Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Natumai uchaguzi utakuwa wa amani – Guterres kwa DRC

Mji mkuu wa DRC, Kinshasa.
MONUSCO/Myriam Asmani
Mji mkuu wa DRC, Kinshasa.

Natumai uchaguzi utakuwa wa amani – Guterres kwa DRC

Haki za binadamu

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakiingia kwenye uchaguzi mkuu wa rais, magavana na wabunge na madiwani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ni matumaini yake uchaguzi huo utafanyika kwa amani, kwa uwazi na ujumuishi.

Stéphane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu, amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwamba uzingatiaji wa mambo hayo utaimarisha taasisi za demokrasia za taifa hilo na hivyo kuiweka nchi hiyo kwenye mwelekeo wa ustawi wa kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa mamlaka nchini humo, viongozi wa kisiasa, mashirika ya kiraia na Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, kuhakikisha wapiga kura wote wanaweza kufikia vituo vya kupigia kura na kupiga kura kwa uhuru, bila hofu ya kutishiwa au kukandamizwa kisiasa.

Epukeni ghasia na uchochezi

Katibu Mkuu amelaani matukio ya ghasia yaliyoripotiwa wakati wa kampeni za uchaguzi na kusihi wanasiasa na wafuasi wao kujizuia kufanya vitendo vyovyote vile vinavyoweza kuchochea ghasia au kuibua kauli za chuki miongoni mwa jamii au makundi,halikadhalika mashambulizi dhidi ya wagombea wanawake.

Kwa mujibu wa Dujarric, Katibu Mkuu “amesihi vyama vyote vya siasa viwe makini katika matumizi ya maneno na vitendo vyao,”

Guterres amesisitiza msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuendelea kusaidia DRC kupitia Mwakilishi wake Maalum nchini DRC. Mwakilishi huyo ndiye pia Mkuu wa MONUSCO ambao ni Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo.

Kuhusu uchaguzi

Takribani raia milioni 40 wa DRC watapiga kura kumchangua rais miongoni mwa wagombea 20 akiwemo Rais wa sasa Félix Tshisekedi anayesaka awamu ya pili na ya mwisho ya miaka 5 ya uongozi.

Kwa mujibu wa CENI, mgombea yeyote atayepata kura nyingi ndiye atakuwa mshindi.

Kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi, matokeo yanatarajiwa kutangazwa tarehe 31 mwezi Desemba.

Uchaguzi wa mwisho ulifanyika Desemba 2018 nchini DRC kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila ambapo Rais Tshisekedi alishindwa kwa asilimia 38.6 ya kura zote zilizopigwa.