Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HABARI KWA UFUPI: COP28, Gaza, Afya

Mtazamo wa jumla ya ukumbi kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP28, kwenye Expo City, huko Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Christopher Pike
Mtazamo wa jumla ya ukumbi kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP28, kwenye Expo City, huko Dubai, Falme za Kiarabu.

HABARI KWA UFUPI: COP28, Gaza, Afya

Tabianchi na mazingira

Katika saa za mwisho za mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 huko Dubai majadiliano yanaendelea kwa matumaini kwamba wajumbe watatoka na makubaliano yatakayoweka ulimwengu kwenye njia ya mustakabali endelevu zaidi. Hata hivyo rasimu ya awali ya makubaliano hayo inaonyesha wito wa kuachana na nishati ya mafuta kiskuku umepewa kisogo, na kusababisha kilio kutoka kwa nchi zilizo katika mazingira magumu ya mabadiliko ya tabianchi na mashirika ya kiraia. 

Kukomeshwa kwa matumizi ya mafuta kisukuku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema ni moja ya funguo za mafanikio ya mkutano huo na ambacho mataifa mengi yamekidai. Lakini badala yake, rasimu ya makubaliano hayo inazitaka nchi kupunguza "matumizi na uzalishaji wa nishati ya kisukuku, kwa njia ya haki, yenye utaratibu na usawa."rasimu ya pili inatarajiwa kujadiliwa baadaye leo.

Gaza

Huko Gaza hali ya kibinadamu inazidi kudororora huku mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yakipaza sauti ya kunusuru maisha ya watu wanaopitia adhabu ya jehanamu duniani. Lile la afya WHO linataka ulinzi na fursa ya kufikisha huduma za kibinadamu, wakati la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA likisema karibu Gaza nzima inazingirwa na kusababisha adhabu ya pamoja kwa zaidi ya watu milioni 2 ambapo nusu yake ni watoto. Na la misaada ya kibinadamu OCHA limesema ingawa wahudumu wa kibinadamu wanafanyakazi bila kuchoka wala kukata tamaa kufikisha misaada , maeneo mengi sasa hayafikiki na hakuna usalama. Na hapa makao Makuu Baraza Kuu leo limeanza tena kikako cha 10 cha dharura kujadili hali ya Gaza.

Afya

Na leo ni siku ya huduma za afya kwa wote mwaka huu ikibeba maudhui “Afya kwa wote , wakati wa kuchukua hatua” Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO Dkt. Tedross Ghebreyesus katika ujumbe wake wa siku hii amesema “Huduma za afya kwa wote inamaanisha kwamba watu wote wanaweza kupata huduma wanazohitaji bila gharama kubwa lakini bado nusu ya watu wote duniani hawana huduma muhimu za afya. WHO ilizaliwa miaka 75 iliyopita kwa Imani kwamba afya ni haki ya binadamu na njia bora ya kutimiza haki hiyo ni huduma za afya kwa wote.”