Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine-Urusi: Baraza la Usalama lakutana kwa dharura

Belgorod mji wa Urusi ulioko mpakani na Ukraine
Unsplash/Petr Magera
Belgorod mji wa Urusi ulioko mpakani na Ukraine

Ukraine-Urusi: Baraza la Usalama lakutana kwa dharura

Amani na Usalama

Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimefanyika alasiri ya Jumamosi tarehe 31 baada ya kuitishwa na Urusi kufuatia mashambulizi huko Belgorod mpakani na Ukraine, mashambulizi ambayo Afisa Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amelaani.

Khaled Khiari ambaye ni Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu kwenye Idara ya Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, UN DPPA, ameliambia Baraza kuwa mashambulizi hayo yamefanyika mapema jumamosi na kusababisha vifo vya raia 18 na zaidi ya 100 wamejeruhiwa.

Urusi iliitisha kikao hicho cha dharura kufuatia mashambulizi hayo kwenye mji huo ulioko takribani kilometa 40 kwenye mpaka wake wa kaskazini na Ukraine, mji ambao ni makazi ya watu 300,000.

Kikao hicho cha dharura kimefanyika chini ya saa 24 tangu Baraza kuitisha kikao kuhusu Ukraine kufuatia mashambulizi makubwa yaliyofanywa na Urusi dhidi ya miji na majiji ya Ukraine.

Tunalaani vikali mashambulizi haya

Khaled Khiari, Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu kwenye Idara  ya Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, UN DPPA, akihutubia Baraza la Usalama
UN
Khaled Khiari, Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu kwenye Idara ya Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, UN DPPA, akihutubia Baraza la Usalama

“Tunalaani dhahiri mashambulizi yote kwenye majiji, miji na vijiji nchini Ukraine na Urusi,” amesema Bwana Khiari. “Mashambulizi dhid iya raia na miundombinu ya kiraia ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu na haikubaliki na lazima yakoseme sasa.”

Amesema hata Baraza linavyokutana leo, ripoti za mashambulizi mapya ya nchini Ukraine kwenye maeneo ya Kharkiv, Sumy, Mykolaiv, Kherson, Cherkasy, Poltava na Dnipropetrovsk.

Bila shaka, saa chache zilizopita, mji wa Kharkiv uliripotiwa kushambuliwa, na kusababisha rai akujeruhiwa, huku miundombinu ya kiraia ikiharibiwa.

Vifo vya raia Belgorod

Bwana Khiari amesema mashambulizi kwenye maeneo ya raia kwenye mji wa Belgorod yameripotiwa kusababisha mauaji na vile vile uharibifu wa miundombinu ya kiraia kama vile Ofisi ya serikali ya mkoa na majengo ya Shule ya kitabibu ya Chuo Kikuu cha Jimbo la Belgorod.

“Mashambulio haya ya karibuni yameripotiwa kuwa makubwa zaidi ya mpakani mwa Urusi tangu Uruti ivamie Ukraine tarehe 24 Februari 2022, vita iliyoanzishwa kinyume na Chata ya Umoja wa Mataifa na Sheria za kimataifa,” amesema Afisa huyo wa UN DPPA.

Ameongeza kuwa mamlaka za kijeshi Urusi nazo zimeripoti shambulio lingine tofauti lililofanywa kwa ndege zisizo na rubani za Ukraine kwenye mikoa ya Bryansk, Oryol, Kursk na Moscow nchini Urusi.

Wakati huo hou, mamlaka za Ukraine zimeripoti mashambulio mapya ya usiku kucha yaliyofanywa na ndege za Urusi zisizo na rubani yakilenga mkoa wa Kherson, amesema Bwana Khiari.

“Kadri vita inavyoendelea, tutaendelea kuona raia wengi zaidi wa Urusi na Ukraine wakiuawa na wakijeruhiwa,” amesema. “Ulinzi wa raia lazima liwe jambo la kipaumbele. Umwagaji damu lazima ukome, vita lazima ikome.”

Vassily Nebenzia, (katikati)  Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye UN akihutubia Baraza  la Usalama
UN
Vassily Nebenzia, (katikati) Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye UN akihutubia Baraza la Usalama

Urusi: EU yafumbia macho ‘shambulio la kigaidi’

Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vassily Nebenzia amesema eneo la kati la mji wa Belgorod ulishambuliwa kwa makombora huku mashambulizi hayo yakitumia vilipuzi vilivyopigwa marufuku kama vile makombora aina ya Vampir yaliyotengenezwa Czech. Maeneo lengwa yalikuwa kituo cha michezo, eneo la kuteleza kwenye theluji na Chuo Kikuu.

“Hakuna kujificha,” amesema. “Nchi za Muungano wa Ulaya zinafumbia macho uhalifu unaotekelezwa na genge la Kyiv,” amesema Balozi Nebenzia ambapo Kyiv anamaanisha Ukraine, kwa kuwa huo ndio mji mkuu wa taifa hilo.

Wajumbe wa Baraza: Raia katu wasilengwe

Wajumbe wa Baraza walilaani kitendo cha raia kulengwa kwenye mashambulio hayo.

Shule zinapaswa kuwa pahala salama kwa ajili ya watoto, alisema Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Falme za kiarabu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mohammed Issa Abushahab.

“Raia wanapaswa kulindwa, na maeneo ya kiraia katu yasilengwe,” amesisitiza.

Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransay kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nicolas de Rivière ‘alishindilia’ hoja iliyoibuliwa na wajumbe kadhaa wa Baraza, akisisitiza kuwa iwapo majeshi ya Urusi hayakuweko kwenye ardhi ya Ukraine, “tusingalikuwako hapa mchana huu.”

Urusi isingalikuweko Ukraine tusingalikuwako hapa

Thomas Patrick Phipps ambaye Afisa kutoka Uwakilishi wa Kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa amesema Urusi inajaribu inajaribu kusaka usawa na kikao cha Ijumaa cha Baraza kufuatia mashambulizi ya Urusi kwenye miji na majiji ya Ukraine.

Hata hivyo Urusi ndio imeanzisha hii vita na inaweza kuimaliza, amesema Phipps.

Wazungumzaji wengi walikubaliana na hoja, wakitoa wito kwa Urusi kuondoka Ukraine na imalize uhasama.

Marekani iliwakilishwa na John Kelly ambaye amesema Urusi yenyewe ndio inawajibika kwa kuanzisha vita, kinyume na Chata ya Umoja wa Mataifa.

“Iwapo Urusi itaendelea kushikilia msimamo, Marekani itaendelea kuunga mkono Ukraine kwenye haki yake ya kujilinda,” amesema Kelly akitoa wito kwa Urusi imalize vita hiyo mara moja, halikadhalika kila upande kwenye mzozo ulinde raia.

Serhii Dvornyk, Kansela na Mratibu wa Masuala ya Kisiasa kwenye Uwakilishi wa Kudumu wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama la UN
UN
Serhii Dvornyk, Kansela na Mratibu wa Masuala ya Kisiasa kwenye Uwakilishi wa Kudumu wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama la UN

Ukraine: Mjiandae kukutana kesho na kila siku iwapo vita itaendelea

Ukraine kwenye kikao iliwakilishwa na Afisa wake Serhii Dvornyk ambaye ameesma bado wana kiwewe kutokana na mashambulizi ya Ijumaa yaliyofanywa na Urusi.

“Saa chache zilizopita, Urusi kwa mara nyingine imeshambulia Kharkiv kwa kutumia kombora aina ya S-300, na kupiga jengo la makazi na hoteli,” amesema akiongeza kuwa “tangu asubuhi hii idadi kadhaa ya miji na vijiji nchini Ukraine vimeshambuliwa na Urusi.”

Ametaja kuwa ni pamoja na Dnipro, Nikopol na Vyshetarasivka kwenye mkoa wa Dnipropetrovsk, Kharkiv, Vovchansk, Kupyansk na Velyka Shpakivka kwenye mkoa wa Kharkiv na Antonivka na Tomina Balka kwenye mkoa wa Kherson.

“Baraza la Usalama lilikutana jana, na leo tena linakutana na muwe tayari kukutana tena kesho, keshokutwa – kila siku iwapo Urusi inaendeleza vita dhidi ya Ukraine,” amesema Afisa huyo.

Pindi ‘Urusi itakapomaliza vita hii katili” hakutakuweko ten ana machungu ya binadamu, hakuna majeruhi na vifo vya raia na hakutakuweko na sababu ya Baraza la Usalama kukutana juu ya suala hili.”