Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Somalia watu 94 wapoteza maisha

Mtoto akinywa maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Mtoto akinywa maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani Somalia

Mafuriko Somalia watu 94 wapoteza maisha

Msaada wa Kibinadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA imesema mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika pembe ya Afrika imesababisha madhara makubwa pamoja na vifo ambapo huko nchini Somalia watu 94 wamepoteza maisha. 

Taarifa iliyotolewa leo na OCHA kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa tangu kuanza kwa msimu wa mvua mapema mwezi Oktoba ambazo zinatarajiwa kuendelea mpaka mwezi Desemba nchini Somalia kumeshuhudiwa mafuriko makubwa ambapo mpaka kufikia hii leo Novemba 29 takribani watu milioni 2 wameathirika, watu 746,000 wameyakimbia makazi yao na wengine 125,600 wamehamishiwa maeneo mengine. 

Utabiri wa hali ya hewa unaonesha katika saa 48 zijazo mvua kubwa itaendelea kunyesha katika eneo la kusini magharibi mwa Somalia. 

Kiujumla wilaya 34 nchini Somalia zimeathiriwa na mvua hizo na takriban nyumba 4,700 zimebomolewa. Maeneo ya Kusini Magaribi mwa nchi hiyo yameathirika huku mikoa iliyoathirika zaidi ikiwa ni Bay (495,600), Gedo (354,900), Juba Kati (280,000), Hiraan (267,000), Mudug (213,300), Juba ya Chini (199,000), na Shabelle ya Kati (103,500).

Misaada inatolewa

Mashirika 145 yanasaidia waathirika wa mafuriko hayo kwa kutoa misaada inayohitajiwa haraka na watu, mengi ya mashirika hayo ni yale yasiyo ya kiserikali. 

Misaada inayotolewa ni pamoja na malazi, vifaa mbalimbali, vitu vya usafi na kujisafi, fedha taslimu, Msaada wa chakula , ulinzi, lishe, elimu ya afya pamoja na uratibu na usimamizi wa kambi zinazohifadhi waathirika wa mafuriko.