Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde tusisahau madhila ya warohingya- UNHCR 

Kambi ya Cox's Bazar inayohifadhi warohingya nchini Bangladesh.
IOM/Mashrif Abdullah Al
Kambi ya Cox's Bazar inayohifadhi warohingya nchini Bangladesh.

Chonde chonde tusisahau madhila ya warohingya- UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuelekea mkutano wa wahisaji kwa ajili ya ombi la kusaidia wakimbizi wa kabila la warohingya tarehe 18 mwezi huu wa Mei, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuazimia upya msaada na mshikamano wao na warohingya. 

Msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema, ombi hilo la dola milioni 943 linajumuisha jitihada za pamoja za serikali ya Bangladesh inayohifadhi wakimbizi hao, mashirika 134 ya Umoja wa Mataifa na ya kiraia na linalenga kusaidia watu milioni 1.4 mwaka huu wa 2021. 

Wanufaika hao ni pamoja na wakimbizi 880,000 na wenyeji 472,000 wanaoishi katika maeneo jirani na eneo la Cox’s Bazar. 

Bwana Mahecic amesema kwa kuzingatia kuwa mzozo wa Mynamar umetimiza miaka minne sasa, Bangladesh inahitaji msaada endelevu wa kimataifa ili kuhakikisha usalama na ustawi wa warohingya ambao hawana utaifa. 

Amesema, “hili halipaswa kuwa janga linalosahaulika. Wote wakimbzi warohingya na wenyeji wao wabangladesh ambao wamewakarimu kwa miongo kadhaa wanapaswa kuona dunia inashikamana nao.” 

Janga la COVID-19 limekuwa kama “chumvi katika kidonda” na kuongeza hali ya wakimbizi kuwa hatarini zaidi. 

Msemaji huyo wa UNHCR amefafanua kuwa, “Hii leo serikali ya Bangladesh kwa msaada wa mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu, imeweza kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti kusambaa wa COVID-19 kwenye kambi za wakimbizi na maeneo jirani, ingawa mwelekeo wa maambukizi hauwezi kutabirika.” 

Mwaka jana Umoja wa Mataifa uliomba dola bilioni 1 kukidhi mahitaji ya warohingywa na jamii wenyeji huko Cox’s Bazar lakini ombi hilo lilitekelezwa kwa asilimia 59.4 pekee.