Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MAHOJIANO:Kuanzia Gaza hadi Ukraine, uwajibikaji ni muhimu kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu: Türk

Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na UN News
UN Photo/Mark Garten
Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na UN News

MAHOJIANO:Kuanzia Gaza hadi Ukraine, uwajibikaji ni muhimu kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu: Türk

Haki za binadamu

Wakati vita ikiendelea kupamba moto huko Gaza na idadi ya vifo vya wanawake na watoto ikiongezeka kila saa, kuhakikisha uwajibikaji wa uhalifu huo ni muhimu sana ili kuzuia ongezeko la manung'uniko amesema hii leo afisa mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa 

Tweet URL

Katika mahojiano maalum na UN News Volker Türk, ambaye ni Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, amesisitiza kwamba uwajibikaji ni muhimu na ni "kiungo kinachokosekana katika migogoro mingi duniani kote ambayo inaendeleza tu mzunguko wa vurugu. Ni muhimu sana kwamba uwajibikaji uwe ni sehemu ya mpango wowote wa siku zijazo kwa sababu tunajua kwamba ikiwa hali ya kutowajibishwa ikitawala, na ikiwa ukweli hautasemwa na tutakuwa na malalamiko ya mara kwa mara," amesema akimaanisha mzunguko wa hivi karibuni wa umwagaji damu wa mzozo baina ya Israel na Palestina.

Mahojiano hayo pia yameenda mbali zaidi ya Mashariki ya Kati, yakiangazia vita inavyoendelea nchini Ukraine, ambapo raia pia wanabeba mzigo mkubwa wa uvamizi wa Urusi.

Amebainisha kuwa kuwafikisha wahalifu mahakamani inaweza kuwa kazi ya polepole, Bwana Türk amemulika uwezo wa mifumo ya uwajibikaji, akilinganisha na maeneo ya kihistoria kama vile Majaribio ya Nuremberg au suluhu ya baada ya vita kufuatia vita katika Yugoslavia ya zamani katikati ya miaka ya 1990, akisema, "Ikiwa mara moja umefanya uhalifu wa aina hii, huwezi kuwa na uhakika kwamba katika wakati fulani huwezi kukamatwa.”

Katika mahojiano hayo, mkuu huyo wa haki za Umoja wa Mataifa pia alizungumzia hatari ya kuongezeka kwa kauli za chuki na kurudisha nyuma haki za wanawake, pamoja na kampeni ya mwaka mzima ya Umoja wa Mataifa ya kuendeleza maendeleo ya haki sawa kupitia maadhimisho ya miaka 75 ya tamko la kimataifa la Haki za Binadamu. .

Hii ni sehemu ya mahojiano hayo kwa ufafanuzi.

Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu za Umoja wa Mataifa akizungumza na UN News katika mahojiano maalum
UN Photo/Mark Garten
Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu za Umoja wa Mataifa akizungumza na UN News katika mahojiano maalum

UN News: Sasa ni zaidi ya miezi miwili katika ongezeko la hivi karibuni la mzozo kati ya Israel na Palestina, kufuatia shambulio la kutisha la Hamas tarehe 7 Oktoba na jibu la Israel. Tumeshuhudia wiki baada ya wiki ya mashambulizi ya kutisha. Zaidi ya Wapalestina 18,000 wamekufa, na idadi kubwa ikiwa ni watoto.

Umeelezea wasiwasi mkubwa sana kuhusu ukiukaji mwingi na wa kutisha wa sheria za kimataifa na umetaka uchunguzi ufanyike. Unaonya kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria. Je, kweli kuna lolote linaweza kufanywa ili kutekeleza sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na kuhakikisha kwamba sheria ya kibinadamu inatumika kwa nchi wanachama wote?

Volker Türk: Awali ya yote, ni janga lisiloweza kudhibitiwa, kile kinachotokea katika Ukanda wa Gaza, katika Ukingo wa Magharibi, lakini pia katika Israeli, kwa sababu mwisho wa siku huathiri jumuiya zote.

Bila shaka, yanayotokea Gaza ni makubwa zaidi. Nimekasirishwa pia kwamba wenzetu wengi wameuawa 135 kutoka UNRWA, mmoja kutoka WHO. Kwamba mfumo wetu wa kibinadamu hauheshimiwi na hatuwezi kutoa kile ambacho kwa kawaida tunaweza kufanya katika hali ya vita, na kwamba haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu zinakiukwa kila siku kwa namna kubwa zaidi.

