Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi: Gaza, Sudan, Uchaguzi Mkuu DR Congo

Palestina. Familia ikipika kwenye kifusi cha nyumba yao
© WFP/Ali Jadallah
Palestina. Familia ikipika kwenye kifusi cha nyumba yao

Habari kwa ufupi: Gaza, Sudan, Uchaguzi Mkuu DR Congo

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yameendelea kusisitiza wito wa usitishwaji mapigano katika ukanda wa Gaza kwani hali inazidi kuwa mbaya kila uchao, lile la afya duniani WHO limesema timu yake ilifanikiwa kufika katika hospitali za Al Ahil Arab na Al Shifa Gaza kaskasini na uharibifu walioushuhudia hauelezeki.

Dkt. Richard Peeperkorn akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo amesema “Wafanyikazi wetu wanakosa maneno ya kuelezea hali mbaya zaidi inayowakabili wagonjwa na wahudumu wa afya waliobaki katika hospitali hizo.”

Zaidi ya watu 20,000 wameuawa hadi sasa ikiwa ni takribani asilimia 1 ya watu wote wa Gaza. Na shirika la msaada kwa wkimbizi wa Kipalestina UNRWA na la mpango wa chakula duniani WFP yameonya kuhusu njaa inayowakabili watu wa Gaza yakisema sasa masoko yote yakikaribia kusambaratika kabisa watu wanalazimika kula mlo mmoja au kulala njaa huku changamoto kubwa ikiwa ni ufikishaji wa misaada na watu wa kuisambaza.

Watoto Sudan mashariki na kati wanasubiri kupokea misaada ya kibinadamu kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Watoto Sudan mashariki na kati wanasubiri kupokea misaada ya kibinadamu kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Vita nchini Sudan

Takriban watu 300,000 wamefungasha virago na kukimbia katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan wa Wad Madani kwenye jimbo la Aj Jazirah kwa mujibu wa shirika la umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM kufuatia wimbi jipya la mapigano ambayo pia yametawanya maelfu ya watu ndani ya jimbo hilo. 

Karibu watu nusu milioni wanawake, wanaume na watoto walichukua hifazi jimboni  Aj Jazirah tangu kuanza kwa machafuko Sudan baina ya vikosi vya jeshi la serikali na wapiganaji wa vikosi vya msaada wa haraka SAF mwezi Aprili mwaka huu. Mkuu wa IOM Amy Pope ameonya kwamba “hili ni janga kubwa la kibinadamu na linadhihirisha haja ya haraka ya kusaka suluhu ya mzozo huo.”   

Uchaguzi Mkuu mwaka 2023 nchini DRC.
Radio Okapi
Uchaguzi Mkuu mwaka 2023 nchini DRC.

Uchaguzi Mkuu nchini DR Congo

Nimalizie nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambako jana watu wapatao milioni 44 walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na wawakilishi wa serikali za mitaa. Rais wa tume ya uchaguzi nchini humo CENI Denis Kadima amesema wale wote walioshindwa kupiga kura jana kwa sababu mbalimbali ikiwemo mvua leo wamepiga kura zao na matokeo ya awali yameanza kubandikwa katika baadhi ya vituo huku zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchi nzima.