Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkulima Kenya: Mradi wa IFAD umenisaidia baada ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi

Francis Njoroge, Mkulima kutoka Muranga nchini Kenya.
IFAD
Francis Njoroge, Mkulima kutoka Muranga nchini Kenya.

Mkulima Kenya: Mradi wa IFAD umenisaidia baada ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Mradi wa kilimo endelevu unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Kilimo, IFAD na Serikali ya Kenya ambao unalenga kukuza miche ya miti na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi umeleta manufaa kwa wakulima wadogo kutoka eneo la Kaunti ya Kiambu nchini Kenya na kuboresha ukulima wao. Mkulima mdogo Francis Njoroge ni mmoja wa mamilioni ya wakulima wadogo wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi lakini kwa bahati nzuri, amefaidika na Mfuko wa Upper Tana Nairobi Water Fund unaolenga kukuza miche ya miti na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Francis anaotesha miche ya parachichi na matunda mengine ili kuwauzia wakulima wengine katika eneo lake. Anaeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni kitu halisi, “Katika miongo michache iliyopita hapa Kenya, tumekuwa na ukame wa muda mrefu na mvua kidogo au hakuna kabisa.” 

Mwaka wa 2022, IFAD ilimwalika Francis kushiriki katika Mkutano wa 27 wa Kimataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianachi, COP 27 nchini Misri, kuona kile ambacho mashirika na viongozi wa dunia wanafanya kusaidia watu kama yeye. Mbali na kukutana na watu wapya, alikuwa sehemu ya jopo ambapo alizungumza kuhusu uzoefu wake mwenyewe na mabadiliko ya tabianchi. 

 "Nadhani kulikuwa na mazungumzo mengi yanayoendelea lakini hatua ni ndogo sana. Mwaka huu, tunahitaji kuhakikisha kuwa fedha zaidi za mabadiliko ya tabianchi zinawekezwa kwa wakulima wadogo wadogo, kama mimi hapa Kenya, ambao wako mstari wa mbele wa mabadiliko ya tabianchi”.  

Francis Njoroge, Mkulima mdogo nchini Kenya akikagua mradi wake wa maji uanomsaidia katika ukulima na ufugaji.
IFAD
Francis Njoroge, Mkulima mdogo nchini Kenya akikagua mradi wake wa maji uanomsaidia katika ukulima na ufugaji.

Francis ameshuhudia kwa muda mrefu ambacho yeye na wakulima wenzake wamepitia, ameshuhudia biashara yake ikiathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, anasema, “Hapa Murang’a nilikuwa nikitegemea mvua tu kuotesha miche yangu. Ikiwa mvua haikunyesha, sikuweza kumwagilia miche yangu kila wakati, na ingekufa." 

Kupitia Mfuko wa Upper Tana Nairobi Water Fund, IFAD na serikali ya Kenya wakulima kama Francis wameweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. IFAD ilipokutana naye kwa mara ya kwanza mwaka jana, shamba lake lilikuwa limefaidika sana kutokana na umwagiliaji, 

“Baada ya kufunga pampu ya maji niliweza kuwa na lita za ujazo za maji 50,000. Miezi inaweza kupita bila mvua lakini sasa ninaweza kuvuna maji”. 

Kwa faida ya miche yake, aliweza kupanua shamba lake na anasema, 

Kupitia mfuko wa maji, niliweza kupata mafunzo ya bure ya jinsi ya kutengeneza sileji na niliweza kuanza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.” 

Francis Njoroge, Mkulima kutoka Muranga nchini Kenya.
IFAD
Francis Njoroge, Mkulima kutoka Muranga nchini Kenya.

Francis anatafakari yale aliyashuhudia baada ya ushiriki COP27, aligundua jinsi yeye pia angeweza kutekeleza sehemu yake katika mabadiliko ya tabianchi. 

“Misri ni nchi kame yenye mvua kidogo sana. Wameweza kuvumbua na kuishi. Nchini Kenya, tuna maji mengi ya mvua. Tunahitaji kujifunza jinsi ya kuvuna na kudhibiti mvua tulionayo. Sasa ninapanua tanki langu la maji hadi lita za ujazo 100,000 ili kukuza miti zaidi.” 

Shukrani sana kwa IFAD na wadau wengine kwa ufadhili na mafunzo ya kilimo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wadogo kama Francis Njoroge, ili kuboresha kilimo chao na maisha yao licha ya changamoto za ukame na mafuriko, na bila shaka wakulima wengine waliohudhuria COP28 huko Dubai, Falme za kiarabu, kwani watakuwa na mengi chanya ya kusimulia mwaka huu.