Tunajua kwamba ikiwa hali ya kukwepa sheria itatawala, na ikiwa ukweli hautasemwa, tutakuwa na manung'uniko ya kila wakati.

Ni muhimu sana kwamba uwajibikaji iwe ni sehemu ya mpangilio wowote wa siku zijazo kwa sababu tunajua kwamba ikiwa hali ya kutowajibishwa itatawala, na ikiwa ukweli hautasemwa tutakuwa na manung'uniko ya kuendelea na kuendelea. Natumai kwamba kwa kazi tunayofanya kutoka upande wa haki za binadamu, lakini pia kile Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai inachofanya, na mifumo tofauti inafanywa, hii itatusaidia kushinda baadhi ya masuala ya uwajibikaji ambayo tunakabiliana nayo. katika hali hii.

UN News: Kwa hivyo, unafikiria hatua gani zinazofuata na nini unachosema kwa wale ambao wanaashiria dalili zinazowezekana za mauaji ya kimbari?

Volker Türk: Tutaendelea kuweka kumbukumbu, kuripoti na kufuatilia hali hiyo. Nina wasiwasi sana kuhusu hatari ya uhalifu wa kikatili. Nina wasiwasi sana kuhusu hali ya Ukingo wa Magharibi, haswa, kwa sababu kile tunachokiona tangu tarehe 7 Oktoba, zaidi ya Wapalestina 271 wameuawa, wakiwemo watoto 69. Nina wasiwasi kuhusu hii inamaanisha nini katika siku zijazo.

Pia nimeshtushwa sana na lugha ya udhalilishaji ambayo nimeona kutoka kwa Hamas lakini pia kutoka kwa wanajeshi na viongozi wa kisiasa wa Israeli. Baadhi yao wametoa maoni ambayo hayakubaliki kabisa ambayo yanatutia wasiwasi sana.

Mashambulio ya makombora yamesababisha uharibifu mkubwa huko Gaza.
WHO
Mashambulio ya makombora yamesababisha uharibifu mkubwa huko Gaza.

UN News: Tukiugeukia Ukraine. Umeshutumu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya Urusi mara kwa mara na hawapati athari hata ndogo au hakuna kabisa, na kuna mifumo kadhaa ya haki za binadamu ambayo inafuatilia ukiukaji na kuchapisha ripoti mara kwa mara. Je, unaweza kuangazia vita hiyo nyingine ya kutisha, ambavyo imekuwa ikiendelea kwa karibu miaka miwili sasa.

Volker Türk: Kwa hivyo, mara tu nitakaporejea Geneva wiki ijayo, ninahutubia Baraza la Haki za Kibinadamu na kuwapa taarifa kuhusu hali ya Ukraine. Kama unavyojua, wakati wa majira ya baridi, hali ni mbaya zaidi kwa sababu baadhi ya jamii, hasa zilizo karibu na mstari wa mbele hazijaweza kupata umeme tena.

Tuna mauaji yanayoendelea, tuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, haswa mateso, ambayo hufanyika wakati wowote vikosi vya Urusi vinapoweza kuchukua eneo. Na ndio, tunahitaji tu kuhakikisha kuwa uwajibikaji utatekelezwa tena.

Tuna njia kadhaa zinazofanana na zile tunazoziona Mashariki ya Kati, mifumo ya uwajibikaji ambayo inatumika na ninatumai kwamba hakika haki itatumikia, kwa maslahi ya waathirika wote.

UN News: Jambo kuu ni uwajibikaji kila wakati?

Jambo kuu ni uwajibikaji kwa sababu imekuwa kiungo kinachokosekana katika hali nyingi za migogoro duniani kote: Volker Türk

Volker Türk: Muhimu ni uwajibikaji kwa sababu imekuwa kiungo kinachokosekana katika hali nyingi za migogoro duniani kote. Na usiposhughulikia uwajibikaji, utaishia tena kwenye vita na migogoro.

UN News: Kwa hivyo, unaweza kusema kwamba kuna matumaini ya kuhakikisha mchakato unaofaa katika vita kama Ukraine?

Volker Türk: Kwanza kabisa, swali ni wakati gani hilo linaweza kufanywa. Lakini tumeona katika hali nyingine nyingi, ukiangalia tu Bosnia na vita katika Yugoslavia ya zamani, lakini pia Rwanda na hali nyingine, kwa kweli unaona watu wamekamatwa.

