Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wenu kwetu umekuja wakati muafaka - wanawake Mbau, DRC

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania kikosi cha 10, TANZBATT 10 wakiwa na wanawake wa na eneo la Mbau jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
George Musubao
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania kikosi cha 10, TANZBATT 10 wakiwa na wanawake wa na eneo la Mbau jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Msaada wenu kwetu umekuja wakati muafaka - wanawake Mbau, DRC

Afya

Mgeni njoo mwenyeji apone ni methali iliyodhihirika huko eneo la Mbau jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC baada ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania kikosi cha 10, TANZBATT 10 walipotembelea hospitali ya La Grace kutoa msaada si tu wa chakula bali pia dawa. Walinda amani hawa wanahudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO. 

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda Kikosi cha TANZBATT-10 Luteni Kanali John Peter Kalabaka,  Meja Neema Alfred Neligwa ameongelea juu ya changamoto zinazowakabili wanawake ikiwemo ukatili unaosababisha wapate changamoto za kiafya. 

Aidha Meja Neligwa amekabidhi msaada muhimu wa dawa na chakula katika Hospitali hiyo ya LA GRACE ambayo ulikuwa hitajio lao la msingi.  

Masika Kadiri ni mwakilishi wa wanawake na ni mkazi wa Mbau amefurahi ujio wa walinda amani kutoka Tanzania Kwa kuwaletea msaada wa dawa na chakula kwa wagonjwa na kuwashukuru Walinda amani hao Kwa kuwapatia elimu ya masuala ya wanawake kutokana na magumu wanayopitia. 

“Kwa kweli wagonjwa hawakuwa na chakula kwa hiyo kama hana inabidi aombe cha mgonjwa mwenzake na kama mgonjwa mwenzake hana chakula basi anasalia na njaa,” amesema Bi. Masika. 

Dokta Charles Saad ni Mganga Mkuu wa hospitali ya La Grace na amefurahi ujio wa MONUSCO Mbau akisema msaada wa dawa utaziba pengo la uhaba wa dawa ambao ulikuwa unawakabili. 

Naye Mganga Mkuu wa Msaidizi wa TANZBATT10  Luteni Kembone Johness Kembone amesisitiza kwamba magonjwa mengi yanayowasumbua wakazi wa hapa ni ya ukanda wa Kitropiko kama vile magonjwa ya malaria, kuhara, na homa ya matumbo ambayo kimsingi yanafanana na ya Tanzania.

Taarifa hii imeandaliwa na George Musubao UN News DRC na Luteni Abubakar Muna Afisa Habari TANZBATT-10.