Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikosi cha kwanza cha SADC chawasili DRC kusaidia kukabili mapigano mashariki mwa nchi

Mtoto akiwa katika kambi ya wakimizi wa ndanijimboni Ituri nchini DRC  kufuatia kufurushwa makwao kutkana na mapigano mashariki mwa nchi
© UNICEF/Diana Zeyneb Alhindawi
Mtoto akiwa katika kambi ya wakimizi wa ndanijimboni Ituri nchini DRC kufuatia kufurushwa makwao kutkana na mapigano mashariki mwa nchi

Kikosi cha kwanza cha SADC chawasili DRC kusaidia kukabili mapigano mashariki mwa nchi

Amani na Usalama

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wanajeshi wa kikosi cha kwanza kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC kitakachokuwa na jukumu la kusaidiana na jeshi la serikali, FARDC kujibu mashambulizi kutoka kwa vikundi vilivyojihami mashariki mwa nchi hiyo, wamewasili huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Radio Okapi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, inasema kikosi hicho cha kwanza kiliwasili usiku wa Desemba 26 na kuwasili kwao kunafuatia makubaliano kati ya SADC na DRC yaliyotiwa saini na Rais Felix Tshisekedi na jumuiya hiyo tarehe 17 mwezi uliopita wa Novemba kwenye mji mkuu Kinshasa.

Wakuu wa SADC walipokutana Luanda, Angola tarehe 4 mwezi uliopita wa Novemba walijadili hali ya Usalama Mashariki mwa DRC tangu kuibuka tena kwa mashambulizi kutoka waasi wa M23 na kukubaliana uwezekano wa kutuma jeshi la kikanda kuchukua nafasi la lile la Jumuiya ya AFrika Mashariki ambalo muda wake ulipomalizika Desemba 8 haukuongezwa.

Tarehe 11 mwezi huu wa Desemba wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita alisema, "hatua hizi za kikanda ni za kupongeza.”

Wanajeshi wengine wake kwa waume kutoka SADC wataendelea kuwasili DRC.

Kupelekwa kwa kikosi hicho cha SADC ni kwa mujibu wa Ibara ya 6, kifungu cha 1 cha Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa jumuiya hiyo inayosema, shambulio la kijeshi dhidi ya mwanachama wa jumuiya litachukuliwa kama tishio la ulinzi na usalama. Hivyo kujibu shambulio hilo hatua za pamoja lazima zichukuliwe.