Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP28: WHO yasema afya ipatiwe kipaumbele kwenye mijadala

Mkunga akimhudumia mwanamke mjamzito katika chumba cha kujifungulia katika hospitali moja nchini Sudan Kusini.
© UNICEF/Mark Naftalin
Mkunga akimhudumia mwanamke mjamzito katika chumba cha kujifungulia katika hospitali moja nchini Sudan Kusini.

COP28: WHO yasema afya ipatiwe kipaumbele kwenye mijadala

Afya

Kuelekea mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP28 huko Dubai, Falme za kiarabu tarehe 30 mwezi huu wa Novemba, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, limesema washiriki wanapaswa waelewe kuwa suala la afya ndilo linapaswa kuchochea majadiliano wakati huu ambapo janga la tabianchi linazidi kushamiri duniani kote. 

Dkt, María Neira ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Umma na Mazingira, WHO ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi ya kwamba, “Wajumbe wanapaswa kuelewa kuwa hawajadili tu punguzo la kiwango cha utoaji wa hewa chafuzi kila mwaka, bali wanajadili pia idadi ya wagonjwa wa pumu, idadi ya wagonjwa wa njia ya hewa, idadi ya wagonjwa wa saratani ya mapafu, idadi ya wagonjwa wa magonjwa yanayohusiana na kukabiliana na hewa chafu au madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Wanahitaji kuelewa wanajadili afya yetu vile vile.” 

Dkt. Neira amesema pamoja na hilo, wanataka washiriki pia waelewe kuwa iwapo watachukua hatua sahihi, mathalani kushughulikia visababishi vya mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa na miji isiyo na uchafuzi, nishati safi na endelevu, hatua hizo zitakuwa na manufaa kwa afya ya kila mtu. Ndipo akatolea mfano iwapo hatua sahihi za kukabili tabianchi zikichukuliwa na matunda yatakayopatikana ifikapo mwaka 2030, “Iwapo tunaangalia afya ya umma, ningependa kupunguza kabisa vifo vya watoto wachanga vinavyosababishwa na uchafuzi wa hewa, ambavyo ni watoto milioni 7 hufia tumboni mwa mama zao. Kwa hiyo tukiongeza upatikanaji wa nishati safi, yaani kwa kuwa tu na hewa safi, tunaweza kupunguza vifo milioni 5 kila mwaka.” 

Kwa mujibu wa WHO madhara ya mabadiliko ya tabianchi yamekuwa makubwa zaidi kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, halikadhalika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia na pia nchi za visiwa vidogo. 

Katika mkutano huo wa COP28 kwa mara ya kwanza kutakuwa na Siku ya Afya ambapo washiriki watajikita zaidi kujadili jinsi tabianchi inarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya afya.