Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres kwa COP28: Viongozi chukueni kuepusha zahma zaidi kwenye tabianchi

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani kufuatia ziara yake nchini Chile na Antarctica
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani kufuatia ziara yake nchini Chile na Antarctica

Guterres kwa COP28: Viongozi chukueni kuepusha zahma zaidi kwenye tabianchi

Tabianchi na mazingira

Kasi ya kuyeyuka kwa barafu katika ncha ya kaskazini na ncha ya kusini mwa dunia ni mara tatu hivi sasa ya ilivyokuwa miaka ya 1990, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akinukuu wanasayansi aliokutana nao mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake huko Antarctica, ncha ya kusini mwa dunia.

António Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo New  York, Marekani amesema  inashtusha sana kusimama kwenye barafu huko Antarctica na kusikia kutoka kwa wanasayansi jinsi barafu inayeyuka kwa kasi kubwa.

Barafu inayeyuka  kwa kasi kubwa

Takwimu mpya zinaonesha kuwa mwezi Septemba mwaka huu, barafu ya Antarctica ilikuwa na ukubwa wa kilometa za mraba milioni 1.5, eneo ambalo ni dogo kuliko wastani wa kipindi kama hiki cha mwaka, na zaidi ya yote ni kiwango cha chini zaidi kuwahi kufikiwa.

Na akarejelea kauli yake kuwa kitokeacho Antarctica ambayo alielezea kuwa ni jabali lililolala hakisalii huko pekee kwani kinagusa maeneo mengine kwa kuwa dunia imeunganika. 

 Mafuriko na maji yenye chumvi yanaingia mashambani na kuharibu mazao na maji, hivyo kutishia uhakika wa kupata chakula -- António Guterres   Katibu Mkuu - UN  

“Kuyeyuka kwa barafu ya baharini, kuna hatari ya moja kwa moja na maisha ya binadamu na mbinu zao za kujipatia kipato hasa kwa jamii za maeneo ya Pwani,” amesema Katibu Mkuu. 

Mafuriko na maji yenye chumvi yanaingia mashambani na kuharibu mazao na maji, hivyo kutishia uhakika wa kupata chakula.

Fidia za bima kwa makazi hakuna tena kwani chanzo cha uharibifu ni majanga ya asili, huku visiwa vidogo vikizama baharini.

Mienendo ya maji huko Antarctica inasambaza joto, virutubisho na hewa ya ukaa duniani na kusaidia kudhibiti mwelekeo wa tabianchi na hali ya hewa katika kanda mbalimbali duniani.

Hata hivyo amesema kasi hiyo inapungua kutokana na bahari ya kusini kuzidi kuwa na joto na barafu kutoweka na hii ikiendelea italeta janga. Sababu amesema ni dhahiri, matumizi ya nishati kisukuku inayoongeza joto duniani.

Viongozi COP28 vunjeni mzunguko wa uharibifu wa tabianchi

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka kubadili mwelekeo asikihi viongozi watakaoshiriki mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi, COP28 huko Dubai, Falme za kiarabu baadaye wiki hii wavunje mzunguko unaochochea madhara ya tabianchi.

Majibu amesema yanafahamika ipasavyo: Hatua kudhibiti joto lisizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi, kulinda watu dhidi ya zahma za tabianchi, kuongeza maradufu ufanisi wa nishati na kila mkazi wa dunia kutumia nishati safi na salama ifikapo 2030.

Kwa kina hotuba ya  Katibu Mkuu kwa wanahabari iko hapa.