Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuhusu majanga ni hali ya usipoziba ufa utajenga ukuta -ripoti ya FAO

Wakulima wadogowadogo.
Photo: FAO
Wakulima wadogowadogo.

Kuhusu majanga ni hali ya usipoziba ufa utajenga ukuta -ripoti ya FAO

Tabianchi na mazingira

Wakulima maskini wanaweza kupata faida za kiuchumi na faida zingine kwa kutekeleza mifumo bora ya kilimo inayolenga kuimarisha uwezo wao katika kukabiliana na majanga na misukosuko ya asili, imesema ripoti mpya ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina “Kupunguza hatari za majanga katika kiwango cha mashambani: Faida mujarabu, bila majuto” imetolewa katika kikao kandoni mwa jukwaa la shirika la Umoja wa Mataifa  la upunguzaji wa athari za majanga UNISDR linaloendelea mjini Geneva, Uswisi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo shughuli nyingi za ubunifu wa kukabiliana na majanga zilizotathminiwa na FAO kupitia majaribio ya miaka kwenye mashamba 900 katika nchi 10 tofauti zinaweza kupatikana kwa haraka na wakulima maskini na hazihitaji uwekezaji wa juu na kwamba isitoshe sio tu kwamba ubunifu huo ni kinga ya athari za majanga lakini katika matukio mengi zinaimarisha mazao na kuongeza kipato hata wakati hakuna janga la asili.

FAO kupitia ripoti hiyo imependekeza baadhi ya mambo ambayo wakulima wanaweza kuyafanya ikiwemo kupanda mikoko ili kulinda maeneo ya pwani kutokana na mafuriko, kutumia aina ya mpunga usioathiriwa na mafuriko, kugeukia mifumo ya kuvuna maji na mifumo ya umwagiliaji maji.

Ripoti imetanabaisha kwamba juhudi za kukabiliana na majanga mashambani (DRR) zina faida za kiuchumi na kwamba kuwekeza kwenye DDR mapema kunaweza kuokoa fedha ambazo zingetumika kukabiliana na madhara ya majanga.

Tathmini hiyo iliyofanywa na FAO inawalenga wakulima kukabiliana na hatari na kutaarifa watunga sera ikizingatiwa kwamba watu bilioni 2.5 duniani kote wanategemea kilimo kidogo.

Faida dhahiri, suluhu zinazogharimika

Kwa wastani shughuli za DRR zilizotathminiwa zilikuwa na faida mara 2.2 zaidi kuliko mifumo iliyokuwa ikitumika na wakulima awali ikiwemo ongezeko la mazo na kuzuia hatari za majanga.

Aidha FAO imesema shughuli kama hizo zinaweza kuzuia hasara katika kaya na faida za papo hapo kwa mabilioni ya wat una zinaweza kuleta faida za kiuchumi katika viwango vya kikanda na kitaifa.

Juhudi zaidi zinahitajika

Ripoti hiyo ya FAO inapendekeza uwekezaji wa juhudi za kinga dhidi ya madhara ya majanga kuliko gharama kubwa ya kukabiliana na madhara yatokanayao na majanga ambapo shirika hilo limependekeza kusonga kutoka miradi ya kilimo kidogo hadi utekelezaji mkubwa zaidi.

Kwa mantiki hiyo imetoa mwongozo wa njia mbili, moja ni kutoka kwa mkulima hadi mwingine ambapo wakulima katika jamii aua eneo wanaweza kuchukua mifumo inayofanywa na jirani zao ambapo uwekezaji mdogo tu ndio unahitajika, pili ni kutekeleza DRR kwa mapana.

FAO imesisitiza kwamba njia zote mbili zinahitaji miundomsini thabiti, uwekezaji toshelezi na maingira mazuri. Aidha sera za kuendeleza kilimo, mipango na shughuli zingine zinapaswa kuzingatia upunguzaji wa hatari dhidi ya majanga kama kipaumbele.