Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaweza kufikia kinu cha kusagisha nafaka cha Red Sea

Nafaka zilizohifadhiwa huko Dhubab, jimbo la Taiz nchini Yemen. WFP kwa muda mrefu ilikuwa imeshindwa kufikia nafaka iliyokuwa imehifadhiwa kwenye kinu cha kusagisha unga cha Red Sea na hivyo kutia shaka pengine itakuwa imeoza
Giles Clarke/OCHA
Nafaka zilizohifadhiwa huko Dhubab, jimbo la Taiz nchini Yemen. WFP kwa muda mrefu ilikuwa imeshindwa kufikia nafaka iliyokuwa imehifadhiwa kwenye kinu cha kusagisha unga cha Red Sea na hivyo kutia shaka pengine itakuwa imeoza

WFP yaweza kufikia kinu cha kusagisha nafaka cha Red Sea

Msaada wa Kibinadamu

Hatimaye shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limepata fursa kwa mara ya kwanza kabisa tangu mwezi Septemba mwaka jana kufikia kinu cha kusagisha nafaka cha Red Sea nchini Yemen.

Msemaji wa WFP mjini Geneva, USwisi, Herve Verhoosel amesema WFP kwa kipindi chote hicho haikuweza kufikia kinu hicho na hivyo kushindwa kusagisha tani 51,000 za ngano kwa ajili  ya kulisha watu watu milioni 3.7 kwa kipindi cha mwezi mmoja.

“Tumechukua sampuli ya ngano na kuiwasilisha maabara ili kuchunguza ubora wake na tunasubiri matokeo. Unga wa ngano umeshambuliwa na wadudu jambo ambalo tulitarajia. Tunahitaji kupulizia dawa ngano hiyo. Hatujaona uharibifu wowote uliosababishwa na maji, jambo ambalo ni dalili njema.”

Hata hivyo Bwana Verhoosel amesema kwa ujumla kinu hicho hakijaharibika licha ya kuwepo kwa dalili za kushambuliwa.

Amesema majenerea kwenye ghala hilo yanafanya kazi, zaidi ya lita 30,000 za dizeli bado zipo na kwamba ziara yao siku ya jana kwenye ghala hilo ni hatua kubwa ya kwanza katika kupata fursa ya kuweza kulifikia ili kupulizia dawa ngano na kuanza kuisagisha.

“Ili kufanya hivyo tunahitaji njia salama kwa wafanyakazi wa WFP na wa kinu hicho kuweza kufika. Itachukua wiki kadhaa za kuweza kufanikisha hilo ili kazi ya kusagisha iweze kurejea katika hali ya kawaida.”

Katika kipindi chote hicho ambacho WFP haikuweza kufikia kinu hicho, Bwana Verhoosel amesema wamekuwa wakitegemea akiba  ya ngano kutoka mataifa mengine na kuagiza kwa njia ya barabara na bahari kutoka nchini Oman.