Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Madagascar kwa duru ya kwanza, ya uchaguzi, sasa twasubiri duru ijayo- Guterres

Matembezi ya amani na demokrasia nchini Madagascar. Matembezi hayo yaliandaliwa na wanawake.
Photo: UNDP Madagascar
Matembezi ya amani na demokrasia nchini Madagascar. Matembezi hayo yaliandaliwa na wanawake.

Heko Madagascar kwa duru ya kwanza, ya uchaguzi, sasa twasubiri duru ijayo- Guterres

Amani na Usalama

Kufuatia hatua ya Madagascar kutangaza jana matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo tarehe 7 mwezi huu wa Novemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amepata taarifa hizo na anapongeza wananchi kwa jinsi walivyotekeleza kwa amani haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa Bwana Guterres imemnukuu pia akipongeza taasisi nchini Madagascar hususan tume huru ya taifa ya uchaguzi na Mahakama Kuu kwa uongozi na ueledi wao wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi.

Amekaribisha dhimay a serikali ya Madagascar ya kuhakikisha kuwa upigaji kura ulifanyika katika mazingira mazuri.

Hata hivyo Bwana Guterres ametoa wito kwa wadau wote nchini Madagascar wajizuie wakati huu wanapoelekea katika duru ya pili ya uchaguzi tarehe 19 mwezi ujao wa Disemba.

“Naamini kuwa mivutano yoyote inayoweza kutokea kuhusiana na mchakato wa uchaguzi itashughulikiwa kwa amani na kupitia njia za kisheria,” amesema Katibu Mkuu.

Ametamatisha akisema kuwa ataendelea kufuatilia hatua zinazofuata za mchakato wa uchaguzi kupitia mshauri wake maalum Abdoulaye Bathily, ambaye anashirikiana kwa karibu na wajumbe wa  Muungano wa Afrika, AU na  Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC na kwamba ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Madagascar itaendelea kusaidia wananchi katika kuimarisha demokrasia na maendeleo endelevu.