Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GBV Taarifa, programu tumishi ya kukabili ukatili wa kijinsia Tanzania

Uzinduzi wa apu ya simu ya kiganjani ya kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia, Tanzania.
UN Tanzania/Laurean Kiiza
Uzinduzi wa apu ya simu ya kiganjani ya kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia, Tanzania.

GBV Taarifa, programu tumishi ya kukabili ukatili wa kijinsia Tanzania

Haki za binadamu

Tanzania shirika la kiraia linalohusika na masuala ya msaada wa sheria na maendeleo kwa wanawake, WiLDAF kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia, Dephics wametengeneza programu tumishi iitwayo GBV Taarifa inayowezesha mtu kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kupitia simu ya kiganjani.  

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Akson akizindua programu hiyo tumizi GBV Taarifa jijini Dar es salaam nchini Tanzania wakati huu wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia,  tukio ambalo liliandaliwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Tanzania na wadau wengine. 

Wildaf ilibuni wazo na kisha Dephics wakatengeneza programu tumishi hii ambayo kwa sasa inafanya kazi kupitia simu Janja au Smart Phones na mtumiaji anapaswa kupakua kutoka Play Store au Apple Store.  

Nikamuuliza Josephat Mandara, Mkurugenzi Mtendaji wa Dephics inafanyaje kazi ? “Akiwa tu na hii programu tumishi kwenye simu  yake, tumeweka moja kwa moja kitufe kimeandikwa Dharura au Toa Taarifa Bonyeza Hapa. Akibonyeza pale atapata fursa ya kutoa taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi au atapiga simu, na taarifa hizo zinapokelewa au zinataratibiwa na taasisi ya WiLDAF wao watazipokea. Tumewatengenezea pia mfumo wa kuwawezesha kuzitoa hizo taarifa wanapozipokea kuelekea sehemu husika kama madawati ya kijinsia, au kama kitu kinatakiwa kipitie vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa hiyo taarifa ya kwanza inawafikia wao na halafu wanasambaza kulingana na tukio ambalo mtu ameripoti liko katika upande upi.” 

Na vipi wakazi wa vijijini? “Kwa sasa hivi hao watu hawataweza kufikiwa na hiyo programu tumishi. Lakini ni kitu ambacho tupo kwenye mchakato. Kwa sababu tuliangalia sehemu gani rahisi ya kuanzia, tukaanzia na simu janja, lakini ni mchakato ambao upo kabisa tunatengeneza kitu cha kuwasaidia. Kuna mfumo unaitwa USSSD unakuwa unabonyesha Nyota namba fulani alama ya reli, utaingia kwenye menú utafuata taratibu za kutoa taarifa. Lakini pia mbali na hapo kutakuwa na mfumo ambao ni wa ujumbe mfupi, hata kama mtu hana simu janga, atakuwa anatuma tu taarifa  kama ni ukatili wa kingono kwenda namba fulani na itapokelewa na kuanzia hapo huyo mtu atakuwa anaendelea kupata huduma.”