Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya Houthi katika Bahari ya Shamu, Baraza la Usalama lalaani vikali

Baraza la Usalama lakutana kuhusu kudumisha Amani na Usalama wa Kimataifa
UN Photo/Manuel Elías
Baraza la Usalama lakutana kuhusu kudumisha Amani na Usalama wa Kimataifa

Mashambulizi ya Houthi katika Bahari ya Shamu, Baraza la Usalama lalaani vikali

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jioni Jumatano hii saa za New York Marekani limepitisha azimio la kulaani "kwa maneno makali" mashambulizi mengi ya waasi wa Houthi katika pwani ya Yemen ambayo yamevuruga biashara ya kimataifa na kuzusha hofu ya kuongeza mzozo zaidi mawanda ya vita inayoendelea Gaza. 

Urusi kwanza ilipendekeza marekebisho matatu kwenye rasimu hiyo lakini yote yameshindwa, na hivyo kuandaa njia ya kupigia kura rasimu ya azimio hilo. Kulikuwa na kura 11 za ndio, hakuna iliyopinga, na nchi nne hazikupiga kura: China, Russia, Algeria na Msumbiji

Mkutano huo unafuatia mkutano wa dharura na mashauriano wiki iliyopita ili kushughulikia tishio linaloongezeka linaloletwa na mashambulizi ya wanamgambo katika mojawapo ya njia kuu za usafirishaji duniani. 

Mapema leo Marekani imeripoti kwamba pamoja na vikosi vya wanamaji vya Uingereza imetungua ndege zisizo na rubani 21 na makombora yaliyorushwa na waasi wa Houthi kutoka Yemen siku ya jana Jumanne katika eneo la kusini la Bahari ya Shamu. 

Kumekuwa na zaidi ya dazeni mbili za mashambulizi tofauti dhidi ya meli za kimataifa zinazofanywa na waasi wanaodhibiti sehemu kubwa ya Yemen, tangu mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas yalisababisha mashambulizi ya Israel huko Gaza. 

Wahouthi wanadhibiti mji mkuu Sana'a na maeneo makubwa ya nchi, ikiwa ni pamoja na pwani ya Bahari ya Shamu. Walianza kulenga kile wanachoamini kuwa meli zinazoelekea Israel katikati ya mwezi wa Novemba baada ya mara ya kwanza kurusha mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel yenyewe, ili kuunga mkono kundi la itikadi kali la Hamas. 

Sasa wamepanua lengo lao kwa makampuni yote ya kimataifa ya meli, hadi, wanasema, pale ambapo Israeli itaruhusu misaada kamili ya kibinadamu kuingia Gaza, na hatua yao hiyo imesababisha makampuni mengi kuelekeza meli kuelekea kusini kuzunguka Cape of Good Hope kule Afrika Kusini, na hivyo kuongeza gharama na kutishia kuvuruga mnyororo mzima wa ugavi wa kimataifa. 

Wanachama wa baraza hapo awali walilaani katika taarifa kwa vyombo vya habari tarehe 1 Desemba 2023 walilaani mashambulizi ya Houthi na kutaka kuachiliwa kwa Kiongozi wa Meli ya Galaxy iliyosajiliwa Japan na wafanyakazi wake.