Hata leo, bado tunayo mamlaka ya kitaifa, mamlaka ya ulimwengu ambayo inatumika. Na mara tu unapofanya uhalifu wa aina hii, huwezi kuwa na uhakika kwamba katika hatua fulani huwezi kukamatwa.

Ninaamini katika utaratibu huu wa uwajibikaji. Hatukuwa nayo miaka 75 iliyopita. Tulikuwa nayo baada ya vita ya pili ya dunia. Na mfumo huo ulioanzishwa kwa majaribio ya Nuremberg umetusaidia sana kujenga mfumo wa uwajibikaji.

Najua sio haraka vya kutosha. Najua tunapaswa kuwa nayo kila mahali na kwa nguvu sawa, lakini ni mwanzo wa kitu ambacho ni muhimu sana.

UN News: Na je ni mchakato ambao unatarajia kuuunda baada ya muda kama kizuizi?

Volker Türk: Nadhani tumeona kuwa ni kizuizi. Tunahitaji kufanya gharama ya kutoufuata iwe juu zaidi. Na ndio maana unahitaji uwajibikaji. Ni sehemu ya kuzuia pia.

Mvulana akiwa amesimama kwenye mabaki ya shule yao huko Novohryhorivka, Ukraine.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Mvulana akiwa amesimama kwenye mabaki ya shule yao huko Novohryhorivka, Ukraine.

UN News: Wewe ni Kamishna Mkuu katika mwaka wa kumbukumbu ya miaka 75 ya Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu. Na umetafakari kwa kirefu hali ya dunia na kile ambacho wanadamu hufanyiana na kwa sayari. Na umetaka hali ibadilike haraka. Unasemaje kwa wale ambao wamepoteza imani na haki za binadamu na wanasema kwamba zinahusu baadhi tu na sio wengine, au kwamba ni polepole utekelezaji wake?

Volker Türk: Ndiyo, ndani ya Umoja wa Mataifa, tulizaliwa kutokana na matukio ya janga. Vita viwili vya Dunia, Holocaust, tishio la nyuklia, watu wengi kufurushwa makwao na Ulaya pekee, kulikuwa na watu milioni 60 waliokimbia makazi yao. Tunapozungumza juu ya takwimu leo, unaweza kuona ilivyokuwa wakati huo.

Kati ya hayo kulitoka Mkataba wa Umoja wa Mataifa na tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu.

Na ilifanyika dhidi ya hali ya nyuma ya kipindi cha kutisha katika historia ya wanadamu, na ilifanyika kwa usahihi na hisia kwamba hayo hayatowahi kutokea  tena.

Na hilo ndilo lililozaa Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu. Tumeona zaidi ya miaka 75 iliyopita, hatuzungumzi vya kutosha kuhusu mafanikio. Tumeona mafanikio makubwa katika masuala ya haki za binadamu. Ukiitazama kwa mtazamo wa kihistoria.

Bila shaka, kuna kushindwa pia, lakini kushindwa sio mfumo wa haki za binadamu wenyewe, ni kushindwa kwa utekelezaji. Na hiyo inaturudisha kwenye kile ambacho nchi wanachama na wajibu wao, lakini pia biashara zinazoongezeka, sekta binafsi na watendaji wasio wa serikali, kwa ujumla . Na hapo ndipo tunahitaji pia kutilia mkazo.

UN News: Unanuia vipi haki za binadamu kuchukuliwa kwa uzito zaidi? Na unaweza kutoa baadhi ya mifano ya jinsi inavyofanya kazi au suluhisho za mbinu bora mashinani?

Volker Türk: Nimetoka Geneva. Tulikuwa na hafla ya siku mbili ya ngazi ya juu kuadhimisha miaka 75 ya Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu. Na ni muujiza mdogo kwamba dhidi ya hali ya mgawanyiko na mivutano ya kijiografia, tulikuwa na zaidi ya nchi 155 zinazotoa ahadi madhubuti ambazo zitakuja kuleta mabadiliko.

Kwa mfano, nchi tano ziliahidi kwamba zitaondoa hukumu ya kifo. Nchi 54 zilikuwa na mapendekezo madhubuti ya jinsi ya kuboresha usawa wa kijinsia, juu ya ulinzi wa wanawake. Nchi kumi na nne au zaidi ambazo zitaanzisha taasisi za kitaifa za haki za binadamu.

