Mafuriko pembe ya Afrika yameongeza mahitaji ya kibinadamu-OCHA

29 Oktoba 2019

Kumekuwa na mvua kubwa katika maeneo mengi nchi za pembe ya Afrika katika miezi michache iliyopita na hivyo kusababisha mafuriko na mahitaji ya kibinadamu hususan nchini Ethiopia, Sudan Kusini na Somalia imesema leo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema nchini Ethiopia, mafuriko yameripotiwa katika maeneo ya

 Afar, Amhara, Gambela, Oromia, SNNP na Somali huku yakifurusha watu 220,000 na kusababisha uharibifu wa mali na vyanzo vya kipato. Takriban watu nusu milioni ka ujumla wameathiriwa na mafuriko ya hivi majuzi.

OCHA imesema nchini Sudan Kusini, mafuriko ya msimu tangu Julai imeathiri zaidi ya watu 900,000 ikiwemo wakimbizi wa ndani, wakimbizi na jamii zinazowahifadhi huku mvua zikitarajiwa kuendelea kwa wiki zingine nne au sita na huenda zikahatarisha watu wengine.

Bwana Laerke ameongeza, “tunatarajia kwamba kutakuwa na uharibifua wa mazao na ardhi na mifugo. Katika maeneo mengi kunakoshuhudiwa mafuriko zaidi ya watu milioni tatu walikuwa wanahitaji msaada kabla ya mvua na asilimia sitini ya kaunti kunakoshuhudiwa mafuriko zimetajwa kuwa na utapiamlo uliokithiri”.

Nako nchini Somalia mvua zilizoanza mapema zimesababisha kuongezeka kwa maji katika mito ya Juba na Shabelle na kusababisha mafuriko Hirshabelle, Jubalanda na majimbo ya kusini maghairbi. Msemaji huyo wa OCHA amesema, “ndani na karibu mji wa Belet Weyne karibu na mpaka wa Somalia na Ehtiopia, takriban watu 164,000 wamefurushwa huku wengi wakihamia maeneo ya juu. Aidha OCHA imesema imepokea ripoti za watu watatu ambao walizama, miundombinu ya kilimo na barabara vimeharibiwa na vyanzo vya kipato vimesambaratishwa katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa sana”.

OCHA katika kukabiliana na hali hiyo imechukua hatua kama anavyosema Jens Laerke, “Katika nchi zote tatu, Umoja wa Mataifa na wadau wa misaada ya kibinadamu wanaimarisha juhudi katika maeneo yaliyoathirika kwa kusambaza maji, chakula, makazi, huduma za afya na huduma zingine za kuokoa Maisha. Lakini kama ilivyo mara nyingi ufadhili ni changamoto, nchini Sudan Kusini kwa mfano Umoja wa Mataifa na wadau wanahitaji kwa haraka dola milioni 35 kwa ajili ya kuimarisha msaada.”

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud