Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Urusi na China zatumia turufu kuzuia rasimu ya Marekani Barazani

Urusi imepiga kura turufu dhidi ya rasimu iliyowasilishwa na Marekani kusaka suluhu ya kiutu huko Gaza, Mashariki ya Kati
UN /Manuel Elias
Wajumbe wa Baraza wakipigia kura rasimu ya azimio wakati wa mkutano kuhusu hali Mashariki ya Kati ikiwemo Hoja ya Palestina
Urusi imepiga kura turufu dhidi ya rasimu iliyowasilishwa na Marekani kusaka suluhu ya kiutu huko Gaza, Mashariki ya Kati

Gaza: Urusi na China zatumia turufu kuzuia rasimu ya Marekani Barazani

Amani na Usalama

Kwa mara ya tatu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kupitisha maazimio kuhusu mapigano yanayoendelea huko Gaza, Mashariki ya Kati, halikadhalika janga la kibinadamu, vyote vikisababishwa na mapigano kati ya Israeli na wapiganaji wa kipalestina, Hamas.

Tweet URL

Rasimu mbili za azimio ziliwasilishwa mbele ya Baraza leo alasiri. Moja iliwasilishwa na Urusi na washirika wake, ilihali nyingine iliwasilishwa na Marekani.  

Katika upigaji kura wa rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Marekani namba S/2023/792   wajumbe 10 walipiga kura ya Ndio, wajumbe 3 kura ya Hapana na wajumbe 2 hawakuonesha msimamo wowote.  

Rais wa Baraza alisema rasimu haikupita kwa sababu wajumbe wawili wa kudumu walipiga kura ya hapana ambayo ni turufu. Wajumbe hao wa kudumu ni China na Urusi.  

Katika upigaji kura wa rasimu ya azimio la iliyowasilishwa na Urusi, Sudan na Venezuela namba S/2023/795 wajumbe 4 walipiga kura ya Ndio, wajumbe 2 kura ya Hapana na wajumbe 9 hawakuonesha msimamo wowote.  

Rais wa Baraza alisema azimio hilo halikupita baada ya kushindwa kupata idadi ya kura zinazotakiwa ambazo ni 9.  

Kufahamu zaidi kuhusu upigaji kura ndani ya Baraza la Usalama bofya hapa.

Kauli kabla ya kupigwa kwa kura  

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield alitetea rasimu yao akirejelea kuwa wiki iliyopita alisema ni lazima Baraza liwezesha Umoja wa Mataifa, Marekani na viongozi wa kanda kufanya kazi yao kufanikisha misaada ya binadamu kufikia wahitaji Gaza, na ndio msingi wa rasimu ya azimio walilowasilisha.  

Balozi Thomas-Greenfield amesema huu ni wakati ambao Baraza liko kwenye mtihani mkubwa.  

Rasimu ya Marekani pamoja na mambo mengine ililaani shambulio la Hamas dhidi ya Israeli Oktoba 7, pamoja na shambulio dhidi ya hospital ya Al Ahli huko Gaza.  

Naye Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vassily Nebenzia amesema hawako tayari kuunga mkono rasimu ya Marekani akidai kuwa haina lengo la kusitisha mapigano. 

Balozi Nebenzia amesema ili Baraza liweze kutekeleza jukumu  lake la kulinda amani na usalama, tumeandaa rasimu bora na hatuoni sababu kwa nini wajumbe washindwe kulipitisha. 

Rasimu mbili kwa wakati mmoja  

Ikumbukwe hii ni mara ya pili ndani ya siku kumi Baraza linazingatia nyaraka mbili shindani kuhusu kinachoendelea Gaza, kufuatia wiki iliyopita ambapo rasimu mbili kuhusu janga hilo zilishindwa kupita barazani.  

Rasimu iliyowasilishwa na Urusi namba (S/2023/772) ilishindwa kupitishwa taehe 16 mwezi Oktoba kwa sababu haikupat kura zinazotakiwa, ilhali rasimu iliyowasilishwa na Brazil (S/2023/773) tarehe 18 Oktoba ilipigiwa kura turufu na Marekani.  

Rasimu ya Urusi ilitaka kukoma kwa mapigano ili huduma za kiutu ziweze kutolewa kwa wahitaji ilihali rasimu ya Brazil ilitaka sitisho la muda la mapigano ili misaada ya kiutu ifikie wahitaji.  

Ingawa wajumbe kwa kiasi kikubwa walikubaliana kuhusu umuhimu wa Baraza kujadili suala hili, majaribio ya kumaliza mgawanyiko mkubwa baina ya wajumbe juu ya mambo yahusianayo na mapigano yanayoendelea bado hayajazaa matunda.