Tuna nchi ambazo zitapitisha sheria ya kuwalinda watu wenye ulemavu. Tuna nchi kadhaa ambazo zilizungumzia kuhusu kufanya juhudi zaidi juu ya masuala ya uwajibikaji na masuala ya haki ya mpito.

Kwa hiyo, hiyo inanipa matumaini. Pamoja na habari mbaya zote tulizo nazo, tunaona maendeleo.

Tumekuwa kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita na nchi saba ambazo zimehalalisha sha uhusiano wa jinsia moja, kwa mfano. Tulikuwa na mbili ambazo kwa bahati mbaya zilienda kinyume, lakini tulikuwa na saba ambazo zilihalalisha.

Kuna maendeleo. Hatupaswi kamwe kukata tamaa na tunapaswa kudumu na kazi yetu.

Mwanamke amesimama kwenye vifusi vya nyumba yake iliyoharibiwa katika Mkoa wa Herat, Afghanistan.
© UNICEF/Osman Khayyam
Mwanamke amesimama kwenye vifusi vya nyumba yake iliyoharibiwa katika Mkoa wa Herat, Afghanistan.

UN News: Umetaja haki za jinsia na wanawake tunaona, kutoka kwa Taliban hadi kurudi nyuma kwa haki za uzazi katika baadhi ya mataifa yanayoitwa yaliyoendelea. Je, unatafsiri vipi kubinywa kwa haki za wanawake duniani kote hivi sasa?

Volker Türk: Tumeona msukumo unaotia wasiwasi sana kuhusu jinsia, haki za kijinsia na haki za wanawake kwa ujumla. Lakini pia tusisahau tulipotoka, na ni muhimu kuzingatia hili.

Kinachonishtua leo ni kwamba mambo ambayo ningedhani hayangekuwa suala tena, haki za afya ya ngono na uzazi, kwa mfano au zaidi, au masuala ya msingi tu ya usawa ambayo sasa yasingekuwa suala la mjadala.

Na ninatumahi kuwa ni upotovu kwamba hiyo itatoweka haraka. Na ndiyo maana tunahitaji kulipigania, kwa sababu hatuwezi kamwe kuchukulia jambo lolote kuwa la kawaida hilo ni mojawapo ya mafunzo tuliyojifunza kutokana na haki za binadamu.

Nadhani kila kizazi kinapaswa kukimiliki, kujitolea tena, na kutafuta njia ya kusukuma nyuma dhidi ya washawishi ambao mara nyingi wana mitazamo ya chuki dhidi ya wanawake, mitazamo ya kijinsia na mitazamo ya mfumo dume ambayo kwa kweli haifai kuwa na nafasi katika karne ya 21.

UN News: Na serikali nzima pia?

Volker Türk: Na, haswa, ukiangalia Afghanistan, ambako kimsingi kuna mamlaka ya ukweli ambayo inawatesa wanawake na wasichana kwa sababu ya wao ni nani. Ninamaanisha, hiyo haijasikika sana katika karne ya 21.

Mateso ya kimfumo ya wanawake na wasichana kwa sababu ya wao ni nani ... hilo halijasikika sana katika karne ya 21.

Na kwa kweli tunahitaji kutafuta njia na suluhu za kukomesha hii. Lakini sio tu huko. Pia tuna masuala mazito sana Yemen. Tunayo katika wengi, kwa mfano, Papua New Guinea, Iran na maeneo mengine machache ambapo kwa hakika kuna ubaguzi wa kimfumo dhidi ya wanawake.

UN News: Kuna wingi wa chaguzi za ngazi ya nchi zilizopangwa kote ulimwenguni mwaka ujao, na tunaona mmomonyoko mkubwa wa kanuni za demokrasia na uvumilivu, ubaguzi. Na wakati huo huo, tunashuhudia pia kuongezeka kwa kampeni za upotoshaji zilizopangwa vyema na kukandamiza maandamano ya amani. Je, unaweza kutuambia ofisi yako inafanya nini kuunga mkono chaguzi huru, za haki na za uwazi?

Volker Türk: Ni jambo la kuhuzunisha sana kwetu kuona hilo huku chaguzi 70 zikifanyika, na watu bilioni 4 wakichagua uongozi wao mpya. Na wakati huo huo, majukwaa ya mitandao ya kijamii ambayo mara nyingi huendeleza taarifa potofu zenye madhara, hata kuchochea vurugu na chuki.

