Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Violah Cheptoo kupitia Tirop’s Angels asongesha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia Kenya

Violah Cheptoo, (wa tatu kushoto) ni mwanariadha wa mbio za marathoni kutoka Kenya ambaye alianzisha taasisi ya Tirop's Angels kwa lengo la kukabili ukatili wa kijinsia baada ya rafiki na mwanariadha mwenzake Agnes Tirop kuuawa mwaka 2021 na mtu aliyemwa…
Tirop's Angels
Violah Cheptoo, (wa tatu kushoto) ni mwanariadha wa mbio za marathoni kutoka Kenya ambaye alianzisha taasisi ya Tirop's Angels kwa lengo la kukabili ukatili wa kijinsia baada ya rafiki na mwanariadha mwenzake Agnes Tirop kuuawa mwaka 2021 na mtu aliyemwamini.

Violah Cheptoo kupitia Tirop’s Angels asongesha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia Kenya

Wanawake

Ulimwengu ukiwa kwenye siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia tunamleta kwako Violah Cheptoo mwanariadha mashuhuri huyu wa kimataifa kutoka Kenya ambaye mwaka 2021 alijikuta akianzisha taasisi ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Tweet URL

Akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mtaifa, mwanariadha huyu akijulikana pia kama Violah Lagat anasema sababu kuu ya kuanzisha taasisi hiyo iitwayo Tirop’s Angels ni kuuawa kwa rafiki na mwanariadha mwenzake Agnes Tirop mwaka 2021.

Kabla ya kuuawa kwake alikuwa amevunja rekodi ya kukimbia mita 10,000 nchini Ujerumani, na wakati tuliporudi nyumbani tulikaa kama wiki mbili hivi tukasikia kuwa amepoteza maisha yake, na tena kwa njia mbaya sana,”  amesema Violah, akiongeza kwa aliuawa na mtu ambaye alimwamini.

Anasema alipata uchungu sana kwani walifanya mazoezi kwa pamoja, walikuwa wanakimbia pamoja na “niliona anaweza kuja kusonga mbele zaidi na hata kushiriki mbio za marathoni au nusu marathoni, nyota yake ilikuwa inang’aa sana.”

Baada ya kuona kuwa Agnes ameuawa kwa dhuluma ya jinsia akiwa na umri wa miaka 25, mambo aliyokuwa anasikia kwa watu wenye umri mkubwa kama dada zake wenye umri wa miaka 40 au 35, “sasa ilipofikia kwa mtu mwenye umri mdogo kwangu, mimi na wenzangu tukaona bora tuanzishe kitu, na tukaanzisha Tirop’s Angels.”

Tirop’s Angels inafanya nini kuzuia dhuluma za kijinsia

Shirika hili lilianzishwa na kubeba ubini wa jina la Agnes, yaani Tirop. Jukumu lao kubwa ni kuelimisha jamii wakiwemo vijana, wanawake na wanaume kuhusu ukatili wa kijinsia. Wanakwenda shuleni, kanisani, kwenye kambi na kuelimisha kuwa ukatili wa kijinsia ni jambo lipo na watu wasiluchukulie mzaha. 

“Kule Afrika dhuluma ya kijinsia inaonekana ni kitu cha kawaida sana. Mfano kama umeolewa na mume wako anakwambia nitakupiga Kofi, au amekupiga Kofi ujue siku moja inaweza kuzidi ifikie hatua ya mtu kukuaa,” amesema Violah.

Taasisi yao pamoja na kuhamasisha manusura wa ukatili kupiga simu polisi na kusaka usaidizi kwenye sheria hilo, inapatia hifadhi wanawake waliokimbia ukatili wa kijinsia, kuwapatia mwanasheria atakayelipiwa na taasisi hiyo, halikadhalika kupatia makazi wakati kesi inaendelea.

Vikwazo kutoka kwa wanaume

Awali wanaume waliona kuwa Tirop’s Angels lilikuwa kundi la wanawake la kuondoa wanawake kwenye familia zao, kwa hiyo taasisi hiyo ikakumbwa na vikwazo kwenye jamii hadi pale wanaume walipobaini kuwa fikra zao hazikuwa sahihi, kwani Tirop’s Angels ilikuwa inahamasisha dhidi ya ukatili wa kijinsi ambao pia unakumba wanaume na watoto wa kiume.

“Hivyo walikuja na tukafanya kazi pamoja, wanaume wamekuja wanaongelesha wanaume wenzao kuwa si vizuri kupigana na mke wako au kudhulumu pia wasichana. Halikadhalika mtu anaweza kupata ushauri nasaha kutoka kwa viongozi wa dini badala ya kupiga mtu,” amesema Violah.

Tirop’s Angels pia wana washauri nasaha kwa walio kwenye ndoa.

Soundcloud

Si kawaida kupigwa au kuitwa maneno dhalili kama mjinga

Ujumbe wa Viola kwa wanawake na wasichana ni kwamba “kupigwa si jambo la kawaida, wala kuitwa mjinga si sahihi. Ukiwa katika hali hiyo tafuta msaada ili usaidiwe na usinyamaze. Sisi tumelelewa kuwa kupigwa ni sawa lakini sasa tumegundua si sawa,”

Amesisitiza kuwa suala la kufikiria jamii au familia watakuona vipi, linapaswa kuepukwa.

Ndoto ya Violah ni kuona sheria inabadilishwa ili ilinde wasichana, wanawake na vijana dhidi ya dhuluma ya kijinsia.