Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu athari za kuongezeka shughuli za kijeshi katika Bahari ya Shamu

Mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu yametatiza sana usafirishaji kwa njia ya maji kimataifa. (maktaba)
© Unsplash/Angus Gray
Mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu yametatiza sana usafirishaji kwa njia ya maji kimataifa. (maktaba)

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu athari za kuongezeka shughuli za kijeshi katika Bahari ya Shamu

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya mkutano wake wa kwanza wa wazi kuhusu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na waasi wa Houthi katika Bahari ya Shamu, ambayo yanazidi kuwa tishio kwa biashara ya kimataifa na uthabiti wa eneo zima huku vita kati ya Israel na wapiganaji wa Palestina huko Gaza vikiendelea. Fuatilia mkutano kwenye UN Web TV.

Katika muktadha wa mzozo wa Gaza, kuongezeka kwa shughuli za kijeshi katika Bahari ya Shamu na vitisho vinavyoendelea dhidi ya usafiri baharini, kutokana na Houthi ambao wanadhibiti sehemu ya Yemen, kunatia wasiwasi mkubwa, Khaled Khiari Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Idara za Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani amelieleza Baraza la Usalama leo.

"Umoja wa Mataifa unaendelea kuonya kuhusu athari mbaya za kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kibinadamu za kuongezeka kwa shughuli za kijeshi katika Bahari ya Shamu na hatari ya kuzidisha mivutano ya kikanda," ameeleza Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Khaled Khiari wakati wa mkutano wa Baraza uliolenga yanayoendelea hivi karibuni katika Bahari ya Shamu.

"Vitisho vinavyoendelea vya Houthi kwa usafiri wa baharini, pamoja na hatari ya kuongezeka zaidi kwa shughuli za kijeshi, bado vinatia wasiwasi mkubwa na vinaweza kuathiri mamilioni ya watu nchini Yemen, kanda na kote ulimwenguni," ameongeza.

Tangu suala hili lilipowekwa mara ya mwisho kwenye ajenda za Baraza la Usalama mnamo Desemba 18, Wahouthi wamedai kuhusika na mashambulizi mawili ya makombora ya majini dhidi ya Meli ya MSC United mnamo Desemba 26 na dhidi ya Maersk Hangzhou tarehe 31 Desemba. Mashambulizi mengine ya Houthi pia yalizuiliwa kabla ya kitokea, kiongozi huyo ameeleza.

Kuingilia kati kwa vikosi vya Marekani

Mnamo Desemba 31, uingiliaji wa kijeshi wa vikosi vya Marekani dhidi ya Houthi kutokana na ombi la msaada kutoka kwa meli ya Maersk Hangzhou ya makontena ikiwa na bendera ya Singapore, ulisababisha vifo 10 kwa mujibu wa Houthi. Kutokana na hali hiyo,tarehe 2 Januari 2024 kampuni ya usafirishaji  ya Maersk imesitisha usafirishaji katika Bahari ya Shamu hadi hadi itakapotangaza tena.

Siku hiyo hiyo, kampuni ya meli ya Hapag-Lloyd ilisema itaendelea kuepuka kupitia Bahari ya Shamu na kuelekeza meli zake kuzunguka kusini mwa Afrika (Cape of Good Hope) hadi Januari 9.

Kwa mujibu wa Bwana Khiari, huu ni mfano mmoja tu wa hatari zinazohusishwa na kuendelea kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya meli za wafanyabiashara na athari zake kwa minyororo ya kimataifa ya usambazaji bidhaa, hasa kuongezeka kwa gharama za mizigo na kuongezwa kwa muda wa ufikishaji mizigo kwa wateja.

"Tunasisitiza kwamba matukio kama haya kutoka maeneo yanayodhibitiwa na Houthi wa Yemen lazima yakome. Hakuna sababu au malalamiko yanayoweza kuhalalisha kuendelea kwa mashambulizi haya dhidi ya uhuru wa usafiri baharini.” Amesisitiza Khaled Khiari.