Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 36 ya TAMWA: Bang style ilisaidia kupigania usawa wa kijinsia Tanzania

Wanachama wa TAMWA katika maadhimisho ya miaka 36 ya chama hicho nchini Tanzania.
UN News
Wanachama wa TAMWA katika maadhimisho ya miaka 36 ya chama hicho nchini Tanzania.

Miaka 36 ya TAMWA: Bang style ilisaidia kupigania usawa wa kijinsia Tanzania

Wanawake

Miaka 36 ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini Tanzania, TAMWA imeonesha ni kwa jinsi gani ujumuishaji wa wanaume kwenye harakati za kutokomeza ukatili wa kijinsia umefanikisha malengo ya kuanzishwa chama hicho ya kutumia kalamu kuleta mabadiliko chanya. 

Hayo yamesemwa na mmoja wa wanaume walioshiriki kwenye harakati hizo na Mwandishi wa habari mkongwe nchini Tanzania, Selemani Mkufya wakati akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa wakati huu dunia ikiwa kwenye kipindi cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

“Wakati TAMWA inaanzishwa mwaka 1987, kulikuwa na vitendo vingi sana vya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na vitendo viovu dhidi ya wanawake na watoto mfano vipigo na watoto wadogo kunajisiwa sasa TAMWA ilivyokuja ikasema hapana hivi kitendo havifai tuviache.," amesema Bwana Mkufya.

Lakini Mkufya anaeleza ili kufikisha ujumbe huo TAMWA ilikuwa na mikakati bora ya kufanya uanaharakati katika kufanikisha mambo yake.

“TAMWA ilivyoanza, ilianza kwa kushirikisha wanaume katika shughuli zake, kwahiyo wanaume walikuwa ni sehemu ya kuanzishwa kwa TAMWA na wakawa wanakwenda katika shughuli za TAMWA katika maeneo ambayo kwa mfano kulikuwa na ukeketaji na vitendo vibaya dhidi ya wanawake na watoto na hii ilikuwa nzuri sababu ilikuwa vita ya waandishi wote.”

Wanawake waliopokea mafunzo yaliyotolewa na chama cha wanahabari wanawake Tanzania, TAMWA kuhusu kuweka na kukopa.
UN News/ Assumpta Massoi
Wanawake waliopokea mafunzo yaliyotolewa na chama cha wanahabari wanawake Tanzania, TAMWA kuhusu kuweka na kukopa.

Bang style

Suala jingine lililogusiwa na Bwana Mkufya katika mazungumzo yake maalum na Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na mchango wa TAMWA katika nchi yao ni namna ya walivyokuwa wakitoa taarifa zao za kupinga ukatili wa kijinsia.

“TAMWA ilianzisha dawati linaloitwa BANG STYLE ambapohabari zinaandikwa an zinapewa mwelekeo wa kihabari mmoja wenye maana na kutangazwa katika vyombo vyote vya Tanzania kwa wakati mmoja na mhariri wake nilikuwa mimi (Selemani Mkufya) na tulifanya kazi hiyo kwa moyo mkunjufu kabisa kuhakikisha kwamba vitendo vya ukatili, unyanyasaji na uonevu vinakomeshwa kupitia habari.” 

Mbali na kuandika habari shirika hilo lilikuwa na vituo ambapo watu walikuwa wakiedna kutoa ushuhuda kuhusiana na vitendovya kifedhuli walivyokuwa wakifanyiwa na kisha wakawa wanakusanya maoni ya watu na matokeo yake mambo mengi yalifichuliwa.

“Kiukweli TAMWA imefanya vitu vingi sana ambavyo kitaifa mpaka leo imeheshimisha nchi yetu ya Tanzania.” 

Kuongeza wanawake ndani ya vyumba vya habari

Naye mwenyekiti wa Bodi ya TAMWA Joyce Shebe anasema mbali na kuwashirikisha wanaume lakini chama hicho pia kilisaidia kuongeza idadi ya waandishi wa habari wanawake katika vyumba vya habari na pia katika nafasi za uongozi ndani ya vyumba vya habari. 

