Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO imetuepusha kutumbukia kwenye usambazaji wa habari za uongo na potofu- Wanufaika

Afisa Habari wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO ofisi ya Beni jimboni Kivu Kaskazini akipatia mafunzo wanahabari, wanaharakati na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuhusu habari potofu na habari za uongo mjini Beni.
UN./George Musubao
Afisa Habari wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO ofisi ya Beni jimboni Kivu Kaskazini akipatia mafunzo wanahabari, wanaharakati na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuhusu habari potofu na habari za uongo mjini Beni.

MONUSCO imetuepusha kutumbukia kwenye usambazaji wa habari za uongo na potofu- Wanufaika

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kesho nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni uchaguzi mkuu ikiwa ni tamati ya kampeni huku Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umeshiriki kwa kusafirisha sio tu vifaa vya uchaguzi lakini pia kuelimisha wananchi jinsi ya kukabili na kuzia habari potofu na za uongo kwani ni tisho la amani na usalama. 

Mwandishi wetu jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC, George Musubao amezungumza na wanufaika wa mafunzo hayo kuona ni vipi yamesaidia kuepusha zahma. Miongoni mwao ni Diane Kasomo mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha ISC mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini.

Diane Kasomo mwanafunzi, Chuo Kikuu ISC- Beni.
UN News/ George Musubao
Diane Kasomo mwanafunzi, Chuo Kikuu ISC- Beni.

Habari za uongo zilisababisha watoto kukimbia makwao

Bi. Kasomo anasema mjini Beni kuna habari nyingi potofu na za uongo ambazo zina sambazwa na watu wenye nia mbaya. Ametolea mfano miaka iliyopita ambapo walipatiwa taarifa za uongo kuwa waasi wa Allied for Democratic Forces au ADF walivamia mji huo.

“Wakati  watu walipata habari hiyo walianza kukimbia pasipo mwelekeo. Kulikuwa na mvua kubwa na watoto waliingia kwenye mvua na kuanza kukimbia na hata leo hatujapata taarifa za waliko hadi leo hii. Hii ilisababishwa na habari ya uongo zilizosambazwa na watu wenye nia mbayá.”

Mwanachuo huyo akafafanua zaidi hatari afahamuyo ya habari potofu na za uongo akisema ni hatari kubwa sana, “kwa sababu inasababisha mauaji, inatesa ewngi moyoni. Habari hizo husababisha msongo kwa watu, huweza kuleta chuki kati ya watu. Kama ni ndugu yangu aliyetoa habari ya uongo, kutakuwa na kuchukiana na ni hatari sana ndani ya jamaa. inatutesa sana".

Nimejifunza jinsi ya kubainisha uongo na kweli

Mafunzo yamemjenga Bi. Kasomo akisema kuwa MONUSCO ndio iliwapatia mafunzo ya kutambua habari za uongo na habari potofu.

"Jean Tobi Okala alitufundisha namna gani kugundua kama habari ni ya uongo ama kweli. Namna ya kwanza alituonesha kuchunguza nani aliweka saini habari ile, habari inatoka wapi na pia habari ilirushwa au ilitangazwa tarehe gani. Ukajua mambo haya matatu utaweza kufafanua kama ni habari ya uongo ama ni ya ukweli,” alisema Bi. Kasomo.

Waandishi wa habari nao wamenufaika na mafunzo

Germain Hassan ni mwandishi wa habari kwenye vityo vya MTV na Canal Afrika. Yeye ni mkazi pia wa mji wa Beni akazungumzia kampeni za uchaguzi na habari potofu na za uongo akisema wakati huu wa kampeni ya uchaguzi ni muda ambao mwanasiasa anakuja na habari mbalimbali. 

“Habari za uongo zimejaa katika mitandao za kijami na katika miji mengi. Mafunzo haya yamenisaidia kwa sababu tumefunzwa namna ya kutambua uongo pia na kama vile uongo umetambaa sana mtandaoni. Pia kuhusu fununu mbalimbali watu wanasambaza ili kuchafua watu wengine.”

Germain Hassan, Mwandishi wa habari nchini DRC.
UN News/ George Musubao
Germain Hassan, Mwandishi wa habari nchini DRC.

Kila mtu apambane na habari potofu 

"Mimi nitaweza kutoa ujumbe kwa wanaotusikia ya kwamba wanapopata habari wanabidi kuchunguza imetokea wapi na ni nani ambaye aliitoa au kuitangaza. Na pia kama zina manufaa gani kwa watu. Kwa sababu kuna habari ambazo zimesambaa kwenye mitandao na kuharibu picha ya wengine.  Inabidi kuchunguza kabla ya kusambaza,” amesema Bwana Hassan. Amesema ni vema kila mtu kupambana na habari potofu kwani zinaleta changamoto. “Tutaendelea kufundisha wengine ili waweze kuchunguza habari kabla ya kusambaza kwani tukisambaza habari ya uongo pasipo kuchunguza tutaunguza miji"

Wanaharakati nao walifikiwa na mafunzo ya kubaini habari za uongo na potofu

Esaie Liko ni mwanaharakati wa shirika la kiraia la LUCHA au Kupigania Mabadiliko. Yeye anasema "mafunzo yalikuwa na umuhimu sana kwetu kwani kwenye mitandao kulikuwa na watu wakialika wengine kwenda kuandama na kushikilia mambo yanayoleta chuki baina ya wakaazi. Yalisababisha changamoto ila wakati tunapochunguza tunagundua kwamba ni habari zilizosambazwa kwa lengo ya kuvunja uhusiano pia na kuleta changamoto ambayo ilizuia maendeleo tunayoihitaji sote.”

Amesema mafunzo yamesaidia pia wao wanarakati kwani wana kazi kubwa ya kuchunguza habari yote ili waweze kuongoza raia wenzetu. Kuna nyakati walipata habari na kujikuta kwenye changamoto kubwa, “tunapopata habari ya kuhusu usalama wa nchi ama ya mji wa Beni tunakuta wale ambao wamesambaza ni watu wenye malengo mengine mabaya tofauti na sisi.”

Sitatumbukia kwenye mtego wa kusambaza habari potofu na za uongo

Ametoa mfano kuna wakati askari wa jeshi la serikali wanapita na vifaa kwenda kuimarisha amani na mtu anasambaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni waasi wameingia. “Na wakati tunapopata habari hii tulikuwa tukisambaza pia mitandaoni kuwazia kuaw tumewaarifa viongozi ila ilikuwa kuogopesha raia zaidi.”

“Baada ya mafunzo tumefahamu kwamba inabidi kuchunguza chanzo cha habari ambayo mtu  ameandika, kujua kama ni yeye anayestahili kuzungumuzia lile jambo na pia kama aliongea na wanaohusika. Tumefunzwa kujua haya yote. Mimi binasfi imenisaidia sana. Nadhani sitatumbukia tena kwenye mtego wa kusambaza habari potofu ama za uongo" 

Habari hii imeandaliwa na GEORGE MUSUBAO, UNNEWS