WHO yazindua Programu ya wahudumu wa afya kuweza kujifunza namna ya kuwasaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia
WHO yazindua Programu ya wahudumu wa afya kuweza kujifunza namna ya kuwasaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia
Wahudumu wa afya mara nyingi ndio watu wa kwanza na wakati mwingine watu pekee ambao mamilioni ya wanawake na wasichana hukutana nao pale wanapofanyiwa vitendo vya kikatili. Wakipatiwa ujuzi unaohitaji, wahudumu wa afya ni watu muhimu katika kuwapatia usaidizi wa kuokoa maisha.
Kuelekea Siku ya kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana tarehe 25 Novemba, ambayo pia ni siku ya kwanza ya siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia (Novemba 25 – Desemba 10) Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limezindua programu mpya ya mafunzo ya kielektroniki iliyotengenezwa rasmi lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa wafanyakazi wa afya kutambua na kusaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia.
Kwa mujibu wa WHO mwanamke 1 kati ya 3 yupo kwenye hatihati ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia na mwenza wake na ndio maana mwaka huu katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kampeni imeelekezwa katika hitaji muhimu la kuzuia hali hii kutokea.
Kozi hii ambayo wahudumu wa afya wataweza kusoma kupitia simu za rununu, kampyuta mpakato na tablet inatolewa bure itawajengea uwezo na kuwapatia ujuzi wa kuwatunza waathirika wa ukatili wa kijinsia waliofanyiwa na wenza wao.
Ikiwa imegawanyika katika mafungu sita, kozi hii ya mtandaoni itawapa wanafunzi nyenzo za kujisomea, kutakuwa na picha mnato, watakuwa na mazoezi ya kufanya, mifano ya kesi zilizowahi kutokea na mwisho watafanyiwa tathmini na kupatiwa cheti.
Ikumbukwe kuwa kozi hii ni nyongeza ya kozi ambayo tayari ipo yenye mtaala wa ana kwa ana na imekuwa ikitumika kwa wanafunzi kujifunza na hivyo hii mpya ya mtandaoni itakuwa ni nyongeza.
WHO imesisitiza kuwa ni jukumu la kila raia kutovumilia kabisa ukatili wa kijinsia. Kila mhudumu wa afya kuwa na huruma, kutoa huduma, matunzo na usaidizi kwa waathirika na kwa Serikali, kufadhili, kulinda na kujenga muitikio wa changamoto za ukatili.
WHO imesema katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wanatarajia kuzindua nyenzo zingine za kusaidia kukabiliana na hali hiyo ndani ya jamii.