwalinde warohingya, Guterres aunga mkono

Majaji wa ICC mjini The Hegue Uholanzi wakifanya maamuzi dhidi ya kesi ya Myanmar
ICJ-CIJ/Wendy van Bree
Majaji wa ICC mjini The Hegue Uholanzi wakifanya maamuzi dhidi ya kesi ya Myanmar

ICJ yaitaka Myanmar iwalinde warohingya, Guterres aunga mkono

Haki za binadamu

Serikali ya Myanmar leo imeamriwa na mahakama ya haki ya Umoja wa Mataifa ICJ, kuzuia machafuko yanayoweza kusababisha mauaji ya kimbari kwa watu wa kabila la Rohingya ambao ni Waislam wachache na kulinda ushahidi wowote wa uhalifu wa siku za nyuma dhidi ya watu hao.

Katika uamuzi wa leo wa bila kupingwa, mahakama ya kimataifa ya ICJ huko  mjini The Hague Uholanzi imeweka "hatua za dharura" kwa nchi ya Myanmar kwa  kuiamuru serikali ya Aung San Suu Kyi kuheshimu matakwa ya mkataba wa 1948 mauaji ya kimbari .

Mahakama ya ICJ imeweka bayana kwamba kuna ushahidi wa ukiukwaji wa mkataba huo na kuonya kwamba takribani Warohingya 600,000 waliosalia nchini Myanmar wako katika hatari kubwa ya mashambulizi kutoka kwa jeshi.

Uamuzi huo ni wa kupingana na utetezi wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi aliyetetea nchi yake dhidi ya tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita wakati wa siku tatu za kusikilizwa kwa kesi ililowasilishwa na Gambia huko ICJ mwezi uliopita.

Guterres aunga mkono uamuzi wa ICJ

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha amri ya Mahakama ya kimataifa ya haki ya Umoja wa Mataifa, ICJ kuhusu Myanmar inayotaja hatua za muda kwenye kesi ya Gambia dhidi ya taifa hilo la barani Asia linalodaiwa kukiuka mkataba wa kimataifa wa kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo jijini New York, Marekani, Bwana Guterres ametambua uamuzi wa kauli moja wa mahakama hiyo ya kuagiza Myanmar kwa mujibu wa wajibu wake wa mkataba huo, “ichukue hatua zote ndani ya mamlaka yake kuhusiana na watu wa kabila la Rohingya waliopo nchini humo na izuie utekelezaji wa vitendo kwa mujibu wa ibara ya II ya mkataba huo ikiwemo mauaji, kusababisha maumivu ya mwili au kiakili pamoja na kuchukua hatua za kudhibiti uzao wao.”

Katibu Mkuu anaunga kwa dhati mbinu za aman iza kusaka suluhu katika mizozo ya kimataifa akitoa wito kwa mujibu wa chata ya ICJ kuwa uamuzi wa mahakama hiyo unatambulika kisheria na kwamba Myanmar inapaswa kuzingatia amri ya mahakama hiyo.

Kwa mujubu wa mkataba wa ICJ ambayo ni moja ya vyombo vya msingi vya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu atawasilisha notisi ya hatua hizo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Je ni hatua zipi zilizowekwa?

Amri za ICJ zinaifunga Myanmar na zinaunda majukumu ya kisheria ambayo lazima yatekelezwe. Hatua za muda zilizowekwa na mahakama zinahitaji serikali kuzuia vitendo vya mauaji, kuhakikisha jeshi la polisi na polisi hawatendi mauaji ya kimbari, kuhifadhi ushahidi wa vitendo vya mauaji na kuripoti utekelezaji wa amri hizo ndani ya miezi nne.

Amri hizo zimetumwa moja kwa mojakwenye  baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa , ambako majibu ya Myanmar yatapimwa. Nchi hiyo inapokea msaada wa kidiplomasia kutoka China, ambayo ni mmoja wa washiriki watano wa kudumu wa baraza hilo.

Kesi hiyo ilifikishwa kwenye mahakama ya ICJ na Gambia, nchi yenye idadi kubwa ya waislamu miongoni mwa nchi za Afrika Magharibi ambayo inadai kwamba Myanmar imevunja mkataba wa wa mauaji ya kimbari, ambao ulipitishwa baada ya mauaji ya maangamizi makuu au Holocaust.