Watumiao madaraka yao kusambaza taarifa za uongo wawajibishwe- Bachelet

28 Juni 2022

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Michelle Bachelet ametoa wito kwa serikali kuzingatia wajibu wao wa kimataifa wa kusongesha na kulinda haki za wananchi kupata taarifa na kujieleza.

Bachelet amesema hayo leo akihutubia mkutano wa 50 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ambao leo ulijikita katika suala la taarifa za uongo na hatua sahihi za kuchukua kukabiliana na tatizo hilo.

Taarifa za uongo ni zipi

Taarifa za uongo ni zile ambazo mtu au watu wanasambaza wakijua ni za uongo na hazina ukweli wowote tofauti na taarifa potofu ambazo zimepindishwa kwa malengo ya wasambazaji.

Bi. Bachelet amesema “matatizo ya jamii zetu hayaanzi na taarifa za uongo, bali huchochewa na taarifa za uongo. Dalili zake ni kuenea kwa magonjwa yanayokabili dunia hivi sasa, mojawapo ni ukosefu wa usawa uliojikita kimfumo, ubaguzi, taasisi zilizo dhaifu, umma kupoteza imani kwenye mifumo ya utawala na ukosefu wa utawala wa sheria.”

Jamaa za watu waliotoweshwa wakiwa kwenye maandamano ya kimya kimya kwenye makao makuu ya UN huko Pristina, Kosovo mwaka 2002. (Picha Maktaba)
UN
Jamaa za watu waliotoweshwa wakiwa kwenye maandamano ya kimya kimya kwenye makao makuu ya UN huko Pristina, Kosovo mwaka 2002. (Picha Maktaba)

Ni kwa nini taarifa za uongo husambaa

Amesema taarifa za uongo zinasambaa pindi watu wanapoona sauti zao hazisikilizwi, halikadhalika kutokuwa na imani na mifumo ya kisiasa, hali ya uchumi kuwa mbaya sambamba na hali ya kijamii.

“Zinashamiri pindi mashirika ya kiraia, waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na wanasayansi hawawezi kufanya kazi zao, hawawezi kukusanyika na kuzungumza kwa  uhuru, uhuru wa kiraia umebinywa au kufungwa kabisa. Haki ya kupata taarifa, kuzungumza na kukusanyika zimetishiwa,” amesema Bi. Bachelet.

Nathan Peiffer-Smadja daktari wa magonjwa ya kuambukiza katika hospitali ya Bichal huko Paris, Ufaransa amembambana dhidi ya taarifa za uongo kuhusu COVID-19 kwa kusambaza taarifa za  ukweli na za uhakika
Nathan Peiffer-Smadja
Nathan Peiffer-Smadja daktari wa magonjwa ya kuambukiza katika hospitali ya Bichal huko Paris, Ufaransa amembambana dhidi ya taarifa za uongo kuhusu COVID-19 kwa kusambaza taarifa za ukweli na za uhakika

Hatua za kuchukua

Hata hivyo amesema “katika kukabili changamoto hizo hatupaswi hatupaswi kutumbukia kwenye mtego wa kujaribu kuamrisha kipi ni uongo na kipi ni sahihi kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kuziba kabisa fursa ya kidemokrasia.

Kwa mantiki hiyo ametaka serikali kujikita katika kutathmini ni kwa vipi mifumo ya mawasiliano inabadilishwa na teknolijia na kuangalia ni kwa jinsi gani zinaweza kudhibiti changamoto zinazosababishwa na habari za uongo na wakati huo huo kushughulkia visababishi vya kukua kwa taarifa za uongo.

Bi. Bachelet amesema hatua za kisera kusaidia uandishi huru wa habari na kuimarisha uwepo wa vyombo vingi vya habari ni muhimu katika kusaidia mtu au watu kujipambanua katika mifumo ya sasa ya habari.

“Kuimarika kwa mifumo ya elimu ya kumwezesha mtu kufanya tafakuri ya kina ni muhimu sana na itasaidia katika mazingira  ya sasa,” amesema Bachelet.

“Wale walio madarakani ambao wanaamua kusambaza taarifa za uongo ili kukandamiza taarifa ambazo hawapenzi kuzisikia au kuonea na kunyanyasa kauli zinazowakosoa, ni lazima wawajibishwe,” amesema Bachelet.

Amekumbusha kuwa kushughulikia changamoto ya taarifa za uongo si wajibu wa serikali pekee, bali pia majukwaa ya mitandao ya kijamii akisema, “nayo yamebadili jinsi taarifa zinasambaa kwenye jamii hivyo nayo yana jukumu hapa. Lazima yatambua ni jinsi gani yanabadili ajenda ya kitaifa na kimataifa,” amesema Bachelet.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter