Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani tunisheni CERF ili ifikie lengo la dola bilioni 1- Guterres

Wakimbizi waliorejea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaishi katika eneo la Djako, Kusini mwa Chad, ambako kiwango cha utapiamlo kiko juu sana na wanahitaji msaada mkubwa wa kibinadamu.
© UNICEF Chad/Alliah
Wakimbizi waliorejea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaishi katika eneo la Djako, Kusini mwa Chad, ambako kiwango cha utapiamlo kiko juu sana na wanahitaji msaada mkubwa wa kibinadamu.

Wahisani tunisheni CERF ili ifikie lengo la dola bilioni 1- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameangazia umuhimu wa mfuko mkuu wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi wa dharura katika kufikisha haraka mahitaji ya kimkakati kwenye maeneo yenye majanga duniani kote. Ni kwa mantiki hiyo ametoa wito wa usaidizi zaidi ili mfuko huo uweze kupanuliwa na kufikia lengo lake la dola bilioni 1. 

Akizungumza kwenye mkutano wa kila mwaka wa kutoa ahadi kwa ajiliya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi wa Dharura, CERF uliofanyika Jumatano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Guterres amesema ni dhahiri kuwa Umoja wa Mataifa ni simulizi yenye mafanikio. 

“Mwaka baada ya mwaka, CERF inadhihirisha dhima yake ya kipekee na isiyofidika kwa kuwasilisha fedha kwa watu walio kwenye majanga na mwaka huu si tofauti,” amesema Katibu Mkuu akitaja upelekaji wa fedha nchini Sudan mwezi Aprili na Gaza mwezi Oktoba. 

Mfuko wa Mkuu wa Usaidizi wa Dharura 

CERF ilianzishwa mwaka 2006 kuwezesha kasi ya operesheni za kupeleka na kufikisha misaada ya kiutu kwa  ufanisi kwenye maeneo mbalimbali duniani. 

Ikiwa ni mfuko wa fedha unaochangiwa kutoka kona mbali mbali, CERF inawezesha msaada wa fedha kufikia mahali husika kwa wakati, na kutatua mahitaji ya dharura ya binadamu, ikifanikisha uchambuzi wa haraka, upitishaji maamuzi kwa wakati na utekelezaji ambavyo vyote hivyo vinaokoa maisha na kulinda jamii zilizo hatarini. 

Kwa mwaka huu wa 2023, fedha nyingine zimepelekwa kutatua changamoto  mfano  nchini AFghanistani wakati wa tetemeko la ardhi, Bangladesh wakati wa mafuriko, na ghasia na ukimbizi wa ndani nchini Burkina Faso, ukame Djibouti, janga nchini Haiti na matetemeko makubwa ya ardhi huko Syria na Uturuki. 

CERF kwa ajili ya hatua kwa tabianchi 

Bwana Guterres pia aliangazia suala kwamba CERF pamoja na kujikita kwenye usaidizi wa kibinadmamu, pia inafanikisha hatua kwa tabianchi, kwa kuwezesha ufadhili kwenye hatua za kukabili majanga yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi. 

Akishukuru wahisaji kwa msaada wao, Katibu Mkuu amewaomba waendelee kuonesha ukarimu wao. 

“Tunahitaji ahadi za fedha zinazoendana na kiwango cha mahitaji. Tunahitaji kufikia lengo la dola bilioni 1, lengo ambalo lilikubaliwa miaka 7 iliyopita,” amesema Katibu Mkuu. 

Mfuko wa wote kwa ajili ya wote 

Aidha akizungumza  katika tukio hilo la kutoa ahadi, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinamu, OCHA Martin Griffiths, ambaye anasimamia CERF kwa niaba ya Katibu Mkuu wa UN, ameainisha jinsi mfuko huo ulivyo na athari chanya kwenya maisha ya binadamu, huku akirejelea wito wa Katibu Mkuu wa kutaka ahadi ziongezwe. 

“CERF imethibisha kuwa ni ‘mfuko wa wote kwa ajili ya wote,’ kama ilivyobainishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati ulipoundwa mwaka 2006. Unahitaji kuendelea kutekeleza dhima yake hiyo muhimu,” amesema Bwana Griffiths. 

Akihitimisha, Bwana Griffiths amesema Mfuko huo ni wa kwanza kuchukua hatua wakati wa majanga, “kwa kutoa kiashirio kidogo cha wema na heshima kwa watu waliokumbwa na majanga.”