Na kwetu sisi, kwa hiyo, ni kwa ajili ya Umoja wa Mataifa kwa ujumla si kwa Ofisi yangu tu, kwetu sisi katika Umoja wa Mataifa, ni muhimu sana kutambua ishara za tahadhari za mapema na kuzifanyia kazi na kuzikabili, ili tuwe ndani. kuwasiliana na makampuni ya kiteknolojia ambayo yanaendesha majukwaa ya mitandao ya kijamii ili yafanye udhibiti wa maudhui, kwa mfano, na kwamba tunapinga kupitia kampeni kuhusu athari mbaya ambayo kauzli za chuki zinazo  au habari potovu, kwenye michakato ya uchaguzi.

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Volker Türk  akizungumza na waandishi wa habari (kutoka Maktaba)
© OHCHR
Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Volker Türk akizungumza na waandishi wa habari (kutoka Maktaba)

UN News: Umetaja kauli za chuki. Unasema nini? Tunaona mgawanyiko ulioongezeka, tunaona migogoro, tunaona kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu. Unasemaje, kwa mfano, kwa wale ambao kabla ya mzozo tunaouona wa Israeli na Palestina wanahisi chuki ikipanda ndani yao?

Volker Türk: Chuki ni mojawapo ya hisia ambazo ni mbaya sana na kwa bahati mbaya, inauzwa vizuri. Na wakati mwingine kuna masilahi ya biashara ambayo huchochea chuki. Na tunahitaji kupunguza hiyo, tunahitaji kuitisha. Tunahitaji kuonyesha mifano hii ya biashara.

Na pia tunahitaji kutafuta njia na suluhu tena kurudisha ubinadamu kwenye msingi wake na misingi yake. Na ninatamani jumbe za amani, za uponyaji, za kubadilisha chuki kuwa vitendo vyema zipate mvuto zaidi, katika vyombo vya habari, lakini pia katika mijadala.

Hatujadili amani tena, ambayo inashangaza au kuhusu haki za binadamu kama chombo cha kuleta mabadiliko kwa ulimwengu bora. Natamani tungekuwa na zaidi ya hii.

UN News: Umetaja maadhimisho ya miaka 75 ya tamko la Ulimwengu mara kadhaa. Tunakaribia mwisho wa kazi ya mwaka mmoja, tukiwa na wiki mbili za matukio mengi ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka huu. Unajisikiaje kutoka nje? Ni nini kimetoka kwenye matukio haya?

Volker Türk: Kama nilivyotaja hapo awali tuna ahadi hizi kubwa. Ninahisi, wakati mwingine ni vigumu kuwasiliana kuihusu kwa sababu tuko katika wakati mgumu, wa huzuni katika historia yetu.

Vijana ... wanajua maana ya kuzungumza na kuhisi haki za binadamu, na hiyo inanipa matumaini mengi

Lakini kuna msingi wa kuunga mkono haki za binadamu. Ninaiona miongoni mwa nchi wanachama. Ninaiona katika sekta binafsi na zaidi ya yote, miongoni mwa vijana. Kwa vijana, tunajua kutokana na kura za maoni tofauti kwamba mabadiliko ya tabianchi na masuala ya haki za binadamu ni ajenda kuu ya ajenda zao.

Tulikuwa na kikundi cha ushauri wa vijana, tulikuwa na mamia ya maelfu ya vijana pia kushiriki katika matukio tofauti kwa sababu ya Tamko la Haki za binadamu. Na ninaweza kukuambia  wanajua maana ya kuzungumza na kuhisi haki za binadamu. Na hiyo inanipa matumaini mengi. Ninaona nguvu hii nzuri ambayo inaweza kutusaidia, unajua, kuweka haki za binadamu katika msingi wa kile tunachohusu.

UN News:  Kwa hivyo, licha ya hali ya sasa ya mambo ya ulimwengu, unahisi kuwa na matumaini kutokana na hili?

Volker Türk: Ninamaanisha, hatuwezi kamwe kukata tamaa na hatuwezi kamwe kuacha kazi yetu, na nadhani ndani ya misiba ya leo, tunaweza pia kuona ni mambo gani ambayo yanatuondoa katika hili, mbali na mteremko huu na tuwe na matumaini kwa siku zijazo zenye amani zaidi na kukumbatia nyingine.