Mvua yaleta madhara kambini Cox’s Bazar, UN yasaidia wakimbizi

Mvua kubwa iliyonyesha mfululizo kwa siku tatu kwenye makazi ya wakimbizi warohingya kutoka Myanmar huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh imeharibu makazi 273 na kujeruhi watu 11 kwenye eneo hilo ambalo ni makazi ya wakimbizi zaidi ya 900,000.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mvua kubwa ilinyesha kwa saa 72 kuanzia Jumatatu na mvua zaidi inatarajiwa wiki hii wakati huu ambapo imesalia miezi minne kabla ya kuanza kwa msimu wa pepo za monsuni.
Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi, Charles Yaxley amewaambia waandishi wa habari kuwa kumekuwepo na matukio 26 ya maporomoko ya udongo huku wafanyakazi wa kujitolea waliopatiwa mafunzo na UNHCR wakifanya kazi usiku kucha kusaidia familia zenye mahitaji na kwamba, “katika maeneo mengine, hii inahusisha kuokoa wakimbizi kutoka kwenye makazi yaliyoharibiwa kwa maporomoko ya udongo. Watu 2,137 tumewahamishia kwa muda maeneo mengine kwa kuwa pengine makazi yao yameharibiwa au kwa sababu ya kuchukua tahadhari.”
Nalo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP tayari limeshachukua hatua kusaidia manusura wa mvua hiyo kubwa huko Cox’s Bazar ambapo limesambaza biskuti zenye virutubisho na vyakula vya moto kwa watu 4,889.
Herve Verhoosel ambaye ni msemaji wa WPF mjini Geneva, Uswisi amewaambia waandishi wa habari kuwa,“WFP itaanza mapema mzunguko wake wa mgao wa mchele, kunde na mafuta ili familia ziweze kupata mgao mpya kuanzia kesho Jumamosi. Tuna tani 65 za ujazo za biskuti zenye virutubisho ambazo zimehifadhiwa kwenye maeneo ambayo yana hatari zaidi huko kambini, biskuti ambazo zinaweza kulisha watu zaidi ya 160,000 wakati wa dharura.”
Kuhusu ukarabati, Bwana Verhoosel amesema tayari kuna vibarua 400 ambao wamehamasishwa kusaidia kazi ya ukarabati maeneo ya miinuko ambayo yameporomoka akisema kazi yao kubwa awkati wa maandalizi ya pepo za monsuni ni ukarabati na kurekebisha maeneo badala ya kuanza miradi mipya.
Amesema WFP kila mwezi inaajiri takribani wakimbizi 2,500 kupitia mradi wake wa fanya kazi upate fedha ambapo vibarua hao wanasaidia ukarabati wa maeneo ya kambi hiyo.
Tangu mwezi Januari mwaka huu wa 2019, wakimbizi 21,000 wameajiriwa kupitia mpango huo.
Wakimbizi hao wa kabila la warohingya kutoka Myanmar walianza kuingia Bangladesh mwezi Agosti mwaka 2017 kufuatia mashambulizi dhidi yao huko jimboni Rakhine.