Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto lukuki zakabili DRC lakini zinaweza kutatuliwa- Bi. Keita

Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC akihutubia Baraza la Usalama la UN 11 Desemba 2023
UN /Eskinder Debebe
Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC akihutubia Baraza la Usalama la UN 11 Desemba 2023

Changamoto lukuki zakabili DRC lakini zinaweza kutatuliwa- Bi. Keita

Amani na Usalama

Taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambalo tarehe 20 mwezi  huu wa Desemba linatarajiwa kuwa na uchaguzi, linakabiliwa na changamoto lukuki lakini si kwamba haziwezi kutatuliwa, amesema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Bintou Keita, siku ya Jumatatu alipohutubia Baraza la Usalama la UN jijini New York, Marekani.

Bi. Keita ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO amesema, “hivi sasa tuko kwenye kipindi muhimu cha uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na DRC, lakini pia ni kipindi muhimu kwa nchi yenyewe. DRC iko kwenye kipindi cha kampeni za uchaguzi, siku tisa kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais, magavana na wabunge, vile vile uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.”

Amesema kipindi hiki kinahitaji pia kuondoka haraka na kwa utaratibu wa vikosi vya MONUSCO ambavyo ripoti ya Katibu Mkuu na mpango wa pamoja wa kuondoka kwa vikosi hivyo imewasilisha mbele ya Baraza la Usalama kwa ajili ya mapendekezo.

Mijadala ya kampeni za uchaguzi yadhihirisha wananchi wana matumaini makubwa

Kwa mujibu wa Bi. Keita, “ingawa changamoto DRC ni kubwa na nyingi, bado si kwamba haziwezi kukabiliwa,” na kwamba “kadri mijadala ya sasa kwenye kampeni za uchaguzi zinavyodhihirisha, wananchi wa DRC wana matumaini makubwa ya uchaguzi huru na wa uwazi, marekebisho pamoja na uwajibikaji wa viongozi wao.”

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja huo wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wakiwa kwenye doria katika kijiji cha Logo mji wa Djugu jimboni Ituri .
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja huo wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wakiwa kwenye doria katika kijiji cha Logo mji wa Djugu jimboni Ituri .

Amesema matamanio hayo na vichocheo vyote vilivyowatia moyo vinaonesha mnepo walio nao na hivyo wanahitaji usadizi wa kina na kamilifu kutoka jumuiya ya kimataifa.

Mkuu huyo wa MONUSCO amesihi kuongezwa kwa muda wa MONUSCO ili kuruhusu kuendelea kwa juhudi hizo za pamoja kwa moyo wa kuheshimiana na kuaminiana.

Usaidizi wa MONUSCO kwenye uchaguzi

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu, amesema yanaendelea vema kwa mujibu wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi, CENI, licha ya changamoto dhahiri za vifaa, kifedha na usalama.

Kama ilivyoombwa na CENI, na kwa mujibu wa majukumu yake, MONUSCO imepatia DRC msaada wa kupeleka vifaa kwenye majimbo ambako bado inaendesha operesheni zake. Tani 50 za vifaa vya uchaguzi vimewasilishwa kwenye maeneo mbali mbali huko kwenye majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

CENI na wagombea uchaguzi

Kwa mujibu wa Bi. Keita, kitendo cha CENI na Mahakama ya Kikatiba kuidhinisha wagombea 26 wa urais, wakiwemo wanawake wawili, ni ishara dhahiri ya ujumuishaji, suala ambalo Umoja wa Mataifa inashukuru na kulikaribisha.

“Hata hivyo, vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia bado yana shaka na wasiwasi juu ya kuchapishwa kwa orodha ya wapiga kura, orodha ambayo bado ilikuwa haijabandikwa kwenye vituo vya kupigia kura hadi tarehe 5 mwezi huu wa Desemba,” amesema Mkuu huyo wa MONUSCO.

Viongozi wanawake na wagombea wa kisiasa wanaendelea kukumbwa na vitisho na kauli zenye lengo la kuwakatisha tamaa wasisishiriki kikamilifu kwenye masuala ya umma - Bintou Keita - Mwakilishi wa UN DRC

Masuala mengine ambayo bado yanatia hofu ni “ubora kadi ya mpiga kura, ugumu wa kupata nakala za nyaraka nchi nzima, ukosefu wa mawasiliano kuhusu namna ya kupiga kura kwa wale ambao vitambulisho au kadi zao za kupiga kura zina kasoro au hawazioni,” mambo ambayo amesema yanaibua kutoaminiana.

Bi. Keita amesema ingawa kampeni za uchaguzi zimeanza kwa amani, huku takribani wagombea wote wa uchaguzi wakiweza kusafiri maeneo mbalimbali nchini humo, bado mapigano makali kati ya wafuasi wa vyama pinzani vya kisiasa yanaendelea kwenye majimbo mengi.

“Viongozi wanawake na wagombea wa kisiasa wanaendelea kukumbwa na vitisho na kauli zenye lengo la kuwakatisha tamaa wasisishiriki kikamilifu kwenye masuala ya umma,” amesema Bi Keita.

MONUSCO hata hivyo kwa upande wake pamoja na mashirika mengine ya UN na wadau wanaendelea kusaidia wanawake na vijana ambao ni wagombea, waangalizi wa uchaguzi na mashuhuda ,kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana kwenye mchakato wa uchaguzi, amesema Mkuu huyo wa MONUSCO.

Kando mwa hayo, kuna ongezeko la habari potofu na kauli za chuki, iwe moja kwa moja au mtandaoni, wakati wa kampeni za uchaguzi na ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na vitendo hivyo huku akisihi serikali iwajibishe wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Usalama kusini mwa jimbo la Kivu Kaskazini unazorota

Mwakilishi huyo wa UN nchini DRC ametaja kuzorota kwa hali ya usalama kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini.

Hali ya usalama, kiutu na haki za binadamu inazidi kuwa mbaya kusini mwa jimbo la Kivu Kaskazini, hasa kufuatia kurejea kwa hali ya chuki na mapigano kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23 tangu mwezi Oktoba mwaka huu  Halikadhalika mashambulizi ya M23 kwenye eneo la Masisi jimboni Kivu Kaskazini tangu kuondoka kwa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki,.

Mvutano kati ya DRC na Rwanda bado ni wa hali ya juu

DRC na Rwanda bado zinaendelea na mvutano mkali na kuna hatari ya kukabiliana kijeshi licha ya juhudi za kikanda na kimataifa kuondoa mvutano huo.

“Bado nina hofu pia kuhusu ongezeko la mvutano hivi karibuni katiya Rwanda na Burundi baada ya makabiliano ya jeshi la Burundi na waasi wa M23 huko Masisi, na hivyo natoa wito wa kumaliza mwendelezo wa mvutano,” ameongeza Bi, Keita.

Kikosi cha EAC kinaondoka, cha SADC kinaingia

Kwa ombi la serikali ya DRC, mamlaka ya jeshi la kikanda kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, ECA, haikuongezwa muda baada ya kumalizika Desemba 8, na hivyo kikosi hicho kimeanza kuondoka.

Na wakati huo huo, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, inajiandaa kupeleka kikosi chake wiki chache zijazo, SAMIDRC, kikosi ambacho kitapatiwa mamlaka ya kujibu mashambulizi.

"Hatua hizi za kikanda ni za kupongeza. Hata hivyo hazitaweza kuzaa matunda bila kuungwa mkono kwa uendelevu na serikali ya DRC, na uwekezaji wa serikali hiyo katika juhudi za kikanda, kitaifa na kimataifa za michakato ya kisiasa ya suluhu za mizozo mashariki mwa taifa hili,” amesema Bi.Keita.