Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa vifaa na mafunzo kupambana na COVID-19 Beirut 

Muuguzi akichunguza joto ya mtoto katika kituo cha afya Beirut, Lebanon wakati huu wa mlipuko wa COVID-19
© UNICEF/Fouad Choufany
Muuguzi akichunguza joto ya mtoto katika kituo cha afya Beirut, Lebanon wakati huu wa mlipuko wa COVID-19

WHO yatoa vifaa na mafunzo kupambana na COVID-19 Beirut 

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linatoa msaada wa aina mbalimbali kusaidia vita dhidi ya janga la corona au COVID-19 nchini Lebanon hasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa  baada ya milipuko iliyotokea mwezi Agosti mwaka huu mjini Beirut.

Mjini Beirut hospitali ya chou kikuu cha Rafik Hariri ni moja ya hospitali kubwa za umma zinazopokea na kutibu idadi kubwa ya wagonjwa wa COVID-19.   

Kwa mujibu wa mwakilishi wa WHO nchini Lebanon Dkt. Iman Shankiti idadi ya wagonjwa wa COVID-19 imeongezeka sana baada ya milipuko ya Agosti 4 mjini Beirut kwani kabla ya mlipuko huo wagonjwa walikuwa kati ya 5000-6000 lakini sasa idadi ni kubwa zaidi. 

Na ili kudhibiti hali hiyo WHO imeamua kutoa msaada wa hali na mali katika hospitali za umma ikiwemo hospitali hii ya Rafiki Hariri msaada ambao ni pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa afya, vifaa muhimu vikiwemo vya upimaji na utaalamu wa kiufundi. Dkt . Shankiti anaongeza “Hii ilikuwa ni hospitali ya kwanza nchini Lebanon ambayo ilikuwa na uwezo wa kupima corona mara moja baada ya kisa cha kwanza kubainika” 

Hospitalini hapa mbali ya kupewa msaada wa vipimo vya COVID-19 WHO pia imeisaidia hospitali kuandaa kitengo cha dharura  cha wagonjwa mahtuti na wodi nzima ya kutibu wagonjwa waliobainika kuwa na COVID-19. 

Dkt. Firass Abiad ni mwenyekiti wa bodi na mkurugenzi wa hospitali ya Rafik Hariri anasema,“WHO imesaidia katika maeneo mengi, vifaa, msaada wa mafunzo, kutoa kanuni, na vitu vingine vilivyoisaidia hospitali yetu kufanya vipimo. Pia WHO imetuunganisha na wataalam mbalimbali duniani ambao wameturuhusu kutumia ujuzi wao katika juhudi na maandalizi yetu.” 

Hata kabla ya COVID-19 kuingia Lebanon WHO kwa kushirikiana na wizara ya afya la Lebanon waliandaa vifaa mbalimbali, vipimo, mambango ya uelimishaji na hatua za kujikinga wakiwalenga raia wa Lebanon na jamii za wakimbizi.