Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 6.3 nchini Ukraine wanaendelea kuwa wakimbizi: UNHCR

Basi la Umoja wa Mataifa likiwachukua wakimbizi wa Ukraine kutoka Moldova hadi Romania. (Maktaba)
Victor Lacken/Lensman.eu
Basi la Umoja wa Mataifa likiwachukua wakimbizi wa Ukraine kutoka Moldova hadi Romania. (Maktaba)

Watu milioni 6.3 nchini Ukraine wanaendelea kuwa wakimbizi: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Takriban miaka miwili baada ya uvamizi kwa Urusi nchini Ukraine, wakimbizi wapatao milioni 6.3 kutoka Ukraine wamesalia kuwa wakimbizi baada ya kufurushwa katika makazi yao, wengi wao ambao ni milioni 5.9 wakiwa barani Ulaya limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Hii ni pamoja na wakimbizi wa ndani milioni 3.7 nchini Ukraine. 

UNHCR imesema “Hili bila shaka linaifanya Ukraine kuwa mojawapo ya nchi zinazozalisha wakimbizi wengi zaidi na ina maana kwamba takriban robo ya watu nchini humo wametawanywa.”

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarsh anesema “Ndani ya Ukraine, mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka, kwani mashambulizi ya makombora yanazidi kuwalenga raia na miundombinu ya kiraia, kama ilivyoonekana katika wiki zilizopita. Hali ya baridi imeongezeka hadi kufikia hali ya kuganda na mamilioni wanaendelea kukabiliwa na ukosefu wa usalama, haswa katika maeneo yaliyo mstari wa mbele.”

Nchi zinazohifadhi wakimbizi

UNHCR imesema “Tuna wasiwasi kwamba wakimbizi wengi wanaanguka kwenye nyufa. Tunakaribisha upanuzi wa wigo wa ulinzi wa muda katika Muungano wa Ulaya hadi Machi 2025, lakini lazima mkazo ubakie katika kujumuisha walio hatarini zaidi katika mifumo ya kitaifa katika nchi mwenyeji.”

Katika mfululizo wa tafiti za wakimbizi, UNHCR imekuwa ikitathmini na kuangazia changamoto zinazowakabili wakimbizi wa Ukraine wakiwa uhamishoni. 

Imesema ingawa wengi wanatumai kurejea Ukraine siku moja, ni asilimia 14 pekee wanapanga kufanya hivyo katika siku za usoni. 

Masuala ya usalama yanasalia kuwa makubwa, pamoja na upatikanaji wa huduma za msingi, nyumba na maisha. 

Shirika hilo limesisitiza kuwa “Wakimbizi hawapaswi kuhisi kulazimishwa kurudi kwa sababu tu hawawezi kujikimu na kuchangia wanapokuwa uhamishoni.”

Limeongeza kuwa wakimbizi wengi wanapanga kubaki katika nchi wanayoishi sasa, ambapo wanahitaji usaidizi endelevu kutoka kwa serikali zinazowapokea na jumuiya ya kimataifa ili kukidhi mahitaji yao ya msingi, kupata huduma muhimu na kujenga uwezo wao wa kujitegemea na kujumuishwa kwa maana katika jamii zinazowapokea.

Asilimia 62 ya idadi ya wakimbizi ni wanawake na wasichana na asilimia 36 ni watoto. 

Muundo huu wa umri na jinsia, pamoja na idadi kubwa ya familia za mzazi mmoja, unaonyesha hatari kubwa ya unyanyasaji wa kijinsia limeonya shirika la UNHCR.

UNHCR hali ndani ya Ukraine

Kwa mujibu wa UNHCR takriban watu milioni 16.9 nchini Ukraine wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa dharura. 

Ufadhili wa kibinadamu lazima uendelezwe ili kukabiliana na mahitaji ya dharura ya kibinadamu katika majimbo ya mstari wa mbele na kusaidia watu walioathirika na vita.

Wakati vita ikiendelea bila kikomo, watu tayari wanafanya kazi ya kujenga upya nyumba na maisha katika sehemu za nchi ambazo hazijakabiliwa na uhasama wa moja kwa moja.

Ukraine imeshuhudia kuongezeka kwa mashambulizi ya makombora ya raia na miundombinu ya kiraia katika wiki zilizopita. 

UNHCR na washirika wamekuwa wakichukua hatua, wakitoa usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, vifaa vya ujenzi kukarabati nyumba zilizoharibiwa, na vitu muhimu vya msaada na msaada wa msimu wa baridi kama vile mablanketi.

Jumatatu ijayo UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA watazindua mpango maalum wa msaada kwa Ukraini kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.