Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: UN yalaani vikali mauaji ya wahudumu 7 wa misaada ya kibinadamu

Msaada wa chakula unaotolewa na World Central Kitchen ukipangwa kwenye boti inayoondoka Italia. (Maktaba)
© Open Arms
Msaada wa chakula unaotolewa na World Central Kitchen ukipangwa kwenye boti inayoondoka Italia. (Maktaba)

Gaza: UN yalaani vikali mauaji ya wahudumu 7 wa misaada ya kibinadamu

Amani na Usalama

Leo maafisa wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mauaji ya wafanyakazi wa misaada 7 wa shirika lisilo la kiselikali au NGO la World Central Kitchen yaliyofanywa na jeshi la Israel, maafisa hao wakirejea kueleza hofu yao kwamba hakuna mahali palipo salia kuwa salama Gaza. Akizungumzia mauaji hayo Jamie McGoldrick, Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika eneo linalokaliwa la Palestina amesema “Hili sio tukio la kipekee kwani hadi kufikia Machi 20 wahudumu wa kibinadamu 196 wameuawa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana na hii ikiwa ni karibu mara tatu zaidi ya idadi ya vifo iliyorekodiwa katika mgogoro mmoja kwa mwaka." 

Bwana McGoldrick amerejea wito wake kwa pande zote katika mzozo ikiwemo serikali ya Israel kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu ambazo zinazuia kulenga wahudumu wa misaada ya kibinadamu.

Amesisitiza kuwa “Jukumu la wahudumu wa misaada ni kupunguza madhila kwa watu Kwenye migogoro, hivyo usalama wao na wa wale raia wanaowahudumia ni lazima uhakikishwe.”

Meli ya shirika la Open Arms ikiwa imesheheni chakula na maji na wafanyakazi waliojitolea tayari kusaidia walio hatarini zaidi huko Gaza. (Maktaba)
© Open Arms
Meli ya shirika la Open Arms ikiwa imesheheni chakula na maji na wafanyakazi waliojitolea tayari kusaidia walio hatarini zaidi huko Gaza. (Maktaba)

Shambulio la Israel

Maoni ya afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa yamekuja baada ya World Central Kitchen kuripoti kwamba shambulizi la anga la Israel limehusika na vifo vya wafanyakazi wake wa kutoa misaada huko Deir al-Balah. 

Kufuatia ripoti hizo na picha za gari hilo lisilo la kiserikali zikionyesha shimo kubwa kwenye paa lake, Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ameeleza kughadhabishwa kwake na shambulio hilo na kusema waliouawa ni "mashujaa, wamekufa wakati wakijaribu kulisha watu wenye njaa".

Kutoka kwa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, msemaji wake Dkt. Margaret Harris amesema ujumbe wa shirika hilo lisilo la kiserikali ulikubaliwa na Israel mapema na kwamba gari la shirika hilo "lilikuwa na alama nzuri, iliyokuwa bayana isemayo World Central Kitchen.”

Akigeukia uharibifu wa Hospitali ya Al-Shifa kufuatia kuzingirwa kwa wiki mbili na jeshi la Israeli, Dkt Harris amesema "Yameondoa kiini cha huduma za afya katika eneo hilo.”

Katika tathmini ya kina ya kufungwa kwa hospitali ya Al-Shifa yenye vitanda 750 katika mji wa Gaza, WHO imesema kuwa timu za misaada zimekuwa zikingoja siku kwa siku ili kupata idhini ya Israeli kufika kwenye kituo kilichoathiriwa. wafanyakazi na wagonjwa wamevumilia viwango vya kutisha vya vurugu.

"Tumewasiliana na wafanyikazi, wakurugenzi wa hospital na wametuambia kuwa Al-Shifa haiwezi tena kufanya kazi kwa njia yoyote, sura au umbo limesambaratika kabisa kama kituo cha matibabu” amesema msemaji huyo wa WHO Dkt. Margaret Harris.

Picha za uharibifu wa hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, kufuatia kumalizika kwa mashambulizi wa hivi karibuni ya Israel. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikariri kuwa hospitali lazima ziheshimiwe na kulindwa; lazima zisitumike kama uwanja wa vita.
UN News
Picha za uharibifu wa hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, kufuatia kumalizika kwa mashambulizi wa hivi karibuni ya Israel. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikariri kuwa hospitali lazima ziheshimiwe na kulindwa; lazima zisitumike kama uwanja wa vita.

Hospitali imesalia kifusi tu

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo Dkt. Harris amesema “Kituo hicho hivi sasa kimesambaratika kabisa na takribani wagonjwa 21 wameuawa wakati wa kuzingirwa na jeshi la Israel kituoni hapo.

Ameongeza kuwa “wakati hali ikiendelea kuzorota katika Hospitali ya Al-Shifa wahudumu wa afya walilazimika kuhamishia wagionjwa katika ofisi Kwenye maeneo ya hospitali hiyo ambako hakuna vyoo , maji wala chakula , na walikuwa wanagawana chupa moja ya maji watu 15.”

Amebainisha kuwa wafanyikazi wa matibabu "hawakuwa na njia za kuwatunza wagonjwa, ambao wengi wao walikuwa wamejeruhiwa vibaya au wagonjwa wa kiwango cha uangalizi mkubwa waliowekewa mipira ya  mkojo lakini hawakuwa na mifuko ya mkojo. Unaweza kufikiria hofu ambayo imekuwa ikiendelea," Amesema Dkt. Harris.

Ikiwa ruhusa itatolewa Jumanne kufikia vituo vichache vya mwisho vya afya vilivyosalia vya Al-Shifa na kaskazini mwa Gaza, vipaumbele vya timu za WHO amesema ni pamoja na kuleta dawa, mafuta na chakula na kutathmini ni vifaa gani vingine vinahitajika na jinsi ya kutoa misaada kwa waliojeruhiwa vibaya zaidi na wagonjwa.

Katika makazi ya muda kote Gaza, UNRWA inatoa huduma muhimu za afya.
© UNRWA
Katika makazi ya muda kote Gaza, UNRWA inatoa huduma muhimu za afya.

Ruhusa zinakataliwa 

"Tumekuwa tukijaribu kwenda siku kwa siku na operesheni zetu nyingi zimekataliwa," amesema Dkt. Harris na kuongeza kuwa "Hatutaweza kutoa vitu ambavyo, hospitali inayofanya kazi inahitaji, lakini kwanza kabisa tunahitaji kufanya tathmini ili kuelewa kile tunachoweza kufanya. Pili nani anahitaji kuhamishwa na wanaweza kwenda wapi na tunaweza kufanya nini kuokoa maisha ya wagonjwa hao waliosalia.”

Hadi sasa, mamia ya wafanyakazi wa huduma za afya wameuawa wakati wakifanya kazi yao, pamoja na raia 32,000, na asilimia 70 kati yao ni wanawake na watoto, huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel baada ya mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas dhidi ya Israel hapo tarehe 7 Oktoba mwaka jana ambayo ilisababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya 350 kuchukuliwa mateka.

"Tunajitahidi kuelewa idadi ya vifo zaidi ya idadi inayoripotiwa ya watu waliouawa katika shambulio la bomu kwa sababu watu wengi hawafiki hospitalini," amesema msemaji huyo wa WHO.