Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lebanon: Haki imetendeka, Mahakama Maalum yafunga pazia, Guterres atuma shukrani

Hukumu ikisomwa wakati wa kesi dhidi ya Ayyash na wenzake baada ya kupatiakana na hatia ya mauaji kwenye shambulio la mwaka 2005 huko Beirut, Lebanon. (Maktaba)
Mahakama Maalum kwa Lebanon
Hukumu ikisomwa wakati wa kesi dhidi ya Ayyash na wenzake baada ya kupatiakana na hatia ya mauaji kwenye shambulio la mwaka 2005 huko Beirut, Lebanon. (Maktaba)

Lebanon: Haki imetendeka, Mahakama Maalum yafunga pazia, Guterres atuma shukrani

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amepongeza kazi kubwa na ngumu iliyofanywa na majaji na wafanyakazi wa Mahakama Maalum kwa ajili ya Lebanon, iliyoanzishwa kuwajibisha wahusika wa shambulio la Februari 14 mwaka 2005 huko Beirut. Mahakama hiyo imemaliza muda wake leo Jumapili Desemba 31, baada ya kufanya kazi kwa miaka 14.

Mahakama hiyo ilianzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa azimio namba 1757 la mwaka 2007 kwa ajili ya kusimamia mashtaka dhidi ya wahusika wa shambulio hilo  lililosababisha vifo vya watu 22 akiwemo Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri. Watu wengine 226 walijeruhiwa katika shambulio .

Majukumu maalum ya Mahakama hiyo iliyozinduliwa rasmi mwaka 2009, yaliongezwa ili kujumuisha pia mashambulio mengine ambayo kimahakama yalibainika kuhusika na shammbulio la Beirut.

Mauaji ya Hariri, yaliyojumuisha vilipuzi vyenye baruti kali zenye uzito wa kati ya kilo 2,500 hadi 3,000. Vilipuzi hivyo vililipuliwa wakati msafara wa Hariri ukipita katikati ya mji mkuu Beirut, na kusababisha shimo kubwa lenye upana wa mita 11.

Mahakama ilikuwa huru

Makao makuu yalikuwa kwenye viunga vya mji wa The Hague nchini Uholanzi na majaji wake walikuwa wa kimataifa na pia kutoka Lebanon.

Iliweza kushtaki watuhumiwa kwa kutumia sheria ya Lebanon, lakini haikuwa sehemu ya mfumo wa mahakama wa Lebanon na haikuwa Mahakama ya Umoja wa Mataifa.

Iliendesha kesi na kumhukumu bila kuweko mahakama Salim Jamil Ayyash kwa kuhusika na shambulio la mwaka 2005, ambapo alihukumiwa hukumu tano za kifo mwaka 2020. Mwaka 2022, mahakama ilibadili uamuzi wake wa kumuachilia huru Hassan Habin Merhi na Hussein Hassan Oneissi na kuwakuta wote na hatia.

Hata hivyo wote watatu hadi sasa hawajulikani waliko.

Hukumu ya kurasa 2,641

Kesi ilivunja rekodi kwa kuwa na ushahidi kutoka mashuhuda 297 na maonesho 3,135 ya vidhibiti na kuwa na jumla ya kurasa 2,641 ya hukumu, ambapo muhtasari wa hukumu ulichapishwa kwenye wavuti wa mahakama kwa lugha za Kiarabu, Kiingereza na Kifaransa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema “fikra zangu zinaendeleakuwa na manusura na familia za waliopoteza maisha wakati wa shambulio la Februari 14, 2005 na mashambulio mengine yanayohusiana nayo,” imesema taarifa iliyotolewa na Stéphane Dujarric, Jumamosi usiku.

“Katibu Mkuu ameelezea shukrani zake za dhati za kujitoa kwa moyo na kwa bidii kwa majaji na wafanyakazi wa Mahakama hiyo Maalum, serikali ya Uholanzi kama nchi mwenyeji na wanachama wote waliofadhili."