“Tulikuwa na lengo la kuhakikisha sauti za wanawake, vijana na watoto zinapewa nafasi katika vyombo vya habari na pia kuhakikisha kuna mgawanyo sawa wa majukumu ndani ya vyombo vya habari na matokeo yake hivi sasa kuna viongozi wengi wanawake katika vyombo vya habari Tanzania.” Alisema Bi. Sheba.

Sheria ya SOSPA

Shirika hilo pia lilikuwa linafanya kazi na wadau mbalimbali ikiwemo serikali, Bunge na jeshi la polisi katika kuleta matokeo ya harakati zao.

“Tulikuwa tunafanya nao kazi katika harakati za kuhakikisha uwepo wa sheria na sera mbalimbali zinazotambua usawa kwa wanawake na walitusikiliza na kushirikianaa nasi katika kutengeneza mazingira ambayo kweli unaweza kusema taifa letu linazingia usawa wa kijinsia.” 

Moja ya sheria ambazo waliweza kushirikiana na serikali na kuhakikisha zinatungwa ni Sheria ya Makosa ya Kujamiiana kwenye suala la ubakaji au SOSPA ya mwaka 1998 ambayo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Lengo la sheria hiyo ni kukomesha vitendo vya ubakaji kwa watoto chini ya miaka 18 na wanafunzi, ambapo pale mtuhumiwa akikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela na kesi ikihusisha watoto wenye chini ya umri wa miaka 10 mtuhumiwa akikutwa na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha jela. 

Kikao cha kila wiki cha wanakikundi cha Mwanzo Mgumu kilichoko Zanzibar, Tanzania. (Maktaba)
UN/Assumpta Massoi
Kikao cha kila wiki cha wanakikundi cha Mwanzo Mgumu kilichoko Zanzibar, Tanzania. (Maktaba)

Ushirikiano wa TAMWA na UN

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa nayo yamekuwa yakifanya kazi na TAMWA katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii nchini Tanzania.  

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben ametaja mashirika mbalimbai ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi

UNFPA, linalohusika na masuala ya wamawale - UN WOMEN na lile la Elimu Sayansi na Utamaduni -UNESCO katika kuleta usawa wa kijinsia ndani ya jamii.

“Tumefanya kazi na UNFPA katika kupinga ukatili wa kijinsia na kueleza athari za ukeketaji. UN WOMEN tumefanya nao kazi kuhusu wanawake na uongozi, masuala ya uongozi kwenye siasa na maeneo mengine na UNESCO tumefanya nao kazi katika kutoa elimu ya ulinzi kwa waandishi wa habari pale wanapokuwa katika majukumu yao na nje ya majukumu yao ya uandishi wa habari.”

Mafunzo yanayofadhiliwa na mashirika mbalimbali kupitia TAMWA hayatolewi kwa wanahabari wanawake pekee bali pia wanaume mmoja wa wanufaika ni Joseph Sabinus mratibu wa gazeti la Habari leo Afrika Mashariki. 

“Tumefundishwa mambo mengi sana ambayo yametusaidia kuelewa na kuchanganua kuhusu suala la haki na ukatili wa kijinsia.” 

Bwana Sabinus amesema miongoni mwa mambo ambaye yamemsaidia yeye binafsi ni pamoja “badala ya kudhani kwamba harakati za usawa wa kijinsia ni uadui kutoka kwa wanawake dhidi ya wanaume mimi na wengine wengi tumefahamu kwamba hizo ni jitihada zinazo hitaji ushirikishwaji wa wanaume hili ni jambo kubwa sana ambalo nimejifunza na najitahidi sana kupitia maandishi yangu nizidi kueleesha watu wengi.”

TAMWA inatumia siku mbili tarehe 28 na 29 Novemba 2023 kufanya maadhimisho ya miaka 36 tangu kuanza kwa shughuli zake maadhimisho yanayofanyika jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na mgeni rasmi ni Rais w anchi hiyo Samia Suluhu Hassan.