Janga la njaa lanyemelea wakazi milioni 45 ukanda wa SADC

Nchini Zimbabwe ambako wengi wanakabiliwa na ukosefu wa uhakika wa chakula.
WFP/Tatenda Macheka
Nchini Zimbabwe ambako wengi wanakabiliwa na ukosefu wa uhakika wa chakula.

Janga la njaa lanyemelea wakazi milioni 45 ukanda wa SADC

Tabianchi na mazingira

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yakizidi kushika kasi, mashirika ya Umoja wa Mataifa yametaka usaidizi zaidi kwa watu milioni 45 walioko kwenye mataifa 16 wanachama wa jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, SADC kwa kuwa watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Mashirika hayo, lile la mpango wa chakula duniani, WFP, chakula na kilimo, FAO na mfuko wa maendeleo ya kilimo duniani, IFAD wametoa wito huo kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa Johannesburg, Afrika Kusini na Geneva, Uswisi.

“Janga hilo la njaa linalozidi kuenea kila uchao kwenye maeneo ya mijini na vijijini linatokana na ongezeko la bei za vyakula, kufa kwa mifugo na ongezeko la ukosefu wa ajia sambamba na hali inayozidi kukua ya utapiamlo uliokithiri miongoni mwa jamii zilizo  hatarini zaidi, “ amesema Herve Verhoosel, msemaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP mjini Geneva, Uswisi.

Bwana Verhoosel amesema kuna zaidi ya watu milioni 11 wanaokabiliwa na janga hilo au udharura wa kukosa chakula katika mataifa 9 ya SADC ambayo ni  Angola, Zimbabwe, Msumbiji, Zambia, Madagascar, Malawi, Namibia, Eswatini na Lesotho.

“Iwapo watu hawa hawatopatiwa msaada, basi idadi yao inaweza kuongezeka na kufikia milioni 13 mwakani, wakati huu ambapo msimu wa mwambo unafikia kilele,”  amesisitiza Bwana Verhoosel.

Mashirika hayo yamesema kuwa wakati eneo la kusini mwa Afrika lilikuwa na msimu wa kawaida wa mvua katika kipindi kimoja kati ya vitano vya upanzi, ukame uliokithiri, vimbunga vya mara kwa mara na mafuriko, vimeharibu mavuno kwenye eneo hilo ambalo kilimo kinategemea zaidi mvua.

Naye mratibu wa FAO kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika, Alain Onibon amesema kuwa kuchelewa kwa mvua, vipindi virefu vya ukame, vimbunga Idai na Kenneth pamoja na changamoto za kiuchumi vimekuwa vichocheo vya janga la njaa kusini mwa Afrika.

“Jamii za wakulima zitahitaji angalau misimu miwili au mitatu ya kilimo kuweza kurejea katika hali ya kawaida ya uzalishaji hivyo usaidizi wa haraka ni muhimu,” amesema Onibon.

Kwa sasa FAO na WFP yanaharakisha hatua za usaidizi kwenye mataifa hayo 9 yakiwa na lengo la kusaidia zaidi ya watu milioni 11 ifikapo katikati yam waka ujao wa 2020.

Hatua ni pamoja na kukidhi mahitaji ya lishe, kusaidia wakulima wadogo kuimarisha uzalishaji na kupunguza upotevu wa chakula, matumizi bora ya udongo na rasilimali za maji na kuwa na mbinu za kilimo hai pamoja na pembejeo za kilimo, mikopo na kampeni za chanjo kwa mifugoo.

Kwa mujibu wa jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabinachi, viwango vya joto katika nchi 6 za kusini mwa Afrika vitaongezeka maradufu kuliko viwango vya dunia na kuleta mabadiliko makubwa katika miaka ijayo.

Mataifa hayo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Malawi, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.