Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulemavu wa kutokuona haujazima ndoto zao za kuwa walimu

Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi tena mwenye ulemavu wa kutoona akisoma kwa kupitia maandishi maalum ya watu wasioona.
© UNICEF/Pirozzi
Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi tena mwenye ulemavu wa kutoona akisoma kwa kupitia maandishi maalum ya watu wasioona.

Ulemavu wa kutokuona haujazima ndoto zao za kuwa walimu

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Lebanoni, wakimbizi wawili ndugu kutoka Syria, pamoja na ulemavu wa kutoona, wameamua kujiendeleza kielimu kwa kujifunza lugha ya kifaransa na maarifa mengine katika mfumo wa kawaida wa shule za umma. 

Hawa ni ndugu wawili, Ahmad Al Aansour na Alaa Al Aansour, kutoka Syria lakini sasa wakiishi ukimbizini Lebanon. Siyo maisha ya ukimbizi wala ulemavu wa macho ambao umewazuia kujiendeleza kimasomo.

Alaa anatumia simu kuukuu ya mkononi au rununu, aliyopewa zawadi kutoka kwa mjomba wake,“Nilianza kwa kujifunza herufi. Nilijikita kwenye herufi. Kwanza nilikuwa nabonyeza kitufe kwenye simu, yeye ananiambia ni herufi gani, kisha herufi mbili, kisha herufi tatu. Hivyo ndivyo nilivyoanza kuandika maneno, sentensi na baadaye matini nzima”

Kwa upande mwingine, Ahmad ana kumbukumbu ya hali ya juu. Kila siku ndugu hawa wawili wanatembea kwenda katika shule ya umma iliyoko karibu na makazi yao katika  wilaya ya kaskazini ya Akkar. 
 
Wakiwa wanaishi katika kijiji ambako kuna makazi duni na katika mazingira ambayo hakuna vifaa maalumu kwa watu wenye ulemavu wa macho na pia wakiwa hawana uwezo wa kumlipa mtaalamu katika shule za binafsi, hatimaye walipokelewa katika shule ya umma ya Lebanoni ambayo ina madarasa ya jioni kwa ajili ya wakimbizi kutoka Syria.

Alaa ana umri kiasi mkubwa kuliko wanafunzi wenzake darasani lakini walimu wake wamefurahishwa na namna alivyopambana na vikwazo vyote.

“Taratibu ameweza kupambana na matatizo yake. Kigezo kwamba hawezi kuona, hakikumzuia kuendelea, kushikamana, kujaribu kujifunza ili kupata shahada kutoka shule hii, kufanikiwa na kupata alama nzuri. Anashindana hata na wale ambao wana akili sana katika darasa lake”

Alla anarekodi masomo yake katika simu yake na kisha baadaye anajikumbusha na kuyarejea akiwa darasani.

“Elimu ni kila kitu. Sipendi kumwona yeyote akiacha shule”

Ndoto zao ni kuwa walimu wa lugha ya kiarabu, lakini lengo la kwanza ni kumaliza shule.

“Mimi ni mzuri sana kwa lugha ya kiarabu. Ningependa kuandika lakini sijui”

Ndugu hawa wawili wanajua safari yao ilivyo na vikwazo lakini hilo haliwazuii kutimiza ndoto yao.